Habari za Punde

Elimu ya Juu Ina Mchango Kwa Taifa Kuzalisha Wataalamu Wengi.


Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa akiongea na wageni waalikwa wakati wa uzinduzi wa safari ya miaka mitano ya Chuo Kikuu cha Mt. Augustino cha Tanzania (SAUT) kuelekea Jubilei ya miaka 25 tangu kuanzishwa hicho mwaka 1998. 

Na Eleuteri Mangi-SAUT
Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT) kimezindua safari ya miaka mitano kuelekea Jubilei ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1998.
Uzinduzi huo umefanywa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa uliofanyika chuoni hapo kwa kuweka jiwe la msingi katika jengo la ukumbi wa mikutano unaojengwa kutumika kwa shughuli mbalimbali za kitaaluma na kijamii.

Akiongea na hadhira ya viongozi mbalimbali, wahadhiri, wanafunzi pamoja na wananchi waliohudhuria  katika tukio hilo liliotanguliwa na ibada ya misa takatifu iliyongozwa na Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha SAUT na Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita Askofu Flavian Kassala, Rais Mstaafu Mkapa amesema kuwa vyuo vikuu vya binafsi vinamchango mkubwa nchini katika kutoa elimu kwa Watanzania bila kujali dini zao wala makabila yao hatua ambayo itawaweze kutoa mchango katika kutekeleza Sera ya Maendeleo ya Taifa ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Kuhusu Sera ya Maendeleo ya Taifa, Rais Mstaafu Mkapa amesema kuwa elimu ya juu ina mchango kwa taifa kwa kuzalisha wataalam wengi wenye ubora, ujuzi na uwezo wa kutatua matatizo ya jamii, kukabiliana na changamoto za maendeleo ili kufikia ushindani katika ngazi za kikanda na za kimataifa.

“Serikali inatambua na inathamini mchango wa sekta binfsi katika vyuo vikuu kwa kutoa elimu nchini, vyuo vikuu binafsi vina nafasi ya kuzalisha wataalamu mbalimbali kwa manufaa kwa mtu mmoja mmoja, jamii, taifa na hata nje ya mipaka ya Tanzania.” amesema Rais Mstaafu.

Katika kukuza na kupanua wigo wa kutoa elimu ya juu nchini, Rais Mstaafu Mkapa atakumbukwa kwa mchango wake wa kuwezesha dini mbalimbali nchini kuwa na vyuo vikuu vyake ikiwemo Chuo Kukuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) kinachomilikiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro (MUM) kinachomilikiwa na Kinachomilikiwa na Baraza la Waislam Tanzania, Chuo Kikuu Cha Mt. John Dodoma kinachomilikiwa na Kanisa la Waangikana Tanzania, Chuo Kikuu cha Tumaini kinachomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania pamoja na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Sebastian Kolowa.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha SAUT na Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita Askofu Flavian Kassala ameishukuru Serikali ya Tanzania kuwa msaada kwa kwa sekta binafsi ambapo baraza hilo linathamini na linaiunga mkono Serikali kwa kutoa elimu nchini ili wanaoipa waweze kutoa msaada kwa watu wanaohitaji msaada huo kwa wakati.

“Kanisa linatoa shukrani kwa Serikali, watu binafsi na taasisi zinazoendelea kutoa mchango kwa SAUT, elimu tunayotoa katika ngazi zote imewasaidia watu kutatua matatizo katika mazingira yao” amesema Askofu Kassala.

Aidha, Askofu Kassala aliendelea kusema “Tunajenga watu ambao wanazingatia maadili na utu wa mtu kwa kusaidia jamii inayohitaji msaada kutoka kwa watu ambao wamepata elimu, SAUT inamchango mkubwa katika kuwajenga na kuwalea watu kiroho na kimwili kupitia elimu” alisisitiza Askofu Kassala.

Naye Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Balozi Prof. Costa Ricky Mahalu amesema chuo chao kinaendelea kuzalisha wataalam kwa kwa ajili ya nchi hatua ambayo amemshukuru Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kuwa mlezi na msaada mkubwa kwa maendeleo ya SAUT.

Balozi Prof. Mahalu amesema kuwa wataalamu wanaoandaliwa katika chuo hicho watokana na vitivo vingine vinne (4) ambavyo ni Kitivo cha Sayansi ya Jamii na Mawasiliano ya Umma, Kitivo cha Biashara na Utawala, Kitivo cha Ualimu, Kitivo cha Sheria na Kitivo cha Uhandisi.

Hatua hiyo imeungwa mkono na Waziri wa Madini Dotto Biteko ambapo alitoa wito kwa Wanzania na wanafunzi wanaosoma na wanaotarajia kujiunga na chuo hicho kuwa katika utoaji wa elimu ya juu SAUT imejipambanua kuwa ni kinu cha kuandaa wanataaluma na viongozi mbalimbali nchini.

“Tunabahati ya kuzaliwa kwenye nchi yenye usawa na haki, SAUT inatoa haki ya elimu kwa vijana wetu hatua inayowapelekea kuhama kwenye taifa la kulalamika na kuwa taifa la watu wa matokeo, tunathamini kazi inayofanywa na chuo hiki ambacho kimekuwa kuwa chachu ya malezi kwa kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.” Alisisitiza Waziri Biteko.

Chuo Kikuu cha SAUT kinamilikiwa na kusimamiwa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kimeanzishwa kwa mujibu wa sheria za nchi na kinafanya kazi chini ya Tume ya vyuo vikuu Tanzania (TCU) kwa mujibu wa masharti ya vyuo vikuu sheria namba 7 ya mwaka 2005 ambapo awali kilikuwa kinajulikana kama Chuo cha Maendeleo ya Jamii Nyegezi (NSTI) kilichoanzishwa tangu mwaka 1960 na wamisionari wa kanisa katoliki ambao kwa sasa wanajulikana kama Wamisionari wa Afrika wakiwa chini ya Askofu Joseph Blomjous  wa Jimbo Kuu la Mwanza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.