Kamishna wa Idara ya Uendelezaji
Sekta ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja, akifafanua
jambo katika mafunzo ya Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha kwa
watendaji wa mikoa ya Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na
Iringa, yaliyofanyika mjini Morogoro.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya
Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha kwa watendaji wa mikoa ya Kanda
ya Kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa wakifuatilia kwa
makini mada mbalimbali zilizowasilishwa wakati wa mafunzo hayo, yaliyofanyika
mjini Morogoro.
Na Farida Ramadhani, WFM, Morogoro
Serikali imewataka watendaji wa mikoa kuhakikisha
wanasimamia na kuendeleza Sekta Ndogo ya Fedha nchini kwa kuhamasisha watoa huduma
katika sekta hiyo wanasajiliwa na kukata leseni kwa mujibu wa Sheria ya Huduma
Ndogo za Fedha ya mwaka 2018.
Agizo hilo limetolewa na Kamishna wa Idara ya Uendelezaji
Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja, wakati
wa mafunzo ya Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha kwa watendaji wa
mikoa ya Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Sngida na Iringa, yaliyofanyika
katika hoteli ya Nashera mjini Morogoro.
Dkt. Mwamwaja alisema kuwa watendaji hao ni watu
muhimu katika kuhakikisha Sekta ya Fedha nchini inastawi kwa lengo la kukuza uchumi
na kuondoa umaskini nchini.
“Mkitoka hapa mtakuwa kisima cha maarifa ambayo
yatasaidia kutatua changamoto mbalimbali za sekta hii ambazo zimekuwa
zikirudisha nyuma maendeleo ya wananchi. Nimatumaini yangu sasa changamoto
zitakapo wasilishwa kwenu mtarudi kuangalia Sera, Sheria na Kanuni zinasemaje
katika kutatua changamoto hizo”, alisisitiza Dkt. Mwamwaja.
Katika mafunzo hayo watoa mada walieleza miongozo na masharti mbalimbali yaliyoanishwa katika Sera,
Sheria na Kanuni za Huduma ndogo za Fedha ya namna ya kuendesha biashara
katika sekta hiyo zikiwemo taratibu
za ukataji leseni na usajili.
Mwanasheria wa Serikali kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI,
Bi. Antelma Mtemahanji, ni miongoni mwa watoa mada hao ambaye alisema pamoja na
Sheria hiyo watoa huduma za fedha nchini pia wanatakiwa kufuata Sheria zingine
za nchi ikiwemo Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu.
Alisema watoa huduma wa daraja la nne (vikundi vya
kijamii vya huduma ndogo za fedha) wameruhusiwa kupokea akiba za wanachama wake,
kukopesha wanachama wake pamoja na kukusanya michango mbalimbali ya uendeshaji
wa kikundi hicho.
“Kikundi kinatakiwa kiwe na akaunti ya benki kwa ajili
ya kuhifadhi fedha, jambo hili ni muhimu ili kuepuka upotevu wa fedha za wanachama
kama ambavyo tumekuwa tukisikia na kuona kwenye vyombo vya habari mara kwa mara
wanavikundi wakilalamikia kuibiwa fedha na watunza fedha wa vikundi hivyo, utasikia
mama fulani alikua anatunza fedha mtoto wake kaiba kisanduku”, asisitiza
Bi. Mtemahanji alisema vikundi hiyo haviruhusiwi kufungua
matawi au kuwa wakala wa benki, kupokea amana kutoka kwa wateja wasio wanachama
na kukopesha watu nje ya vikundi vyao.
Aliwatoa hofu wanavikundi katika daraja hilo kwa
mujibu wa Sheria kuwa vikundi vyao havitafungiwa bali vitaelelimishwa utaratibu
wa kuvitambua na kuvisajili ili viweze kuendelezwa na kuchangia uchumi wa nchi.
Naye mtoa mada kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Deogratius
Mnyamani alisema kuwa Sheria hiyo imeanisha misingi ya kumlinda mtumiaji wa huduma
ndogo za fedha kwa kutoa miongozo mbalimbali ikiwemo utaratibu wa kukusanya
madeni, uwazi katika utoaji wa mikopo na
ulipaji gawio kwa wanachama wake.
Alisema sasa ni wakati wa kufuata Sheria na kuacha
kasumba ya kudai kwa vitisho na kudhalilisha wakopaji kwa kuwa Sheria hiyo imetoa
maelekezo ya kumtaka mkopeshaji kutoa elimu kwa kina kwa mkopaji namna ya kuulipa
mkopo huo.
Bw. Mnyamani amewaonya wakopeshaji kutochukua kadi za kutolea
fedha banki wakopaji kama dhamana ya mikopo wanayopewa kwa kuwa ni kinyume cha sharia
na kwamba Sheria Mpya ya Huduma Ndogo ya Fedha imetoa miongozo ya dhamana za
mikopo.
Kwa upande wake Mwanasheria kutoka Tume ya Maendeleo
ya Ushirika ambaye pia ni miongoni mwa watoa mada, Wakili Shanil Mayosa alisema
kuwa Sheria hiyo kama Sheria zingine za nchi ina adhabu ambazo zitachukuliwa
kwa watoa huduma watakaokiuka.
Alisema adhabu hiyo haijawekwa kwa ajili ya kuwatisha
watoa huduma na wananchi kwa ujumla bali inalenga kuimarisha usimamizi, udhibiti
na uendelezaji wa Sekta ya Fedha nchini.
Washiriki wa mafunzo hayo wameipongeza Serikali kwa
kuendelea kuwajali wananchi hususan wa hali ya chini ambao wamekuwa wakidhulumiwa
na watu wasio waaminifu ambao wamekuwa wakitumia upenyo wa kutokuwepo kwa
Sheria mahsusi inayosimamia Sekta Ndogo ya Fedha.
Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Bw. Robert George
ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo ambaye aliishauri Serikali kutoa
mafunzo kama hayo mara kwa mara katika masuala mbalimbali kwa maendeleo ya nchi.
Mafunzo hayo ni muendelezo wa Mpango wa Elimu kwa Umma
kuhusu Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha uliozinduliwa Desemba
mwaka jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, ili
kuwawezesha wananchi kufuata matakwa ya Sheria na kuinusuru sekta ndogo ya fedha
ambayo ni miongoni mwa sekta muhimu
katika ukuaji wa uchumi
wa Nchi.
No comments:
Post a Comment