Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe.Mussa Azzan Zungu akionyesha mifuko mbadala isiyokuwa na nembo na hairuhusiwi kutumika hapa nchini
(kulia) na kulia ni Mifuko yenye Nembo inayoruhusiwa kutumika hapa nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu, akiongea na watendaji na Menejimenti ya Mwananchi Communications
Limited (MCL) Francis Nanai.
Na. Lulu Mussa. Dar
es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Zungu amesema Serikali iko
katika tafiti kuhakikisha matumizi ya gesi kama mbadala wa kuni na mkaa
yanakuwa ya bei nafuu kwa wananchi wote.
Hayo ameyasema hii leo
Jijini Dar es Salaam mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Vyombo vya
Habari vya Azam Media na Mwananchi Communications.
Amesema changamoto kubwa
hivi sasa ni kukithiri kwa ukataji wa miti kwa matumizi ya kuni na mkaa. Hivyo
katika kukabiliana na tatizo hilo suluhu ya haraka na rafiki kwa mazingira ni
matumizi ya gesi, “Tunakuja na programu ya kuweza kulipia gesi kadri
unavyotumia (paymetre)” Zungu alisisitiza.
Waziri Zungu amesema kuwa kwa
siku mwananchi anatumia sio chini ya shilingi 1500 -2000 kununulia mkaa, gesi
tunayoongelea itagharimu kati ya Shilingi 900-1000 na tafiti zinaendelea ndani
ya Serikali kwa kushirikiana na wadau. “Tunataka bei ya gesi ishuke ili wateja
wawe wengi ili kunusuru mazingira yetu”.
Katika hatua nyingine Waziri
Zungu amewatahadharisha wananchi kuwa makini na ununuzi wa mifuko mbadala aina
ya Non-Woven ambayo haikidhi viwango vilivyoainishwa.
Amesema kuwa mifuko aina ya
Non-Woven ni lazima ikidhi viwango vya ubora vilivyoainishwa na Shirika la Viwango Tanzania
(TBS) ikiwa ni pamoja na kuwa na uzito usiounguza (GSM 70), iwe inaweza
kurejelezwa, ionyeshe uwezo wa kubeba na iwe imethibitishwa na TBS.
“Nawasihi wananchi wetu kuwa
makini na mifuko isiyokidhi viwango vya ubora kwa kuwa ina athari kwa mazingira
na kiuchumi. Mifuko inayotengenezwa nchini mingi inakidhi viwango vilivyoweka
na hivyo inachangia ulipaji wa kodi na maendeleo ya taifa letu. Mifuko
isiyokidhi viwango inatoka nchi jirani na inaua viwanda vya Tanzania” Zungu
alisisitiza.
Amesisitiza kuwa walinzi wakubwa
wa mazingira ni wananchi wenyewe hivyo ametoa wito kwa umma kutoa taarifa kwa
wote wanaokiuka Sheria ya Mazingira ili Sheria ichukue mkondo wake.
No comments:
Post a Comment