Na
Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma.
Katika
hali ya kawaida herufi huunda neno na maneno huunda sentensi nayo sentensi
huunda kikundi cha maneno. Kwa kawaida neno ni tamko mojawapo miongoni mwa
mengi ambalo mtu hulitamka katika mchakato wa mazungumzo unaopelekea iwepo misemo
ambayo ni fungu la maneno yenye maana mahususi ili kutoa fundisho kwa jamii.
Kwa
mantiki hiyo, semi ni maneno yanayozungumzwa na watu yanayoleta maana mahususi
katika lugha inayozungumzwa katika eneo fulani. Kiswahili ikiwa lugha ya Taifa
la Tanzania kimekuwa pia lugha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya nchi
za Kusini mwa Afrika (SADC), na lugha ya Umoja wa Afrika (AU). Bila kusahau
kuwa ni lugha ya kufundisha katika shule, taasisi na vyuo vikuu katika mataifa
mbalimbali duniani.
Watafiti
wa mbalimbali duniani katika tafiti zao wanabainisha kuwa lugha ya Kiswahili inashika
nafasi ya kumi katika lugha elfu sita zinazozungumzwa na watu wengi duniani
ambapo kwa nchi za Afrika kinashika nafasi ya pili kwa kuongelewa na watu wengi
Barani humu.
Tafiti
wa wataalamu wa lugha kutoka Umoja wa Nchi za Afrika unabainisha kuwa hadi
kufikia mwaka 2063 lugha ya Kiswahili ndiyo itakuwa lugha kuu ya mawasiliano
katika nchi zote za Afrika.
Ukuaji
na utambuzi huu wa Kiswahili katika Afrika na duniani kote unaipa heshima
Tanzania ikiwa ndio kitovu cha Kiswahili kuwa lugha maridhawa, adhimu na yenye ubora
wa kipekee yenye msamiati unaofaa kufundishia mataifa mbalimbali duniani.
Tanzania
ikiwa nchi Mama kwa lugha hiyo, haina budi kuwa mstari wa mbele katika kutumia
maneno ya Kiswahili sahihi na fasaha. Kutokana na sababu hiyo, Serikali imeamua
kusisitiza matumizi sahihi ya Kiswahili haswa katika misamiati yake.
“Kumekuwa
na matumizi mabaya ya maneno ‘Kisimbuzi’ na ‘King’amuzi’ Serikali haiwezi
kufumbia macho watu au taasisi ambazo zinaharibu matumizi sahihi ya maneno haya
ama kwa makusudi ama kwa kutofahamu.”Anasema Dkt Harrison Mwakyembe, Waziri
Mwenye dhamana ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Dkt.
Mwakyembe ameendelea kulipigia chapuo suala hili kwenye ziara zake za kikazi
katika mikoa Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Mwanza, Singida na Tanga ambapo
alipata fursa ya kuzungumza na wadau wa habari pamoja na wa utamaduni.
“Watanzania
tuwe mfano kwa kutumia Kiswahili fasaha ili kuudhihirisha ulimwengu kuwa Kiswahili
kitovu chake ni Tanzania.” Aliongeza Waziri Mwakyembe katika ziara zake
alizozifanya hivi karibuni.
Aidha,
akiwa katika
kongamano la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Wanafunzi na Wahitimu wa Kiswahili
Vyuo Vikuu na vya Kati Tanzania (CHAWAKITA) Januari 4, 2020 katika Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT) cha
jijini Mwanza, Dkt. Mwakyembe alibainisha umuhimu wa vyombo vya habari vya
Tanzania kuwa mstari wa mbele katika kusimamia matumizi sahihi ya lugha ya
Kiswahili.
Kwa
umahiri wa hali ya juu Waziri Mwakyembe alitoa somo la Kiswahili kwa matumizi
sahihi ya maneno haya huku washiriki wakimsikiliza kwa umakini na shabaha ya Serikali
ni kuwa baada ya ufafanuzi huo makosa yaliyokuwa yakifanyika awali kutojirudia.
Alisema
kuwa kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili neno “Kisimbuzi” lina maana ya kifaa
kinachotumika kufichua alama za kielektroniki zilizofichwa ili ziweze kusikika
na kuonekana kupitia kwenye simu, televisheni, faksi na intaneti kwa kutumia
mfumo wa dijiti.
Aliongeza
kuwa kamusi hiyo hiyo neno “King'amuzi” maana yake ni kifaa kinachotumika kufichua
vitu vilivyofichwa au kupotea aghalabu mabomu yaliyofukiwa ardhini, madini na vito
vya thamani au ni kitu kinachotambua vitu au hali ya hatari kama vile moshi, moto
na mazingira mengine ya hatari.
Waziri Mwakyembe
alisisitiza kuwa imezuka kasumba ambayo imejengeka miongoni mwa watumiaji wa
lugha ya Kiswahili vikiwemo vyombo vya habari ambavyo vinatumia vibaya lugha ya
Kiswahili ama kwa makusudi ama kwa kutokujua kutumia.
“Kupitia kongamano
hili, naliagiza Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kuvionya mara moja baadhi
ya vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vinara wa matumizi mabaya ya neno ‘king’amuzi’
badala ya neno ‘kisimbuzi’.” alisisitiza Dkt. Mwakyembe.
Ni ukweli usiopingika
ukisikiliza vyombo vya habari vya redio, televisheni na magazeti pamoja na
mitandao ya kijamii ikiwemo Face Book, Twitter, Instagram na mitandao mingine ya
kijamii. Maneno haya ‘Kisimbuzi’ na
‘King’amuzi’yanatumika ndivyo sivyo, ni vema vyombo vya habari
vichukue nafasi yake ya msingi ya kuelimisha jamii juu ya matumizi sahihi ya
maneno hayo.
Katika kongamano hilo,
Waziri Mwakyembe alikuwa Mgeni Rasmi ambapo alisisitiza kuwa nafasi ya Lugha ya
Kiswahili kuwa kati ya Lugha kumi bora duniani, kuna haja kubwa ya kuithamini,
kutunza na kuiendeleza ili ikue zaidi.
Kutokana na uhitaji
wa lugha ya Kiswahili kwa mataifa mengine, Watanzania wanafursa ya kusoma lugha
hiyo ili kupata wataalamu wa kukifundisha Kiswahili sanifu na fasaha, uhariri
na ukalimani. Hii ni fursa kwa wakufunzi, wahadhiri, wataalamu waliopo katika
sekta ya Kiswahili ama wanafunzi wa vyuo vikuu wanaosoma somo la Kiswahili
kuchukua hatua za makusudi ili waweze kuingia kwenye kada mbalimbali zilizopo
kwenye ya lugha ya Kiswahili.
Pia alitilia mkazo
juu ya umuhimu wa wajuzi wa lugha yetu kujua kutumia vyombo vya kisasa vya
kufundishia lugha ya Kiswahili katika muktadha mbalimbali iwe vyuoni, kwenye
ukalimali na maeneo mengine.
Miongoni mwa
washiriki wa kongamano hilo ni Mwakilishi wa BAKITA ambaye pia ni Mhadhiri Chuo
Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT) Dkt. Nestory Ligembe alimshukuru
na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli na Waziri mwenye dhamana na Lugha ya Kiswahili Dkt. Harrison Mwakyembe
kwa uongozi wao thabiti ambao umeleta mafanikio makubwa katika kukuza na
kuendeleza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi.
Akisoma risala
kwa niaba ya Chama cha Wanafunzi na Wahitimu wa Kiswahili Vyuo Vikuu na Vya Kati
Tanzania (CHAWAKITA) tawi la SAUT Mwenyekiti wa chama hicho Tumaini Masanja
amesema kuwa wanawajibu wa kuendeleza lugha ya Kiswahili katika ngazi ya Vyuo
Vikuu na Vyuo vya Kati, kukuza vipaji vya wanafunzi katika lugha ya Kiswahili,
kuwaunganisha wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati katika suala la kuithamini na
kuendeleza lugha ya Kiswahili na kuitangaza ndani na nje ya nchi.
Kongamano
liliongozwa na kauli mbiu “Kiswahili Urithi wetu kwa maendeleo ya Uchumi wa
Viwanda Tanzania kwa kuwa chimbuko lake ni Tanzania” kwa lengo la kuendeleza
kampeni ya kukuza na kuendeleza Kiswahili.
Ni muda
muafaka sasa kila mwenye taaluma ya Kiswahili aone ana mchango katika kukuza,
kuhifadhi na kuendeleza lugha ya Kiswahili. Soko la lugha hii adhimu sasa
limevuka mipaka ya nchi za SADC zikiongozwa na Afrika Kusini iliyoonesha uhitaji
wa walimu wa Kiswahili.
Rais Dkt.
Magufuli ameonesha njia, ni wakati sasa wa kutumia fursa hiyo, wakati ndio huu,
tumia Kiswahili katika kukuza uchumi na kipato cha mtu mmoja mmoja na hatimaye
uchumi wa taifa.
No comments:
Post a Comment