Habari za Punde

TUME YA UCHAGUZI HAIWEZI KUSIMAMAIA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA - MAJALIWA * Asema si jukumu lake kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi haiwezi kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kama ambavyo imependekezwa na baadhi ya Wabunge.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Aprili 9, 2019) Bungeni jijini Dodoma, kwenye mkutano wa 15 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020.

Alikuwa akijibu hoja iliyotolewa kwamba Uchaguzi wa Serikali za Mitaa usisimamiwe na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na badala yake usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Pia waliitaka Serikali ishughulikie jambo hilo mapema ili kuepuka usumbufu unaoweza kutokea.

Akitoa ufafanuzi wa hoja hiyo, Waziri Mkuu alisema Serikali inawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa imani kubwa walioionesha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo ni huru, juu ya utekelezaji wa majukumu yake, na kuona umuhimu wa kuiongezea jukumu la kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Hata hivyo, Waziri Waziri Mkuu alisema, majukumu ya Tume hiyo, yameainishwa katika Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kusimamia Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Hivyo, jukumu la kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa si miongoni mwa majukumu ya Tume kwa mujibu wa Katiba,” alisema.

Katika hatua nyingine, akizungumzia kuhusu uwekezaji kwenye zao la pamba,Waziri Mkuu alisema sekta ya pamba na mnyororo wake wote wa thamani ni sekta ya kipaumbele ambayo mbali na kuwahakikishia soko wakulima na kuongeza kipato chao, uwekezaji katika viwanda vya nguo unatengeneza ajira nyingi kwa vijana hivyo kuinua kipato chao na kuboresha maisha ya watu wengi.

“Kwa kutumia mkakati wa kuzalisha nguo na mavazi mbalimbali (Cotton to Clothing - C2C), Serikali itaendelea kuhamasisha uwekezaji wa viwanda kwa kutumia teknolojia za kisasa za kutengeneza nguo kuanzia kuchakata pamba hadi nguo kwa kuhakikisha kuwa taratibu zote zinafanyika nchini na msisitizo uwe kwenye utengenezaji wa nyuzi,” alisema.

Alikuwa akijibu hoja iliyotolewa kwamba bado zao la pamba halijatumiwa vizuri katika kuongeza pato la Taifa na kuinua maisha ya Watanzania.  Pia Wabunge walitaka Serikali ijizatiti kusimamia uwekezaji kwenye kilimo cha zao la pamba ili kufanikisha utekelezaji wa mkakati wa viwanda vya nguo nchini wa kufikia malengo ya kuwa Taifa lenye uchumi wa kati.  

Wakati huohuo, Waziri Mkuu alisema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi mwaka 2017, ilifanya tathmini ya kina na kuandaa Blueprint ambayo imebainisha masuala yote muhimu yanayokwamisha uwekezaji na kuainisha maeneo yote muhimu yayohitaji kurekebishwa ikiwemo sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia uwekezaji nchini kwa kila taasisi.

Alikuwa akijibu hoja kuhusu umuhimu wa Serikali kufanya tathmini na kuangalia vikwazo vinavyokwamisha harakati za uwekezaji nchini, kutunga sheria mpya, kurekebisha baadhi ya sheria ili kuendana na mahitaji ya Blueprint.

Alisema sambamba na hatua hiyo, huduma zimeimarishwa kwa kuanzisha mifumo ya kielektroniki ambapo wawekezaji wataweza kufanya maombi ya vibali mbalimbali wakiwa popote bila kulazimika kufika kituoni.

“Mifumo hii itaondoa urasimu na kuharakisha utoaji wa vyeti vya uwekezaji, leseni na vibali mbalimbali. Hatua hizi zitapunguza gharama na muda wa mwekezaji kufuatilia vibali na leseni kwa kila taasisi,” alisema.

Alisema, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) hivi sasa kina ofisi saba za kanda ambazo ni Mwanza, Dodoma, Moshi, Kigoma, Mtwara, Mbeya na Dar es Salaam ambazo zimeanzishwa kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wawekezaji.

Bunge lilikubali kupitisha sh. 148,886,523,581/- kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka 2019/2020. Kati ya hizo, sh. 86,290,355,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 62,596,168,581/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Vilevile, Bunge liliidhinisha sh. 124,182,537,600 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo kati ya hizo sh. 116,573,026,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 7,609,511,600/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
 S. L. P. 980,
 41193 – DODOMA,                      
JUMANNE, APRILI 9, 2019.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.