Habari za Punde

Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa Amtembelea Mhe. Mbowe Hospital ya Ntyuka Alikolazwa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye amelazwa katika  hospitali ya Ntyuka jijini Dodoma, kwa matibabu Juni 9, 2020. Mbowe anatibiwa majeraha aliyoyapata baada ya kushambuliwa  na watu ambao bado hawajajulikana wakati akiingia nyumbani kwake jijini Dodoma usiku wa kuamkia   leo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Juni 9, 2020 amemtembelea na kumjulia hali Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye amelazwa katika hospitali ya Ntyuka jijini Dodoma kwa matibabu.

Waziri Mkuu amemuombea kiongozi huyo uponyaji wa haraka wa majeraha aliyoyapata baada ya kuvamiwa na watu ambao bado hawajajulikana wakati akiingia nyumbani kwake jijini Dodoma usiku wa kuamkia leo Juni 9, 2020.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa  taarifa za tukio la kuvamiwa kwa Mheshimiwa Mbowe na watu ambao bado hawajajulikana, namuomba Mwenyezi Mungu amjalie  apone haraka ili aweze kurejea katika majukumu yake.”

Baadhi ya wabunge wa Upinzani waliokuwepo hospitalini hapo na ambao walimpokea Waziri Mkuu ni Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, Mbunge Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA,                      

JUMANNE, JUNI 9, 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.