Habari za Punde

Waziri Mhe.Mavunde :Serikali Kuendeleza Kuliwezesha Kwa Ujuzi Kundi la Vijana Nchini.


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya kazi,Vijana na ajira Anthony Mavunde akizungumza wakati wa akifunga mafunzo ya ujasiriamali kwa Vijana yaliyofanyika mkoani Tanga.

Na.Assenga Oscar                                                                                                                           
Serikali imesema itahakikisha inaendelea kuliwezesha kwa ujuzi kundi la Vijana ili waweze kushiriki kwa vitendo katika shughuli za kiuchumi na ujenzi wa Taifa

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya kazi,Vijana na ajira Anthony Mavunde Leo wakati wa kufunga mafunzo ya ujasiriamali kwa Vijana yaliyofanyika mkoani Tanga

Alisema kuwa kwa mujibu wa utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2014 inaonyesha kuwa ukosefu wa ajira kwa Vijana ni asilimia 11.7% duniani ambapo kitaifa ni asilimia 10.3%.

Hivyo kutokana na changamoto hiyo serikali imeweza kuja na mikakati endelevu ya kuliwezesha kundi Hilo kupata ujuzi wa kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa.

"Tunatambua kwamba kikwazo kikubwa kwa Vijana kushindwa kunufaika na fursa hasa za miradi ya kimkakati ni kutokuwa na ujuzi stahiki ,hivyo kwa mafunzo hayo Nina imani yatakwenda kumaliza changamoto ya ajira nchini"alisema Naibu Waziri Mavunde.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi Beng'i Issa alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa vijana kwani wanayahitaji kwa kutambua kuwa ujuzi ndio msingi mkubwa wa maendeleo.

Alisema kuwa mafunzo hayo yatawaongezea ubunifu na kutatua changamoto wanazokutana nazo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi wanazozifanya.

Mpaka Sasa jumla ya vijana 1,222 wamenufaika na mafunzo hayo katika mikoa ya Dodoma,Ruvuma,Geita, Mwanza, Mbeya, Lindi na Tanga
 Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi Beng'i Issa akizungumza wakati wa mafunzo hayo.

Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.