RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar Awamu ya Saba ina dhamiria kuendeleza sekta ya kilimo kwa gharama
yoyote ile kutokana na umuhimu wa sekta hiyo.
Dk. Shein aliyasema hayo katika ufunguzi wa Maonyesho
ya Nane Nane yaliyofanyika huko Langoni, Wilaya ya Magharibi “A” Mkoa wa Mjini
Magharibi ambayo yalihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na
Serikali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja
na wananchi wengine.
Rais Dk. Shein alisema kuwa kwa kutekeleza dhamira
hio, Serikali imechukua mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 59 kutoka Exim
Benki ya Jamhuri ya Korea kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji
maji katika hekta 1,524 Unguja na Pemba.
Aliyataja mabonde yatakayohusika na mradi huo kuwa
ni Makwararani, Mlemele kwa upande wa Pemba na Cheju, Kibokwa, Chaani,
Kinyasini na Bumbwisudi kwa Unguja ambapo hivi sasa mkandarasi wa Kampuni ya
KOLON kutoka Jamhuri ya Korea tayari ameshaanza ujenzi huo kwa bonde la Chaani
na Kinyasini.
Alieleza kuwa lengo kuu ni kuimarisha kilimo cha
kisasa kwa kuongeza zao la mpunga nchini na kupunguza kwa kiasi kikubwa
kuutegemea mchele kutoka nje ya Zanzibar, huku akiiagiza Wizara ya Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuongeza maduka wanayouza mchele ambao unazalisha
hapa Zanzibar.
Aliongeza kuwa Serikali imetenga Dola za
Kimarekani Milioni 20 ambazo ni zaidi ya TZS milioni 40, ambapo Milioni 10 kutoka
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Milioni 10 ni msaada wa Mfuko wa “Khalifa
Fund” kutoka Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) kwa kipindi cha miaka
mitano kutoka 2019 hadi 2024.
Hii ni kwa ajili ya program ya kuwaendeleza vijana
ambapo sekta ya Kilimo itakuwa ni sekta ya kipaumbele ambapo lengo kuu la hatua
hii ni kutoa fursa nyingi za ajira kwa vijana, kuongeza uzalisjai na hatimae
kukuza uchumi wa Zanzibar.
Alisisitiza kuwa katika mwaka wa fedha wa
2019/2020 bajeti ya kilimo imeongezeka
hadi kufikia TZS bilioni 88.17
kutoka TZS bilioni 62.62 zilizoingizwa mwaka 2018/2019 ambapo ongezeko hilo ni
sawa na asilimia 29 ambalo ni kubwa kwa kipindi cha mwaka mmoja.
“Serikali itahakikisha kwamba inaendelea kuongeza
bajeti ya kilimo kila mwaka, lisilobudi hutendwa kwa kuzingatia sheria na
taratibu kwani sekta ya kilimo kwa ujumla wake ni miongoni mwa sekta zilizo
muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu” alisisitiza Rais Dk. Shein.
Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa sekta ya kilimo
ambayo kama inavyoeleweka kuwa inajumuisha mazao, mifugo, uvuvi, misitu na
maliasili zisizorejesheka inaendelea kuwa ni tegemeo kubwa kwa uchumi wa
Zanzibar na inachangia moja kwa moja kwa wananchi katika kujikimu maisha yao.
Rais Dk. Shein alisema kuwa kauli mbiu ya mwaka
huu isemayo “Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa Ukuaji wa Uchumi wa Nchi Yetu”
inakwenda sambamba na Mipango na Mikakati ya Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya
mwaka 2015-2020, MKUZA III na Malengo Makuu ya Maendeleo Endelevu.
Alisema kuwa sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi
zimepangiwa mikakati madhubuti inayohakikisha kwamba malengo ya Serikali
yanatimizwa kwa mafanikio makubwa katika kuinua sekta hizo.
Pia, Rais Dk. Shein alisema kuwa ili kuweza kupata
mafanikio mazuri katika kuendeleza sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, Serikali
imeweka mkazo zaidi hivi sasa wa kuziendeleza sekta hizo kwa kutumia teknolojia
na mbinu ya kisasa.
Kwa lengo la kuendeleza sekta ya uvuvi, Rais Dk.
Shein alisema kuwa Serikali imetenga jumla ya TZS Bilioni 2.2 kwa ajili ya
ununuzi wa boti mbili za uvuvi zenye uwezo wa kuchukua tani 43 za samaki na
kuvua katika kina kirefu cha maji;
Dk. Shein alisema kuwa boti hizo zinatoka Srilanka
na Maldives ambapo boti moja itafika nchini hivi karibuni huku Serikali ikiwa
katika hatua za mwisho za matayarisho ya ujenzi wa jengo la Kampuni ya Uvuvi ya
Zanzibar (ZAFICO) lenye thamani ya TZS Bilioni 6.0 ambapo pia, kitakuwepo
kiwanda cha samaki.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa katika kuendeleza
aukuaji wa biashara ya dagaa ambayo inakua kwa kasi hapa Zanzibar na kutoa
ajira kwa makundi mbali mbali, Serikali imemamua kujenga ujenzi wa kiwanda cha
kukaushia dagaa chenye thamani ya TZS milioni 500 chenye uwezo wa kutoa dagaa
kavu tani 10 kwa siku.
Alieleza hatua zilizochukuliwa na Serikali kwa
kupata msaada wa TZS Bilioni 18 kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo la
Japan (JICA) na Serrikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga TZS Bilioni 3.6 kwa
ajili ya diko na soko la kisasa la samaki katika bandari ya Malindi, ambapo
matayarisho ya ujenzi wa soko hilo yameshaanza na ujenzi utakapokamilika
litaweza kutoa huduma kwa wananchi wapatao 6,500.
Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa anachotaka hivi
sasa vijana waandaliwe ipasavyo kimawazo, kimtizamo, na kimkakati ili wapende
kujiajiri wenyewe katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi.
Hivyo, alitoa agizo kwa Wizara ya Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo
zihakikishe kwamba katika siku hizo saba za maonyesho hayo mwaka huu inapeleka
makundi mbalimbali ya wanafunzi hasa wa Taasisi ya elimu ya juu kwa utaratibu
maalum.
Nae Kaimu Waziri wa Kilimo , Maliasili, Mifugo na
Uvuvi ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, mawasiliano na Usafirishaji Dk. Sira Ubwa
Mamboya alitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa miongozo na busara zake katika
uongozi wake hatua ambayo pia imeleta maendeleo katika wizara hiyo sambamba na
kufanyika kwa maonyesho hayo.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mariam Abdalla
Sadalla alieleza kuwa maonyesho hayo ya pili ya kilimo yaliyoanza mwaka 2017
yameweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa na kupelekea jumla ya taasisi 172 kushiriki ikilinganishwa na taasisi 83 zilizoshiriki
mwaka huo wa 2017.
Alieleza kuwa matayarisho yake yalianza mwezi Mei
mwaka huu ikizishirikisha Sekta za Serikali, binafsi na wajasiriamali
ambapo jumla ya TZS milioni 106
zimetumika ambapo Serikali imetoa TZS milioni 86 na zilizobaki zimetoka kwa
sekta binafsi na wajasiriamali.
Mapema kabla ya kuyafungua maonyesho hayo Rais Dk.
Shein alitembelea eneo la mabanda ya maonyesho na kupata maelezo kutoka kwa
wahusika.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment