Habari za Punde

Wakuu wa Madiko katika Wilaya ya Magharibi ''B'' Unguja Waomba Kupatiwa Ufumbuzi wa Ukataji wa Leseni na Uvuvi Haramu

Na.Takdir Suweid - Maelezo Zanzibar.
Wakuu wa Madiko katika Wilaya ya Magharibi ‘’B’’ Unguja wameomba kupatiwa ufumbuzi matatizo yanayowakabili ili waweze kufanya kazi kwa Ufanisi na kuingizia Mapato  kwa Serikali.
Wakizungumza katika Kikao cha Wajumbe wa kamati ya huduma za jamii na Wakuu wa Madiko wa Wilaya hiyo, huko Ofisi za Baraza la Manispaa Wilaya ya Magharibi ‘’B’’ Unguja kwa mchina wamesema baadhi ya Wavuvi kutokata Leseni za Uvuvi na kushamiri kwa Uvuvi haramu kunalikosesha Mapato Baraza hilo.
Wamesema Serikali imefanya Ugatuzi ili kuwapatia huduma bora na rahisi Wananchi wake hivyo kutopatiwa ufumbuzi matatizo hayo ni kurudisha nyuma juhudi za Serikali katika kuwatumikia Wananchi.
Kwa upande wake Makamo Mwenyekiti wa Kamati ya huduma za Jamii Baraza la Manispaa Wilaya ya Magharibi ‘’B’’Unguja Bi.Thuwaiba Jeni Pandu amesema wanakusudia kufanya Doria Baharini na kuimarisha Ulinzi maeneo ya Fukwe za Bahari ili kuondosha Uvuvi haramu unaoendelea.
Hata hivyo amewataka Wakuu wa Madiko kushirikiana na Baraza la Manispaa Wilaya ya Magharibi ‘’B’’ Unguja ili kujadili na kuyapatia Ufumbuzi matatizo yanayosababisha kuvuja Mapato ya Serikali hasa katika Sekta zilizogatuliwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.