Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kupiga Vita Vitendo Vya Udhalilishaji wa Kijinsi

Na. Mwanajuma Juma. 
Wanaharakati wanaopambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia wamepinga kauli ya Mwakilishi wa Jimbo la Chaani Mhe.Nadir Abdulatif aliyetaka watu wanaofanya mapenzi ya jinsia moja ''mashoga'' kutimuliwa kazini au wasipewe nafasi ya kuajiriwa.

Mwenyekiti wa kamati ya kupinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia Ndg.Nassor Hamad Omar akizungumza na waandishi wa habari,alisema kauli iliyotolewa na mwakilishi huyo ni ya ''kibaguzi'' ikiwa na lengo la kuwavunja moyo vijana wa aina hiyo ambao wengine tayari wamefanikiwa kurekebisha tabia zao.

Alisema vijana wanaofanya vitendo vya mapenzi ya jinsia moja hawakupenda kuwa hivyo,lakini hayo ni matokeo ya ushawishi kutoka kwa jamii ambayo ni sehemu ya ukatili wa kijinsia.

Alisema wameanza harakati za kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia tangu mwaka 2013 kupitia Jumuiya ya Maimamu na kuyakabili makundi hayo ambapo mafanikio makubwa yamepatikana.

Aliyataja mafanikio yaliyopatikana ikiwemo baadhi ya vijana waliokuwa wakijishughulisha na vitendo hivyo kuacha na kurudi katika jamii ya familia zao kama zamani.

''Kauli za kutowaajiri Serikalini au kuwafukuza kazi sio nzuri kwani huko ni sawa na kuwavunja moyo au kuwatenga katika jamii....sisi tunafanya ushawishi wa kurekebisha tabia zao na kurudi katika familia na jamii kama zamani''alisema.

Mmoja ya Kijana ambaye alikuwa akifanya vitendo vya ushoga na sasa kuachana navyo na kurudi katika jamii ambaye hakupenda kutaja jina lake alimpongeza mkuu wa mkoa wa mjini magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud kwa juhudi zake za makusudi za kuwashawishi makundi hayo kuachana na vitendo hivyo.

Alisema nasaha pamoja na ushawishi huo kwa kiasi kikubwa umesaidia kujenga imani na kuweza kuacha vitendo hivyo na sasa kukubalika katika jamii huku wengine wakiajiriwa katika sekta mbali mbali.

''Kinachoharibika hakitupwi......hutengenezwa na sisi tulikuwa tumejiingiza katika vitendo ambavyo havikubaliki katika jamii si kwa hiari yetu na sasa tumerudi katika jamii''alisema.

Hivi karibuni akichangia bajeti ya Wizara ya Afya,mwakilishi wa jimbo la Chaani Nadir Abdulatif alitaka watu wanaofanya mapenzi ya jinsia mmoja wasiajiriwe katika utumishi wa umma kutokana na tabia yao ya jeuri na dharau.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.