Habari za Punde

WAZIRI MKUU MAJALIWA: NCHI ZA SADC TUENDELEE KUPAZA SAUTI KUONDOLEWA VIKWAZO ZIMBABWE

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akiwapungia mkono Mawaziri waliokuwa wakifuatilia ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC waliokuwa wakifuatilia kwa njia ya Video leo  Jumatano (Machi 18, 2020)   Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Dkt. Stergomena Tax akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC leo Jumatano (Machi 18, 2020)  Jijini Dar es Salaam, ambapo mkutano huo umefanyika kwa njia ya video. 
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC leo Jumatano (Machi 18, 2020)  Jijini Dar es Salaam, ambapo mkutano huo umefanyika kwa njia ya video. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC leo Jumatano (Machi 18, 2020)  Jijini Dar es Salaam, ambapo mkutano huo umefanyika kwa njia ya video. 
Mawaziri wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC leo Jumatano (Machi 18, 2020) Jijini Dar es Salaam, ambapo mkutano huo umefanyika kwa njia ya video.
(Picha na Maelezo Dar es Salaam)


Na Mwandishi Wetu, MAELEZO DAR ES SALAAM 18.3.2020
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutumia majukwaa ya kikanda, kitaifa na kimataifa kwa ajili ya kupaza sauti zao ili kusaidia kuondolewa kwa vikwazo kandamizi vya kiuchumi kwa Jamhuri ya Zimbabwe.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC leo Jumatano (Machi 18, 2020) Jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Tanzania kupitia nafasi yake ya Uenyekiti wa SADC imeendelea kupaza sauti kwa ajili ya kuisaidia Serikali ya Zimbabwe.
Aliongeza kuwa mwezi Oktoba mwaka jana Tanzania ilifanya kongamano kubwa la kihistoria lililowaleta pamoja wadau mbalimbali wa kitaifa na kimataifa, ambapo katika kongamano hilo wadau hao walitoa, ambapo Serikali ya Tanzania inaamini kuwa ujumbe wa mkutano huo uliwafikia walengwa.
Aidha Majaliwa alisema kuwa wakati Nchi Wanachama wa SADC wakielekea kuitekeleza ya mwaka 2020 (SADC Post 2020 Agenda), mataifa hayo hayana budi kuungana pamoja na kupaza sauti zao hadi hapo vikwazo hivyo vitakavyoondolewa kwa Jamhuri ya Zimbabwe, vikwazo ambavyo athari zake zimekuwa kubwa kwa uchumi wa wananchi na Nchi ya Zimbabwe.
‘’Vikwazo hivi vya kidhalimu, athari zake ni kubwa kwa ustawi wa uchumi wa Zimbabwe na wananchi wake kwa ujumla, hivyo hatuna budi kuungana pamoja katika kupaza sauti zetu ili kuisaidia Jamhuri ya Zimbabwe kuondolewa vikwazo hivi’’ alisema Majaliwa.
Kuhusu mafanikio ya SADC, Majaliwa alisema tangu Januari mwaka huu Tanzania kupitia nafasi yake ya Uenyekiti wa SADC, inaendelea na jitihada mbalimbali za kuimarisha jumuiya hiyo ili kuweza kufikia malengo, ambapo imefanikisha kufanyika kwa mikutano mitano ya kisekta ikiwemo Mkutano wa Mawaziri wa Sekta ya Mawasiliano, Uchukuzi, TEHAMA na Hali ya Hewa.
Anaitaja Mikutano mingine ni pamoja na Mkutano wa Mawaziri wa sekta za Maliasili na Utalii, Mkutano wa Mawaziri wa Sekta ya Afya, Mkutano wa Mawaziri wa Sekta ya Kazi na Ajira, Mkutano wa Mawaziri wa Menejimenti ya Maafa katika SADC.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka 40 tangu kuanzishwa kwa SADC, Jumuiya hiyo imeendela kupata mafanikio mbalimbali ikiwemo miradi ya miundombinu, viwanda, elimu, mazingira na jinsia na kuzitaka Nchi wanachama kuchukulia changamoto zinazojitokeza kwa sasa ikiwemo kisera, bajeti, ushiriki hafifu wa sekta binafsi kuwa sehemu ya maandalizi ya Mpango Mkakati wa miaka 10 ya Jumuiya hiyo wa 2020/2030.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi alisema Tanzania kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya hiyo, imewezesha kwa kiasi kikubwa kufanikisha mafanikio ya mkutano huo uliofanyika kupitia njia ya mtandao (Video Conference) kutokana na tishio la uwepo wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya COVID 19.
Prof. Kabudi alisema Tanzania kupitia nafasi yake ya  Uenyekiti imeendelea kuhakikisha kuwa ajenda ya utengamano wa Jumuiya hiyo inafikiwa kama ilivyoanishwa katika Mkataba wa Uanzishwaji wa SADC inayoongozwa na nyaraka mbili za kimkakati amazo ni Mkakati Elekezi wa Kanda 2015-2020 na Awamu ya Pili ya Mpango Mkakati wa Asasi za Siasa, Ulinzi na Usalama.
Aliongeza kuwa kupitia maazimio na mikakati hiyo, SADC imewezesha kuleta mchango na maendeleo makubwa ndani ya ukanda huo kwa kuhakikisha kuwa nchi wanachama zinakuwa na mtazamo mpya wa kimkakati na kupata matokeo chanya yatakayoakisi maendeleo jumuishi na endelevu kwa ajili ya ustawi wa wananchi wa jumuiya hiyo.
Kwa mujibu wa Waziri Kabudi alisema katika mkutano pia, Baraza hilo linatarajia kupokea na kujadili taarifa ya maandalizi ya Dira ya Jumuiya ya 2050 pamoja na Mpango Mkakati wa utekelezaji wa malengo ya dira hiyo na kutoa mtazamo mpya wa kimkakati unaotoa mwongozo kwa ajili ya kuimarisha mtangamano.
Naye Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Dkt. Stergomena Tax alisema Jumuiya hiyo imeendelea kupiga hatua za maendeleo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi ikiwemo viwanda, nishati, maji kupitia utekelezaji wa maazimio na mipango mbalimbali ya utekelezaji iliyowekwa katika mwaka 2019/2020 na 2020/2021.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.