Na: Thomas Valentine, Maelezo
Baada ya Rais Dkt.
John Pombe Magufuli kuruhusu shule zote kufunguliwa tarehe 29 mwezi huu wakati akifunga
Bunge la 11 Jijini Dodoma, shule ya Sekondari King’ongo iliyopo katika kata ya Saranga
wilaya ya Ubungo Jijini Dar es Salaam imepokea msaada wa madawati 50 na viti 50
yenye thamani ya shilingi milioni 24 kutoka kwa Wakala wa Vipimo (WMA).
Akizungumza katika
hafla hiyo ya kukabidhi madawati katika shule hiyo Jijini Dar es Salaam,
Mkurugenzi wa Ufundi Wakala wa Vipimo Bi. Stella Kahwa amesema kwamba mchango huo
ni sehemu ya utekelezaji na dhamira ya Wakala wa Vipimo kuunga mkono jitihada za
Serikali katika kuboresha elimu.
“Huu ni mchango wetu
kama wakala wa vipimo katika kuhamasisha, naamini watoto watasoma katika mazingira
mazuri na wataweza kusoma vizuri zaidi na kufanya vizuri zaidi katika masomo yao
na mitihani ya kata na ya taifa.” Amesema Kahwa.
Makabidhiano yamehudhuriwa
na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Bi. Tatu Pambe ambaye amesema madawati hayo
50 na viti 50, yataboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi na kutoa wito kwa
wadau wengine kuunga mkono zoezi hilo kwani tatizo la uhaba wa madawati katika shule
hiyo ni changa moto sana.
“Kwanza
tunashukuru Serikali kupitia Wakala wa Vipimo kwa kuweza kutuwezesha kwa ajili ya
madawati.
Shule yetu ya sekondari
kuna madarasa mengi lakini tatizo ni madawati, lakini kupata madawati 50 na viti
50 tunashukuru sana.” Amesema Tatu.
Naye mwalimu mkuu
wa shule ya Sekondari King’ongo Bw. Joseph Msangya ameipongeza Wakala wa Vipimo
kwa msaada huo wa madawati na kusema kuwa msaada huo utasaidia kupunguza changamoto
ya madawati kwani mahitaji ya madawati ni mengi shuleni hapo.
Mkuu wa shule hiyo
amesema ongezeko la madawati utasaidia katika kuongeza ufaulu wa masomo kwa wanafunzi
kutokana na kusoma katika mazingira mazuri.
“Shule yetu ina wanafunzi
1,052 kwa hiyo uhitaji tunao ni mkubwa sana. Tuna madarasa matatu ambayo hayana
kiti wala meza, lakini tunashukuru Wakala wa Vipimo kwa mchango wao baada ya kuona
na kuguswa kwa hili na pia tunawaomba wada wengine ambao wameguswa kwa namna moja
au nyingine kutusaidia maana mahitaji yetu ni mengi.”Amesema Msangya.
No comments:
Post a Comment