Habari za Punde

Azma ya Kugombea Wadhifa Huo Ni Kuwatumikia Wananchi wa Zanzibar -Dkt. Hussein Mwinyi.


Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, akizungumza na Wananchi na Wanachama wa CCM katika viwanja vya Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Jijini Zanzibar, wakati wa hafla ya mkutano wa mapokezi uliofanyika leo baada ya kuwasili Zanzibar akitokea Dodoma.  

Mgombea wa Kiti cha Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi alisema azma ya kugombea wadhifa huo ni kuwatumikia Wazanzibar pamoja na Watanzania wote kwa uwezo wake wote, akibainisha dhamira ya kuwaletea maendeleo na ustawi katika maisha yao.

Alisema miongoni mwa vipaumbele vyake ni pamoja na kuendeleza amani iliopo ili Zanzibar iweze kupiga hatua zaidi za maendeleo, huku akiahidi kazi hiyo kufanyika kwa ushirikiano kati ya wananchi  na vyombo vya ulinzi na usalama.

Alisema analenga kuimarisha umoja na  mshikamano wa Kitaifa miongoni mwa Wazanzibari wote ili kuondokana na hatari ya kuibuka kwa ubaguzi wa kimajimbo.

Aidha, alieleza kuwa ataendeleza kasi ya maendeleo iliyoanzishwa na mtangulizi wake na kukamilisha miradi yote ya maendeleo kwa maslahi ya Wazanzibari.

Katika utekelezaji wa majukumu yake, Dk. Mwinyi alisema hatakuwa na muhali, huruma wala na atasimamia vita dhidi ya rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma, uzembe pamoja na watendaji wote wasiowajibika ipasavyo.

Aliwataka viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa kujiweka tayari kwa kazi ili kuweza kukipatia ushindi chama hicho, kupitia kampeni zitakazoendeshwa  kisayansi ili hatimae kushika Dola.

Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi aliahidi kutetea maslahi ya Zanzibar kupitia Jumuiya zote za Kikanda na zile za kimataifa.

Mapema, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Juma Abdalla Sadalla alisema hatua ya kwanza ya uteuzi wa mgombea wa chama hicho imekamilika, kupitia vikao halali vilivyoendeshwa kwa uwazi na bila makundi.

Alimsifia mgombea huyo kuwa ni mwanachama mchapakazi, mweledi, mwenye uelewa wa mambo na uwezo  mkubwa katika kutoa maamuzi kwa hekima na busara.

Mapema kiongozi huyo alipata mapokezi makubw akutoka kw awnanachi na wanachama wa CCM, waliojikusanya kutoka uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume hadi Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui, akiwemo msanii maarufu wa kizazi kipya kutoka Tanznaia Bara Ali Kiba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.