Habari za Punde

ZAWA Yatakiwa Kufanya Jitihada Kusambaza Maji Safi na Salama Kwa Wananchi Katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan Katika Maeneo Wananchi Hawapati Maji.



MAMLAKA ya Maji Zanzibar (ZAWA) na Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati zimeagizwa kufanya jitihada za kusambaza maji safi na salama katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika maeneo ambayo wananchi hawapati huduma hizo ipasavyo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa agizo hilo katika risala ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani aliyoitoa kupitia vyombo vya habari, ikiwa ni utaratibu wake aliouweka kila ukikaribia mwezi huo Mtukufu kila mwaka.
Katika risala yake hiyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa kama kawaida yake katika risala zake zote kama hizo ambazo huzitoa kila mwaka hutoa agizo hilo kwa taasisi hizo husika kwa kuhakikisha kuwa zinawapelekea maji wananchi katika yale maeneo ambayo hawapati maji vizuri agizo ambalo amelirejea tena mwaka huu.
Aidha, Rais Dk. Shein aliwataka wananchi wote wa Zanzibar wa dini na madhehebu mbali mbali kuendeleza utamaduni wa tangu kale na dahari wa kupendana, kusaidiana, kuheshimiana na kuvumiliana na kutoa wito kuendeleza utamaduni huo ambao ni miongoni mwa misingi inayofanya kuishi kwa amani na utulivu nchini.
Aliongeza kuwa wale ambao hawahusiki na ibada ya funga, hapana shaka kama kawaida yao wataendelea kutumia busara na kuonesha ustaarabu kwa kujiepusha na mambo yasiyowapendeza wananchi wenzao wanaotekeleza ibada hii ya funga.
Vile vile, Rais Dk. Shein alitoa wito kwa vyombo vya ulinzi kuimarisha doria za ulinzi katika maeneo mbali mbali hasa kwa wakati ambao watu wengine watakuwa katika shughuli za ibada.
Kadhalika, Rais Dk. Shein aliwakumbusha madereva wazingatie sheria za usalama wa barabarani ili kupunguza tatizo la kuongezeka kwa ajali za barabarani katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Rais Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kuwaagiza wafanyakazi wa Jiji la Zanzibar na Manispaa zake, Mabaraza ya Miji na Halmashauri za Wilaya waongeze bidii katika kusimamia usafi wa Jiji la Zanzibar na miji mingine, masoko pamoja na nidhamu ya kufanya biashara.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliwahimiza wauzaji wa bidhaa mbali mbali kuzingatia matumizi bora ya mvua za Masika zinazoendelea kwa kudumisha usafi na kuimarisha nidhamu katika masoko na maeneo maalumu yaliyotengwa kwa shughuli za biashara.
Aidha, Rais Dk. Shein aliwahimiza Waumini wa Dini ya Kiislamu kuzielekeza nafsi zao katika kufanya mambo ya kheri waliyohimizwa na Mola Mtukufu katika Qurani na Hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W) ili kuweza kupata rehma na kufaidika na fadhila kubwa za mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
“Ni wajibu wetu tuzichunge ndimi zetu kwa kujiepusha kusengenya, kutoa kauli mbaya pamoja na kufanya vitendo vinavyoweza kuzusha fitna na hasada ndani ya jamii”, alisema Dk. Shein.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliwataka wananchi wakati wote kuwa makini kwa yale mambo wanayoangalia na kuyasikiliza katika redio na televisheni pamoja na yale wanayoyaandika katika mitandao ya kijamii kupitia simu za mikononi.
Alisisitiza haja ya kujitathmini juu ya aina ya taarifa na picha wanazoziingiza katika mafaili ya simu zao za mikononi na kuwataka kujidhatiti katika kuyashinda matamanio yote ya nafsi yanayoweza kuzibatilisha funga zao.
Katika risala hiyo pia, Rais Dk. Shein alitoa pongezi za dhati kwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Kupambana na Maafa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar pamoja na wajumbe wote.
Kadhalika, Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa Mwenyekiti wa wa Kamati ya Kupambana na Maradhi yanayosabaishwa na virusi vya COVID 19 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaaliwa Majaaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wajumbe wote kwa kufanya kazi kwa pamoja na kwa uzalendo.
Vile vile Rais Dk. Shein alitoa shukurani kwa viongozi wengine mbali mbali wa Serikali, dini, jamii na wananchi wote kwa jumla kwa kuziunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na maradhi hayo.
Shukurani za dhati alizitoa Rais Dk. Shein kwa madaktari na wataalamu wa afya ambao tangu yalipoanza maradhi hayo wamefanya juhudi kubwa ya kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kuwapatia huduma mbali mbali kwa wale wote walioathirika au kuonesha dalili za maradhi hayo.
Rais Dk. Shein pia, aliwapongeza wafanyabiashara na wananchi ambao wameanza kuchangia kwenye Akaunti zilizofunguliwa kwenye Benki ya PBZ na CRDB katika kukabiliana na COVID 19 na kuwashukuru wale wote waliochangia kwa kutoa vifaa maalum na nyenzo mbali mbali ambazo zitasaidia mapambano dhidi ya COVID 19.
“Tuzingatie ule usemi maarufu wa Kiswahili usemao “Kutoa ni moyo si utajiri”. Wazee wetu walitueleza tangu kale na dahari maneno yao yaliyojaa hekima ya kuwa “Haba na haba hujaza kibaba”. Serikali ipo tayari kupokea chochote kilicho haba, ili kwa pamoja tujaze kibaba kupitia mfuko maalum”,alisisitiza Dk. Shein.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wahusika mbali mbali inapanga kuongeza kiwango cha taaluma ili wale ambao wanaonekana hawajazingatia vizuri elimu na taarifa zilizotolewa nao waweze kuelimika zaidi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.