Habari za Punde

WAZIRI MPINA AZINDUA AGENDA ZA UTAFITI NA KUIBUA TAFITI ZILIZOFICHWA MAKABATINI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Agenda ya Kitaifa za Utafiti wa Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji wa Viumbe Maji ya mwaka 2020-2025 katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA mjini Morogoro wengine wanaoshuhudia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu SUA, Profesa Raphael Chibunda. Picha na Mpiga Picha Wetu
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akimkabidhi Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wavuvi Wadogo Dar es Salaam, Feisal Mohamed Ally Agenda ya Kitaifa za Utafiti wa Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji wa Viumbe Maji ya mwaka 2020-2025 baada ya kuizindua katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA mjini Morogoro. Wengine Katikati ni Katibu Mkuu Mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel na Katibu Mkuu Uvuvi, Dk. Rashid Tamatamah Picha na Mpiga Picha Wetu
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akionesha kitabu cha Agenda ya Kitaifa ya Utafiti wa Mifugo muda mfupi baada ya uzinduzi wa Agenda ya Kitaifa za Utafiti wa Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji wa Viumbe Maji ya mwaka 2020-2025 katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA mjini Morogoro wengine wanaoshuhudia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu SUA, Profesa Raphael Chibunda. Picha na Mpiga Picha Wetu.

 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akimkabidhi Mdau wa Ufugaji Samaki kwenye Vizimba –Ziwa Victoria, Said Mecky Sadiq Agenda ya Kitaifa za Utafiti wa Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji wa Viumbe Maji ya mwaka 2020-2025 baada kuizindua katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, Mjini Morogoro. Katikati ni Katibu Mkuu Mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel. Picha na Mpiga Picha
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare Agenda ya Kitaifa za Utafiti wa Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji wa Viumbe Maji ya mwaka 2020-2025 baada kuizindua katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, Mjini Morogoro. Wengine ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu SUA, Profesa Raphael Chibunda. Picha na Mpiga Picha Wetu.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akiwa katika picha ya pamoja na Wafugaji na Wadau wa Ufugaji wa Samaki kwenye Mabwawa kutoka Jimbo la Kisesa Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu huku wakionesha kitabu cha Agenda ya Kitaifa za Utafiti wa Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji wa Viumbe Maji ya mwaka 2020-2025 baada kuzinduliwa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, Mjini Morogoro

Na Mwandishi Wetu, Morogoro
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amezindua Agenda ya Kitaifa ya Utafiti wa Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji wa Viumbe Maji ya mwaka 2020-2025 na kutangaza kuzifumua na kuziibua tafiti zote  zilizofanywa na wasomi na kutelekezwa kwenye makabati miaka ya nyuma na kuziingiza kwenye mfumo rasmi wa matumizi ili kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo.

Pia agenda hizo zitaleta msisimko mpya wa kufanya utafiti nchini na kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma ambapo tafiti nyingi zilifanywa na kutelekezwa kwenye makabati na watafiti mbalimbali wakiwemo Wanafunzi wa Shahada ya Uzamili (Masters Degree)  na Shahada ya Uzamivu (PHD) katika vyuo vikuu mbalimbali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa agenda hizo kitaifa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA),  Kampasi ya Mazimbu mjini Morogoro, Waziri Mpina aliziagiza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo(TALIRI) na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi(TAFIRI) kubadilika ili kufanya tafiti kwa vigezo vilivyowekwa na kuleta mabadiliko chanya katika sekta za mifugo na uvuvi nchini.

Waziri Mpina alisema chimbuko la kuandaliwa kwa ajenda hizo za utafiti ni baada ya kubaini kuwa ajenda zilizokuwepo awali za Mifugo na Uvuvi zilishindwa kuibua na kuzitumia tafiti zilizofanywa kuchochea mabadiliko kwenye sekta hiyo muhimu ya uzalishaji.

Pia ajenda za utafiti zilizokuwepo za Mifugo na Uvuvi hazikuwa na utaratibu wa kuzitambua, kuziorodhesha na kuzitumia tafiti zinazofanywa na Wanafunzi wa Shahada ya Uzamili (Masters Degree) na Uzamivu (PHD) lakini sasa ajenda za utafiti zilizozinduliwa zimeweka utaratibu wa namna ya kuzitambua, kuziorodhesha na kuzitumia tafiti za wasomi hao.

“Haiwezekani tafiti za wasomi wa kiwango cha juu kiasi hicho wanazozifanya wakati wa kukamilisha masomo yao ziishie kupata alama za ufaulu na kutupwa kwenye makabati, Leo kila mhitimu atalazimika kuandaa policy brief ambayo itawezesha watumiaji na Serikali kurekebisha au kuandaa Sera na Sheria” alisema Waziri Mpina.

Aliongeza kuwa Ajenda za Utafiti zilizokuwepo za Mifugo na Uvuvi hazikuwa na utaratibu wa kuweka Kanuni ambazo zitahakikisha kuwa utekelezaji  wa ajenda za utafiti unafanyika, lakini ajenda za utafiti iliyotangazwa inaweka Kanuni zitakazotoa mwongozo na usimamizi wa utekelezaji na wajibu wa kila mhusika.

Aidha Waziri Mpina alibainisha kuwa ajenda za utafiti zilizokuwepo za Mifugo na Uvuvi hazikuwa na utaratibu wa kuwaunganisha Watafiti wa Mifugo na Uvuvi nchini, na hivyo kupelekea kila mmoja kufanya utafiti kivyake hali iliyosababisha jambo moja kufanyiwa utafiti na mtafiti zaidi ya mmoja na kukosa jukwaa la kuratibu na kuchambua tafiti zinazofanywa nchini.

“Agenda ninayoizindua leo inakwenda kujumuisha watafiti na wataalam mbalimbali waliobobea katika fani za mifugo, uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji ili kuyapitia matokeo ya utafiti, teknolojia zilizoibuliwa na utafiti na kuzisambaza kwa watumiaji kwa manufaa ya Taifa” alisema Waziri Mpina

Pia Waziri Mpina alibainisha mapungufu mengine yaliyomo kwenye ajenda za utafiti zilizokuwepo za Mifugo na Uvuvi ni pamoja na kutoweka msingi mzuri wa kusimamia Watafiti na kufanya tafiti kulingana na mahitaji ya soko badala yake  Taasisi za Utafiti na Watafiti kufanya tafiti nyingi za nje na mambo muhimu ya wananchi yanayohitaji kufanyiwa utafiti kutelekezwa.

“Leo hii agenda ninazozizindua zimeweka utaratibu wa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa, kupanua mtandao wa utafiti  na kufanya tafiti zote kulingana na mahitaji ya wananchi.  Mfano katika maeneo ya nyama, maziwa, samaki, ngozi, chakula cha samaki na mifugo, magonjwa, malisho na migogoro” alisema Mpina.

Aidha dosari nyingine zilizokuwepo kwenye ajenda za utafiti zilizokuwepo za Mifugo na Uvuvi ni kutojumuisha katika vipaumbele masuala mengi muhimu yenye changamoto nyingi ikiwemo  Mitaala na hali ya ajira.

Mpina alisema mitaala inapoanzishwa haifanyiwi utafiti wa mara kwa mara matokeo yake mafunzo yanayotolewa sio yale yanayohitajika katika soko la ajira huku Wanafunzi wanaohitimu mafunzo hawajulikani wanakwenda wapi baada ya kuhitimu na hakuna mfumo wowote wa uratibu.

“Ukienda kwa wafugaji wanaofuga na kuchunga sio hao waliosomea mifugo, ukienda kwa Wavuvi na Ukuzaji viumbe maji wanaovua na kufuga si hao waliosomea taaluma hizo, ukienda viwandani vilevile”alisema Mpina.

Pia Masoko na Biashara, Uongezaji wa mnyororo wa thamani wa mazao ya mifugo na uvuvi (Livestock & Fisheries value chain & value addition), agenda iliyopita ilizingatia uzalishaji pekee bila kuangalia upande wa soko wakati vitu hivi vinakwenda kwa pamoja kwani hakuna uzalishaji bila soko.

Waziri Mpina pia alisema licha ya kushamiri kwa migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi na eneo hilo kugubikwa na changamoto nyingi  ikiwemo  mifugo kutaifishwa, kupigwa risasi, kufilisiwa, kuuwawa kwa watu na mifugo  na kupigwa faini kubwa kiasi cha kutishia uendelevu wa sekta lakini eneo hili halikujumuishwa katika Agenda ya utafiti iliyopita.

Pia masuala mtambuka, afya ya wanyama na magonjwa ya afya ya jamii (Zoonotic Diseases) ambapo hivi sasa asilimia 60 ya magonjwa yasiyoambukiza yanatokana na mazao ya mifugo, malisho, nyanda za malisho na vyakula vya mifugo na samaki, uvuvi endelevu katika maji ya asili (Uvuvi Haramu na utoroshaji wa mazao ya uvuvi)  ambayo nayo hayakuzingatiwa katika agenda za utafiti zilizopita .

Hivyo Waziri Mpina aliwahakikishia watanzania kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti zinazofanywa zinawafikia walengwa kwa wakati ili tafiti hizo ziongeze tija na kipato kwa watuamiaji na Taifa kwa ujumla. 
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Raphael Chibunda alimhakikishia Waziri Mpina kuwa kwa niaba ya watafiti wa Chuo kikuu hicho watatakwenda kuwa sehemu ya utekelezaji wa agenda hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.