Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe akimkaribisha Miss World 2018
Vanessa Ponce kutoka Mexico wakati wa uzinduzi wa taulo za kike (Uhurupads)
uliofanyika katika shule ya sekondari Moshono leo jijini Arusha.
Na. Eleuteri Mangi, WHUSM, Arusha
Ni
heshima kubwa kwa Tanzania kutembelewa na Mwenyekiti na Mwendeshaji wa Shindano
la Miss World Bi Julia Morley pamoja na Mshindi wa Miss World 2018 Vanessa
Ponce.
Hayo yamesemwa na Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe wakati wa
uzinduzi wa taulo za kike zinazojulikana kama Uhurupads uliofanyika leo katika
shule ya sekondari Moshono iliyopo jijini Arusha.
“Ujio
wao leo hapa Arusha, ni heshima kwa taifa. Katika mataifa yote duniani,
wameichagua Tanzania, hii ni heshima kubwa na wametuletea zawadi ya Uhurupads
ambazo zitawaweka huru watoto wetu katika kutimiza ndoto zao hasa wanapokuwa
shuleni” amesema Waziri Dkt. Mwakyembe.
Aidha, Waziri Dkt.
Mwakyembe amesema kuwa bidhaa ya taulo hizo alizozindulia leo ni rafiki kwa
mazingira kwa kuwa zinaweza kutunzwa mahali popote na zisiwe na madhara kwenye
mazingira kwa kuwa haina mchanganyiko
wowote wa plastiki. Taulo hizo zinazotengenezwa na kikundi cha wanawake 12 kiachojulikana
kama timu ya Uhuru Kit Ltd ambao wanaunga mkono juhudi za Serikali katika
kutunza mazingira kwa marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki nchini Julai,
2019.
Katika kuhakikisha
Tanzania inatumia vema fursa ya ujio wa Mshindi wa Miss World 2018 Vanessa
Ponce wa Mexico, Dkt. Mwakyembe amesema kuwa Serikali itaandaa ziara maalum kwa
Uongozi wa Miss World ukiongozwa na Mwenyekiti na Mwendeshaji wa Shindano la
Miss World Bi Julia Morley kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini
ikiwemo mbuga za Serengeti, hifadhi ya Ngorongoro pamoja na mji wa kihistoria
wa Zanzibar.
“Uwepo
wa Miss World 2018 Vanessa Ponce, dunia nzima macho yao yapo hapa nchini, ni
vema kuitangaza nchi yetu kimataifa kupitia ujio wake” amesema Waziri Dkt.
Mwakyembe.
Kwa upande wake Mwenyekiti
na Mwendeshaji wa Shindano la Miss World Bi Julia Morley amesema kuwa
amefurahishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania ambapo ni mara
ya kwanza kwake kuja nchini.
“Nimefurahi
sana Tanzania ni nchi nzuri, nilipopanda ndege kuja hapa nilipata matangazo
yanayosisitiza marufuku ya kutumia mifuko ya plastiki, Serikali imefanya vizuri
kujali kutunza mazingira” alisema Bi Julia Morley.
Nao Miss World 2018
Vanessa Ponce kutoka Mexico pamoja na Miss Tanzania 2019 Sylivia Sebastian
wamesema kuwa urembo ni heshima, UhuruPads zitawasaidia wasichana kupata elimu
wakiwa huru wakizingatia kauli mbiu ya ‘Uzuri wenye malengo.’
Uzinduzi
huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti na Mwendeshaji wa shindano la Miss World Bi
Julia Morley, Mshindi wa Miss World 2018 Vanessa Ponce kutoka Mexico, Mshindi
wa Miss Tanzania 2019 Sylivia Sebastian Bebastian Bebwa pamoja, mwandaaji wa
Mashindano ya Miss Tanzania Bi. Basilla Mwanukuzi pamoja na walimu na wanafunzi
wa shule ya sekondari Moshono ya jijini Arusha.
No comments:
Post a Comment