Habari za Punde

SERIKALI YA TANZANIA YAJIPANGA KUTEKA SOKO LA WATALII CHINA


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akizungumza jambo na Viongozi wa  Chuo cha Mafunzo ya kigeni na Utalii  cha nchini China kijulikanacho kwa jina la JXCFFS mara baada ya kuwatambulisha wageni hao  Bungeni Dodoma  leo  waliokuja nchini kwa lengo la  kuwajengea uwezo wa mafunzo  watumishi na wadau wa utalii nchini






Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema kwa sasa muelekeo wa soko la Utalii nchini umelenga kupata watalii wengi kutoka nchini China na kama Wizara inayoshugulikia masuala ya Utalii,  suala la  kujifunza lugha ya kichina kwa baadhi ya watumishi na wadau wa utalii ili kuteka soko hilo ni jambo lisiloepukika.
Imesema nguvu nyingi kwa sasa zinaelekezwa nchini China hivyo  ni muda muafaka wa kuandaa timu ya wataalamu mbalimbali wakiwemo  waongoza watalii watakaoweza kuzungumza lugha ya kichina ili kuweza kulimudu soko hilo.
Hayo yamesemwa leo  jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu  wakati alipokuwa akizungumza na Viongozi wa  Chuo cha Mafunzo ya kigeni na Utalii  cha nchini China kijulikanacho kwa jina la JXCFFS
Amesema  lengo mkutano huo ni  kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya
China na Tanzania katika suala la kuwajengea uwezo watumishi na wadau wa Utalii nchini.
Mkutano huo  umehudhuriwa na ujumbe kutoka China ukiongozwa na Makamu wa Chuo hicho,Prof.Xiong Nanyong,Kaimu huku kwa upande wa Wizara  Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw.Lucius Mwenda pamoja na ya wajumbe wa Menejimenti ya Wizara.
Amesema ni muhimu kwa watumishi wa wizara pamoja na wadau wa utalii kujiandaa ili kuweza kuzungumza lugha ya kichina badala ya vifaa maalum vya kutafsiri lugha ilhali kuna uwezekano kwa Watanzania kujifunza.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Xiong Nanyong amesema wamejipanga kutoa mafunzo mbalimbali likiwemo suala la lugha ya kichina pamoja na utalii ili kuwajengea uwezo Watumishi hao
Ameongeza kuwa tayari wameshaomba kibali kutoka Ofisi ya Rais Utumishi wa umma na Utawala Bora  kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo nchini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Lucius Mwenda  ameahidi kutoa ushirikiano kwa Uongozi wa Chuo hicho ili  kujengeana uwezo  baina ya Serikali ya  Tanzania na China.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.