Habari za Punde

Vijana Wilaya ya Magharibi B Unguja Watakiwa Kuchangamkia Fursa

Na Takdir Suweid. Maelezo Zanzibar.
Vijana nchini wametakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ili kuweza kufikia malengo ya kujikwamua na tatizo la umasikini katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa na Katibu wa Baraza la Sanaa,Sensa na Filamu Zanzibar Dkt.Omar Abdallah Adam wakati alipokuwa akifunguwa Mafunzo ya siku mbili kwa Baraza la Vijana Shehia ya Pangawe,Mafunzo ambayo yamefanyika katika ukumbi wa Skuli ya Msingi Kijitoupele Wilaya ya Magharibi B.
Amesema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuwasaidia Vijana kufikia malengo ya kujikwamua na tatizo la umasikini ikiwemo kuanzisha Mfuko maalum wa Khalifa Found hivyo ni vyema kwa Vijana hao kuandaa Miradi itakayokubalika na kupatiwa Mitaji ya kukuza Uchumi wao na Taifa kwa Ujumla.
Aidha amewataka Vijana hao kufuata Misingi na taratibu za nchi zilizowekwa ili kuweza kujuwa Wajibu wao katika kutetea,kulinda na kujenga nchi yao.
Hata hivyo amewataka kutii maelekezo wanayopewa na Viongozi wao ili kuepuka kutumiwa vibaya na baadhi ya Watu wasiopenda maendeleo ya Zanzibar.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Shehia ya Pangawe Mtumwa Suleiman Mnoga amesema lengo la kuandaa Mafunzo hayo ni kuwajenga Vijana kuwa Wazalendo wa nchi yao katika kuilinda kuitumikia na kuwaomba kushirikiana ili kuweza kufikia malengo yaliopangwa na Serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.