Habari za Punde

Ubalozi wa China Zanzibar Wakabidhi Msaada wa Vifaa Kwa Ajili ya Kupambana na Maradhi ya Corona

Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaowu’s Kulia akimkabidhi Waziri Mohamed Abpud msaada wa Vifaa mbali mbali vilivyotolewa na China kupitia Ofisi hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed Kushoto na Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaowu’s wakionyesha Vitabu walivyotia saini mkataba wa makabidhiano wa Vifaa vya kukabiliana na Virusi vya Corona. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed akiishukuru China kwa kuendelea kuiunga Mkono Zanzibar.
Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bw. Xie Xiaowu’s akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya vifaa mbali mbali kwa ajili ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona.
Mkurugenzi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Khatib Makame akitoa maelezo ya vifaa vilivyopokelewa na Taasisi yake kutoka kwa Uongozi wa Ubalozi wa China hapa Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini mchango mkubwa unaoendelea kutolewa na Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China katika kuunga mkono Maendeleo na Ustawi wa Wananchi wa Zanzibar.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed alitoa kauli hiyo katika hafla fupi ya kupokea msaada wa Vifaa mbali mbali vya kusaidia mapambano dhidi ya Virusi vya Corona vilivyotolewa na China kupitia Ubalozi wake Mdogo uliopo Zanzibar hapo katika Majengo ya Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Maruhubi.
Mheshimiwa Mohamed Aboud alisema msaada huo wa Maboksi 225 yenye vifaa tofauti ikiwemo nguo za kinga kwa ajili ya Madaktari wanaoshughulikia Maradhi ya Corona, Maski, Vipima Joto la Mwili pamoja na mashine nyengine za uchunguzi umekuja wakati muwafaka wa mapambano dhidi ya Maradhi hayo thakili.
 Alisema juhudi hizi za pamoja kati ya Mataifa na Taasisi za Kimataifa bila shaka zitaleta mafanikio makubwa sio kwa China na Zanzibar pekee bali kwa Dunia Nzima kwa vile wanaopatiwa huduma za Kiafya kwenye janga hilo wamo pia Watu wa Mataifa mbali mbali ulimwenguni.
Waziri Aboud alibainisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais wake Dr. Ali Mohamed Shein imejizatiti kuongeza Mikakati ya mapambano dhidi ya kupunguza au kuondosha kabisa Virusi vya Corona Nchini ambapo inatia moyo kuona Jamii imeshaelewa nguvu ya mnaradhi hayo thakili.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar kwamba Zanzibar itaendelea kushirikiana na Taifa hilo katika kipindi hichi cha mpito wa janga hilo lililoathiri Dunia Nzima.
Alisema Uchumi wa Dunia, Zanzibar ikiwa ni sehemu za Dunia hiyo umeporomoka kutokana na kusimamam kwa muenendo mzima za Sekta ya Mawasiliano ya Anga na hata Bahari inayounganisha harakati za Kiutalii ambazo hunchangia kwa kisi kikubwa Uchumi huo.
Mapema Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana. Xie Xiaowu’s alisema msaada huo umekuja kufuatia uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya China na Zanzibar na Tanzania kwa Ujumla.
Balozi Xie alisema China inaelewa athari kubwa inayotokana na Janga la Corona ambalo lilianzia ndani ya Taifa hilo. Hivyo aliahidi kwamba Nchi  hiyo kupitia Afisi yake ya Ubalozi iko mbioni muda wowote kuanzia sasa kuleta shehena nyengine ya Msaada kama huo ili kuona maradhi hayo yanaondoka kabisa.
Akitoa Shukrani kutokana na msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Khatibu Makame amewapongeza Washirika wa Maendeleo akitolea mfano China na Shirika la Afya Ulimwenguni kwa jitihada zao za kuiunga Mkono Zanzibar kwenye masuala mbali mbali ya Ustawi wa Jamii.
Nd. Makame alisema Msaada huo mkubwa ni nguvu nyengine za ziada zitakazosaidia juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Mapambano dhidi ya kuondosha kabisa mripuko wa Virusi vya Corona Nchini.
Akitoa salamu za Shirika la Afya Ulimwenguni Mwakilishi wa Shirika hilo Kanda ya Zanzibar Dr. Andemichael Girmay aliitanabahisha Jamii lazima ikubali kwamba Virusi vya Corona vipo Nchini na Taasisi za Kimataifa zimejitolea kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya Virusi hivyo.
Dr. Girmay alisema masuala ya mzala inapaswa yaachwe miongoni mwa baadhi ya Jamii kwa vile kuendelea kubakia Virusi hivyo Nchini ni hatari kutokana na Jamii kuendelea kubakia kuwa na maisha ya kubahatisha katika harakati zake za kutafuta riziki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.