Habari za Punde

Balozi Seif ashiriki na wanafamilia kuomboleza kifo cha Job Lusinde

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimpa pole Mke wa Marehemu Mzee Job Lusinde Waziri wa Zamani wa Tanzania Mama Sara Lusinde Nyumbani kwake Mjini Dodoma
 Balozi Seif Ali Iddi akitia Saini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha Waziri wa Zamani wa Serikali ya Tanganyika na baadae Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Mzee Job Petro Lusinde hapo Mtaa wa Farahani Jijini Dodoma.
 Baadhi ya wanafamilia ya Mzee Joab Lusinde wakiendeleza maombolezo kufuatia msiba wa Mpendwa wao huyo aliyefariki Hospitali na Rufaa Muhimbili akiwa na Umri wa Miaka 90.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa pole kwa wanafamilia na Wakaazi wa Jiji la Dodoma kufuatia kifo cha Waziri wa Zamani wa Serikali ya Tanganyika na baadae Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Mzee Job Petro Lusinde.
Picha na – OMPR – ZNZ

Na Othman Khamis, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema mchango wa Mzee Job Petro Lusinde aliyefariki Dunia Jana katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbuili Jijini Dar es salaam utaendelea kubakia Historia ndani ya Mioyo ya Watanzania.
Balozi Seif Ali Iddi akiambatana na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi alisema hayo wakati alipofika Nyumbani kwa Mzee Lusinde Mtaa wa Farahani Jijini Dodoma kuweka saini Kitabu cha Maombolezo, kuifariji pamoja na kuipa pole Familia na Kiongozi huyo Mkongwe Nchini Tanzania.
Alisema Kiongozi huyo akiwa Muasisi wa Baraza la Kwanza la Mawaziri la Serikali ya Tanganyika mara tuu baada ya Uhuru na baadae Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania amebobea katika masuala ya Kidiplomasia ambapo aliwahi kuiwakilisha Jamuhuri ya Muungano katika Mataifa tofauti Duniani.
Balozi Seif alisema akianza Kazi ya Udiplomasia katika Wilzara ya Mambo ya Nje ya Tanzania alibahatika kufundishwa kazi na Mzee Lusinde alip[okuwa Balozi wa Tanzania Nchini Jamuhuri ya Watu wa China.
Alisema mafunzo aliyoyapata kwa Mzee huyo yalimpatia fursa ya kusimamia ufunguliwaji wa Ubalozi wa Tanzania Nairobi Nchini Kenya ambapo baadae Mzee Lusinde alihamishiwa Nchini humo na kuendelea na nafasi yake ya Ubalozi kuanzia mwaka 1980 hadi 1990.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa niaba ya Wananchi wa Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Familia yake ameitaka Familia ya Marahemu pamoja na watu wake wa Karibu kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha msiba.
Marehemu Mzee Joab Petro Lusinde aliyezaliwa mnamo Mwaka 1930 akifikisha Umri wa Miaka Tisini aliyefariki kutokana na Ugonjwa wa Moyo ameacha Kizuka Mmoja na Watoto Wanne. Mwenyezi Mungu alilaze roho yake mahali pepa peponi Amin.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Wanafamilia ya Mzee Joab Petro Lusinde Mdogo wake Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mzee John Samuel Malesela aliwashukuru Watanzani wote waliojitolea kuungana na familia hiyo tokea kuuguza hadi mauti ya Mzee Lusinde.
Mzee Malesela alisema kitendo hicho cha ushirikiano kilichojumuisha na safari ya kuusafirisha Mwili wa marehemu kutoka Muhimbili Jijini Dar es salaam hadi Dodoma kimewapa fafraja kubwa wanafdamilia hao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.