Habari za Punde

TUZALISHE KWA WINGI BIDHAA TULIZOKUWA TUNAAGIZA KUTOKA NJE: PROF SHEMDOE


Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe wa kwanza kulia akiwa kwenye Mkutano wa Watalaam wa Mashirika ya  Viwango kutoka nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwa njia ya Video katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, Tanzania, wa pili kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Bw.Athuman Ngenya.
Watalaam wa Shirika la Viwango kutoka Tanzania wakifuatilia kwa makini Mkutano wa Mashirika ya Viwango wa nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwa njia ya Video katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, Tanzania.

 Picha na Idara ya Habari-MAELEZO.

Na Erick Msuya – MAELEZO -21.04.2020
Wazalishaji wa Bidhaa mbali mbali nchini wametakiwa kuzalisha kwa wingi bidhaa zilizokuwa zinaagizwa kutoka Nje ya Nchi, kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa hizo kulikosababishwa na ugonjwa wa Corona, pamoja na kuitumia fursa ya uwepo wa Bandari hasa kwa ajili ya kuhudumia soko la SADC.

Wito huo umetolewa Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe wakati akifungua Mkutano wa wataalam wa Mashirika ya Viwango kwa nchi za SADC uliofanyika kwa njia ya Video katika Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere JNICC.

Prof. Shemdoe amesema kutokana na kufungwa kwa baadhi ya mipaka ya Nchi na upungufu wa upokeaji wa bidhaa kutoka Nje, wakati sasa umefika kwa wazalishaji wa ndani kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kuzalisha bidhaa kwa wingi zaidi.

“Tunatatizo la Corona nchini, na baadhi ya biashara kupitia mipakani zimepungua hivyo kusababisha kupungua kwa bidhaa kwenye nchi zinazotegemea bandari zetu, hii ni fursa kwetu hivyo tuzalishe kwa wingi kwa ajili ya nchi hizo ambazo zinatuzunguka na ambazo zinategemea bandari zetu” alisema Prof. Shemdoe

Aidha Prof. Shemdoe alisema lengo kuu la Serikali ya Tanzania ni kuzalisha kwa wingi Viwandani bidhaa zenye ubora na zenye uwezo wa kushindana katika masoko ya nchi za SADC na Kimataifa ili kuweza kufikia malengo makuu ya kupambana kiuchumi hasa katika kipindi hiki ambacho maradhi ya Corona yameenea katika nchi mbalimbali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania Dkt. Yusuph Ngenya amewataka wamiliki wa Viwanda na Wazalishaji wa bidhaa kuendelea kuzalisha bidhaa zenye Ubora na Viwango ili waweze kushindana na kununuliwa kwa wingi na nchi 16 wanachama wa jumuiya ya SADC na Afrika Mashariki kwa ujumla.

“Niwaombe wenye viwanda na watengezaji wa bidhaa ndani ya nchi wajitahidi kutengeza bidhaa zenye viwango na ubora, sababu kiwango kikishapita hapa Tanzania, basi soko lote la nchi 16 za SADC bidhaa itaweza kununuliwa, hivyo ni wakati sasa wa soko kututambua ndani ya Afrika na Nje ya Afrika. AlisemaDkt. Ngenya

Shirika la Viwango Tanzania TBS ni miongoni mwa mashirika ya viwango yanayotambulika na kuheshimika kimataifa kwa weledi na utoaji wa viwango vya kimataifa hivyo bidhaa za ndani zitakazothibitishwa na Shirika hilo zitakuwa na ubora na viwango vya Kimataifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.