Habari za Punde

Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC Yatoa Tarehe ya Uchaguzi Mkuu Zanzibar.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar  (ZEC ) Mhe. Jaji Mkuu Mstaaf wa Zanzibar Hamid Mahmoud, akizungumza na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vilioko Zanzibar, kuhusiana na utoaji wa taarifa ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kwa Urais, Uwakilishi na Udiwani, unaotarajiwa kufanyika mwaka huu 2020.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar  (ZEC ) Mhe. Jaji Mkuu Mstaaf wa Zanzibar Hamid Mahmoud, akizungumza na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vilioko Zanzibar, kuhusiana na utoaji wa taarifa ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kwa Urais, Uwakilishi na Udiwani, unaotarajiwa kufanyika mwaka huu 2020.
Picha na Abdalla Omar


TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imetangaza Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa urais na uwakilishi utafanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Mkuu mstaafu, Hamid Mahmoud wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi tarehe 30 Julai 2020 visiwani humo.

Jaji Mahmoud amesema, kura ya mapema kwa watendaji wanaosimamia majukumu ya uchaguzi huo, itafanyika siku moja kabla yaani Jumanne tarehe 27 Oktoba 2020.
“Natangaza rasmi tarehe ya uchaguzi itakuwa Jumatano tarehe 28 Oktoba mwaka huu, ndugu wananchi, sheria ya uchaguzi imetoa nafasi kufanyika kura ya mapema, napenda kuwajulisha, upigaji kura ya mapema itafanyika tarehe 27 oktoba 2020 siku moja kabla ya upigaji kura pamoja,” amesema Jaji Mahmoud.

Mwenyekiti huyo wa ZEC amesema, kura ya mapema itahusisha wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wa vituo vya uchaguzi na askari polisi watakaokuwa zamu siku ya uchaguzi. Wajumbe na watendaji wa tume.

“Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, upigaji kura mapema utahusisha watendaji wanaosimamia majukumu ya uchaguzi siku ya uchaguzi, watendaji hao ni wasimamizi wa uchaguzi, wasaidizi wasimamizi uchaguzi, wasimamizi wa vituo, askari polisi watakaokuwa kazini siku ya uchaguzi ,” amesema Jaji Mahmoud.
Siku hiyo ya uchaguzi mkuu, inafanana na ile iliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania kuwa, uchaguzi mkuu utafanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020.

NEC ilisema shughuli ya uchukuaji fomu kwa wagombea ambapo wagombea wa ubunge na udiwani watachukua fomu tarehe 12 hadi 25 Agosti 2020, katika ofisi za NEC za halmashauri na kata nchi nzima.

Uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 25 Agosti 2020, huku kampeni zitaanza tarehe 26 Agosti hadi 27 Oktoba 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.