Habari za Punde

Timu ya wavu ya Polisi yatwaa tena ubingwa wa michuano ya Jembe Mirijiam jijini Mwanza

NA MWAJUMA JUMA
MAAFANDE wa timu ya  Polisi ya mpira wa Wavu Zanzibar wametetea vyema taji lao kwa kufanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Jembe Mirijiam yaliyomalizika juzi mkoani Mwanza.

Polisi ambao wanakuwa mabingwa mara mbili mfululizo katika mashindano hayo ilifanikiwa kutwaa ubingwa huo kwa kuifunga Mara seti 3-2 katika mchezo wa fainali uliojawa na ushindani.

Katika mchezo huo miamba hiyo ilidiriki kucheza hadi seti tano kufatia kutoka sare 2-2 na kuongeza seti ya tano ambapo Polisi iliibuka na ushindi na kutawazwa tena ubingwa huo.

Polisi ambao walidhamiria kuibuka na ubingwa huo kwa mara ya pili mfulilizo licha kuonekana mashindano hayo ni magumu lakini walijitahidi kuhakikisha wanavuka milima na mabonde mpaka kufikia lengo lao.

Katika  seti hiyo ya tano upinzani ulizidi kuwa mkali zaidi ya seti zote ambayo ilimalizika kwa Polisi kuwa na pointi 15 na wapinzani wao ambao ndio wenyeji wa mashindano hayo kupata pointi 13.


Itakumbukwa kwamba Polisi ilifikia hatua ya fainali baada ya kuifunga Sauti ya Mwanza wakati Mara iliifunga Pentagon ya Arusha

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Kocha wa timu hiyo Ali Moahmmed alisema kuwa michuano hiyo haikuwa rahisi kama inavyoonekana ambapo katika hatua ya makundi waliweza kufungwa mchezo mmoja ambao haukuwavunja moyo na kuendelea kupambana.

‘Tulifungwa katika makundi lakini sasa tumeshinda katika fainali na kutwaa ubingwa haya ndio matarajio yangu ambayo kama mwalimu najivunia sana”, alisema.

Hata hivyo alisema kuwa anashukuru kuona vijana wake wamejituma na kupata ubingwa huo ambao umewadhihirishia kulinda heshima ya jeshi hilo.


Zanzibar katika michuano hiyo ilishirikisha timu mbili ambapo timu ya pili Nyuki huku kocha huyo wa timu ya Polisi akichaguliwa kuwa kocha bora wa mashindano hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.