Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na wananchi wa wa Kijiji cha Mwongolo wilayani Kondoa, ambapo wananchi hao walimuomba awatatulie kero ya maji ambayo imekua changamoto kubwa kijijini hapo.
Na. Mwandishi wetu, Kondoa
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini mkoani Dodoma Dkt. Ashatu Kijaji ameahidi kumaliza kero ya maji inayo wakabili wakazi wa Kijiji cha Mwongolo mkoani humo.
Ametoa ahadi hiyo alipokutana na wananchi wa kijiji hicho ambao walimweleza kuhusu changamoto yao ya muda mrefu ya kukosa huduma ya maji safi na salama pamoja na changamoto nyingine za ukosefu wa miundombinu mingine inayoweza kuchochea kasi yao ya maendeleo.
Wananchi hao walisema kero kubwa inayo waumiza ni upatikanaji wa maji katika kijiji hicho ambapo wanawake wamekuwa wakilazimika kwenda umbali mrefu kuchota maji jambo ambalo limewafanya kuchoka na kuhatarisha usalama wa maisha yao.
Dkt. Kijaji alisema kuwa amekuwa akichimba visima katika vijiji mbalimbali wilayani humo ambapo hadi sasa jumla ya visima 65 vimeshakamilika na kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
"Leo nimekamilisha kisima cha 65 Shule ya Msingi Kalamba niliposoma ndani ya miaka minne ya uongozi wangu, hapa Mwongolo ni nyumbani na kwa mapenzi niliyonayo kwa ndugu zangu wa Mwongolo, mhandisi akimaliza kuchimba kisima cha kijiji cha Mwaisanga atakuja Mwolongo katika kipindi cha mwezi huu au wa kumi kisima kitakuwa kimechimbwa" alisisitiza Dkt. Kijaji.”
Aidha ameahidi kufuatilia visima 14 vilichoahidiwa kuchimbwa kwenye sehemu ya machinjio ya kijiji hicho na Wizara ya Maji kupitia Wakala wa Uchimbaji Visima na Mabwawa, (DDCA), ili nao waweze kupata maji kwa ajili ya shughuli zao za kila siku.
Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni sikivu hivyo itaendelea kuboresha huduma mbalimbali za jamii kama vile Sekta ya elimu, huduma za afya, nishati, maji, miundombinu ili ziweze kuwafikia wananchi wote nchini kwa urahisi zaidi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwolongo Bw. Miraji Ramadhani, amemshukuru Dkt. Ashatu Kijaji kwa kutenga muda wa kwenda kutembelea kijiji hicho na kutatua baadhi ya kero zilizokuwa vinawasumbua muda mrefu.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji ameahidi hadi kufikia 2020 vijiji vyote 84 vya Jimbo lake la Kondoa Vijijini vitakua vimepata huduma ya maji kwa njia ya visima vya maji ili kumaliza kabisa kero ya maji Jimboni humo.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kondoa, Dodoma Alhaji Othman Gora(kushoto) akiteta jambo na Katibu wa CCM Wilaya hiyo Bw. Nicholaus Kasendamila wakati wa mkutano wa hadhara kati ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na Wananchi wa Kijiji cha Mwolongo alipotembea Kijiji hicho.
Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Mwolongo wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (hayupo pichani), alipokuwa anatolea majibu ya baadhi ya changamoto zilizotolewa na wanakijiji hao.
Bi. Khadija Irorya akimuelezea Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (hayupo pichani), changamoto ya ukosefu wa maji katika Kijiji hicho na kumuomba awasaidie kuitatua kero hiyo iliyodumu kwa muda mrefu.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akiteta jambo na Diwani wa Kata ya Ilolo Bw. Ramadhani Bakari alipotembea Kijiji hicho.
No comments:
Post a Comment