Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein,akiwa katika mahojiano na Mtoto Nabir Mohammed na Ummukurthum kutoka (ZBC TV) wakiwa katika Ukumbi wa Ikulu Zanzibar wakati wa hafla ya kutoa Mkono wa Eid El Fitry kwa Watoto na Wananchi waliofika katika Viwanja vya Ikulu Zanzibar.
MADEREVA wa gari nchini wametakiwa kutoendesha gari zao kwa
mwendo wa kasi na badala yake waendeleze furaha ya Sikukuu ya Id El Fitri kwa
salama na amani ili kuepuka kusababisha ajali zisizo za lazima hasa kwa watoto
wadogo.
Dk. Shein aliyasema
hayo katika mahojiano ya kipindi maalum
cha “Watoto na Mheshimiwa Rais” kinachotayarishwa na Televisheni ya Shirika la
Utangazaji la Zanzibar (ZBC), mahojiano yaliofanyika Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake
Rais Dk. Shein aliwataka madereva wa gari kuzingatia sheria, kanuni na taratibu
za barabarani hasa katika kipindi hichi cha Sikukuu na kuacha kuendesha gari kwa
mwendo wa kasi ili kuepusha ajali kwa watu wanaopita barabarani wakiwemo watoto
wadogo.
Aliongeza kuwa katika
kipindi hichi cha Sikukuu kwa kawaida barabara huwa zinatumiwa na watu wengi
wakiwemo watoto wadogo ambao wanahitaji uangalizi mkubwa wakati wakitembea
barabarani hivyo, aliwanasihi madereva kuwa makini wanapoendesha gari zao.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa Zanzibar hivi sasa gari zimekuwa nyingi hivyo, ni vyema watoto wakachua
hadhari kwa kujikinga wenyewe sambamba na kuwa makini katika kutembea
barabarani. “muwe waangalifu na muepushe kupisha gari kwa vipega ni hatari ” alisisitiza
Alhaj Dk. Shein.
Aidha, Rais Dk. Shein
aliwataka watoto kusikiliza nasaha za wazazi wao kwani wamewazaa na wanaendelea
kuwalea hivyo ni vyema wakawa wasikivu hasa katika kipindi hichi cha Sikukuu
pale wanapoambiwa kurudi mapema wafanye hivyo pamoja na kuvaa vizuri kama
ilivyo desturi yao katika kipindi hichi cha Sikukuu.
Alhaj Dk. Shein aliwataka
watoto kutambua kuwa hakuna watu wazuri tu katika mitaa yao bali pia, kuna na
watu wabaya hivyo, ni vyema wakazingatia nasaha za wazazi wao pamoja na nasaha anazowapa
yeye kwa upande wake huku akiwasisitiza kurudi nyumbani mapema ili kujiepusha
na vitendo viovu katika kipindi hichi cha Sikukuu.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein pia, aliwataka wazazi kwa upande wao kuendelea kuwalea, kuwatunza na kuwaamuru watoto wao maneno mazuri pamoja
na watoto wa majirani zao kwani nao pia ni watoto wao huku akiwataka kuzidisha
urafiki miongoni mwao kwani Uislamu unasisitiza hivyo.
Aliwanasihi watoto
kuzingatia nasaha za wazazi na wazee wao na kuwataka wasivuke mipaka katika kufurahia
sikukuu hiyo ya Id El Fitr.
Dk. Shein pia, alieleza
kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi nyingi
katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati iliyotoa wanazuoni kadhaa, hapo
siku za nyuma ambapo pia, watu wengi kutoka ukanda huo walikuja kusoma elimu ya
dini ya Kiislamu Zanzibar.
Hivyo, Rais Dk. Shein
aliwataka Vijana waendelee kusoma zaidi elimu ya dini ya Kiislamu ili wafike
hatua waliyofika wazee wao hapo siku za nyuma.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza miongoni mwa faida za funga kiafya na kueleza kuwa wataalamu
wa afya waliobobea walifanya utafiti wa kuthibitisha ukweli kwamba funga ya Ramadhani
inaimarisha afya kwa kiasi kikubwa kwa mtu aliefunga.
Alieleza kuwa kiafya
miili yote inahitaji mazoezi hivyo ipo haja ya kufanya mazoezi kwani bila ya
kufanya mazoezi mwili hubaki na mafuta mengi ambayo hatimae kusababisha maradhi
kadhaa yakiwemo maradi ya moyo na kisukari.
Alisisitiza kuwa
kuna haja ya kufanya mazoezi kwani watu
walio wengi wanaona maradhi ya moyo na sukari yako mengi hivi sasa lakini hiyo
imekuja kutokana na watu wengi kujiangalia afya zao kinyume na ilivyokuwa hapo
siku za nyuma lakini hata hivyo, maradhi hayo yalikuwepo tokea zamani.
Alhaj Dk. Shein pia,
alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa vijana wa Zanzibar wanaoshiriki mashidano
ya kuhifadhi Qur-an na kupata nafasi za juu katika mashidano hayo yanayofanyika
ndani na nje ya nchi na kuweza kuijengea sifa nchi yao kama ilivyokuwa
hapo siku za nyuma.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment