Habari za Punde

Watanzania Wenye Uwezo Kujenga na Kuendeleza Utamaduni wa Kutoa Misaada Kwa Watu Wenye Mahitaji Maalum.

Mkuu wa Wilaya ya Muheza akimkabidhi cheti maalum cha heshima Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi ikiwa ni sehemu ya kutahamini jitihada zake katika kuwalea watoto wenye mahitaji maalum wa wilaya ya Muheza.
Na.Kassim. Abdi.OMPR. 
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi amewataka watanzania wenye uwezo kujenga na kuendeleza utamaduni wa kutoa misaada mbali mbali kwa watu wenye mahitaji maalum ili kuwajengea miundombinu wezeshi itakayowasaidia kupata elimu bila changamoto.
Ameleza kuwa kufanya hivyo  kutaisaidia serikali kuu kufikia shabaha yake ya kuwawezesha watu wenye mahitaji maalum kupitia Nyanja mbali mbali ikiwemo suala la elimu ambalo serikali zote mbili zimeweka mkazo wake kwa kutoa kipau mbele katika kuwapatia wananchi elimu bila ya malipo.
Mama Asha Suleiman Iddi alieleza hayo katika makabidhiano maalum ya vifaa vilivyotolewa na mwakalishi wa jimbo la Uzini Mhe. Mohamed Raza kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa Skuli ya Msingi Mbaramo  Mkoani Tanga wilaya ya Muheza.
 Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa Mhe. Mohamed Raza ni mtu mwenye kujali maendeleo ya Tanzania kwani amekuwa na utamaduni wa kutoa misaada kwa makundi mbali mbali yenye uhitaji bila ubaguzi jambo ambalo linafaa kuigwa na watanzania wengine.
Akikabidhi vifaa hivyo  Muwakilishi wa Jimbo la Uzini Mhe. Mohamed Raza alisema kukabidhi kwa vifaa hivyo kutokana na ahadi yake alioitoa kupitia Harambee maalum iliofanyika Machi mwaka huu ambapo Mama Asha alikua ndie Mgeni Rasmi.
Mhe. Raza alisema kila mtanzania ana wajibu na jukumu la kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum kwani ulemavu walionao watoto hao ni mipango yake M/Mungu hivyo amewahimiza viongozi wengine kujitokeza kwa wingi katika kuwasaidia vijana hao na kuongeza kuwa serikali ya chama cha mapinduzi inayoongozwa na Dk. Magufuli na Dk. Shein hazina ubaguzi katika kuwatumikia wananchi wake.
Aidha, alisisitiza kuwa Jamii ya watanzania pia ina jukumu na wajibu wa kuleta maenedeleo ya chi hii kwa kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake anashirki katika suala zima la ulipaji wa kodi kwani kufanya hivyo kutaisadia serikali kukusanya mapato yatakayowezesha kulekeza nguvu katika kuinua uchumi wanachi kwa kuimarisha miundombinu ya sekta mbali mbali.
Muwakilishi huyo wa jimbo Uzini pia alimkabidhi Mwenyekiti wa wazazi Taifa Ndugu Edmund Mdolwa vifaa vya michezo kwa Skuli sita za wazazi zinazopatikana katika wilaya ya Muheza na aliahidi kuzisadia vifaa hivyo vya michezo skuli zote za wazazi zilizopo nchini Tanzania.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na vitanda thelasini, magoro  na mito yake, mashuka thelasini, taula thelasini pamoja na vyakula ikiwemo mchele, sukari, mafuta na siagi
Nae Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhe. Mwanaasha Tumbo alisema jitihada za Mama Asha kupitia Harambee alioiendesha Mwezi Machi mwaka huu zimezaa Matunda kwani wilaya imefanikiwa kujenga Bweni moja katika skuli ya Msingi Mbaramo ambalo litawasaidia vijana wenye mahitaji maalum.
Mhe. Mwanaasha alisema serikali kupitia halmashauri ya wilaya ya Muheza imepiga hatua katika kuwasidia watu wenye mahitaji maalum kwani halmashauri imewawezesha watu wenye ulemavu kwa kuwapa mikopo kwa takribani 70%  na alitoa wito kwa watu wenye ulemavu waendelee kujikusanya katika vikundi.
Akigusia suala la aridhi Mkuu huyo wa wilaya alieleza kuwa katika Mkoa wa Tanga serikali inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli imefuta hati sita za mashamba na kuamuru mashamba yao kufanyiwa utaratibu wa kupatiwa wananchi alesema hatua hiyo ipo katika mchakapo wa kuyapima ili hatimae kufanyiwa utekelezaji wa kupatiwa wananchi.
Akitoa Shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzake mwanafunzi wa skuli hiyo ya Mbaramo Saida Mwakidanga alieleza kuwa wanaishukuru serikali ya chama cha mapinduzi kutokana na jitihada zake za kuwawezesha vijana wenye mahitaji maalum ili waweze kupata elimu.
Mama Asha Suleiman Iddi alikamilisha ziara yake hiyo kwa kula pamoja chakula cha mchana na wanafunzi wenye mahitaji maalum wa wilaya ya muheza ikiwa ni sehemu ya kuwafariji watato hao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.