Habari za Punde

Balozi Seif Atembelea Mradi wa Jengo la Mall Michezani Jijini Zanzibar.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hifadhio ya Jamii Zanzibar {ZSSF} Bibi Sabra Issa Machano akimtembeza Balozi Seif Ali Iddi na Ujumbe wake sehemu mbali mbali za Jengo hilo la Biashara.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi akiwa na Waziri wa Fedha Kushoto yake Balozi Mohamed Ramia na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi mh. Hassan Khatib Kulia yake wakilikagua Jengo la Biashara Michenzani {Michenzani Mall} alipofanya ziara ya kuangalia maendeleo ya ujenzi huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi na Ujumbe wake akikaguzwa  jengo la Mall Michezani na Mkurugenzi Mtendaji wa ZSSF Bibi Sabra Issa Ghorofa ya pili itakayokuwa na Mkahawa, Michezo ya Watoto pamoja na Ofisi.
Mkurugenzi Sabra Issa Machano akimtembeza Balozi Seif na Ujumbe wake kwenye Jnego la Biashara la Thabit Kombo { Thabit Kombo Mall} katika eneo la Kisonge Michenzani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi na Ujumbe wake wakilikagua eneo la chini la Biashara Ghoroga ya kwanza ndani ya Jengo la Biashara Michenzani linalojengwa na Wahandisi kutoka Kampuni ya Kimataifa ya China ya CRJE.
Waziri wa Fedha na Mipango wa SMZ Balozi Mohamed Ramia akitoa maelezo jinsi Majengo ya Biashara Michenzani yatakavyotoa huduma za Kibiashara pale ayatakapoanza rasmi kazi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi akitoa nasaha zake mara baada ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Majengo ya Biashara Michenzani ambayo yako katika hatua za mwisho kumalizika.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.
Wakati Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ikiwa tayari imeshaingia ndani ya Uchumi wa Kati mapema Mwaka huu hivi sasa inaendelea kuchanja mbuga katika kuimarisha Miradi ya Kiuchumi, Biashara na Maendeleo ili kuvuka salama katika Daraja hilo la Kiuchumi ndani ya miaka michache ijayo.
Ujenzi wa miundombinu katika Sekta ya Kiuchumi hasa Miradi ya Biashara uliopamba moto katika pembe zote za Visiwa vya Unguja na Pemba ni ushahidi wa mabadiliko hayo yanayozidi kustawisha Maisha ya Wananchi kutokana na Pato la Taifa kutarajiwa kukuwa kwa kasi ya asilimia 7-8% mwaka 2020.
Mtaa wa Michenzani uliosheheni Majengo ya Kisasa ya Biashara { Maarufu Michenzani Mall na Thabit Kombo Mall} yanayomalizika Ujenzi wake ndani ya Wiki mbili hizi yameanza kubadilisha haiba ya Mji wa Zanzibar unaoanza kufananishwa na baadhi ya Miji Maarufu Ulimwenguni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alishawishika kufanya ziara maalum ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa Majengo pacha hayo ya Biashara Michenzani  yanayotarajiwa kukamilika rasmi si Zaidi ya siku Kumi na Nne kuanzia sasa.
Akimtembeza Balozi Seif na Ujumbe wake katika maeneo mbali mbali ya Majengo hayo pacha Meneja Uwekezaji na Utafiti wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar {ZSSF} Nd. Abdulaziz Ibrahim Iddi alisema jengo kubwa la Michenzani lenye Ghorofa Tisa limesheheni huduma zote zinazostahiki kupatikana katika maeneo ya Biashara.
Nd. Abdulaziz alizitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na eneo la Maduka, Mkahawa, huduma za Kibenki, sehemu ya kuchezea Watoto, mazoezi, Sinema, Ukumbi wa Mikutano pamoja na Ofisi zitakazokodishwa kwa Wateja na Taasisi tofauti zitakazohitaji.
Akizungumzia Jengo la Thabit Kombo Mall Meneja huyo wa Uwekezaji na Utafiti wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar alisema ZSSF imeshirikiana na Maskani ya Kisonge katika kuona Jengo hilo linakamilika kwa lengo la kutoa huduma za Kibiashara.
Alisema eneo la Chini ya Jengo hilo watakabidhiwa Uongozi wa Kisonge kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kwa vile Maskan hiyo ilikubali kutoa Jengo lake kwa kuridhia kupisha ujenzi wa Jengo hilo la Biashara, wakati sehemu nyengine za Biashara na Ofisi zitakodishwa kwa mujibu wa maombi ya Wafanyabiashara.
Akitoa shukrani zake baada ya kuridhika na ujenzi wa majengo hayo mapya na ya kisasa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alielezea faraja yake kutokana na mabadiliko makubwa ya Kisonge  yanayokwenda kwa kasi kubwa ya Maendeleo.
Balozi Seif alisema Zanzibar kadri ya siku zinavyopotea inazidi kubadilika Kimaendeleo kutokana na harakati kubwa ya uimarikaji wa Miundombinu ya Kiuchumi inayobeba mfumo mmoja wa upatikanaji wa huduma  bila ya kujali maeneo ya Mijini au Vijijini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi na Watendaji wote wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar {ZSSF} kwa uamuzi wake wa kuendelea kushirikiana na Serikali Kuu katika kuimarisha Miradi ya Kiuchumi, Biashara na Maendeleo ya Ustawi wa Wananchi.
Balozi Seif  aliunasihi Uongozi utakaopewa jukumu la kusimamia Uendeshaji wa Majengo hayo ya Biashara Michenzani kuzingatia upangaji wa bei zitakazokidhi mahitaji ya wale watakaoonyesha nia ya kutaka kutoa huduma za Biashara katika eneo hilo.
Mapema Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Mohamed Ramia alisema hakuna ahadi iliyowekwa kwa Wafanyabiashara wa Makontena waliokuwa wakifanya Biashara eneo hilo lakini maombi yao yatazingatiwa na kupewa nafasi ya pekee.
Hata hivyo Balozi Ramia alitanabahisha wazi kwamba Maduka mapya yaliyojengwa katika mfumo wa huduma za Kimataifa za Kisasa yatazingatia Zaidi muombaji atakayekidhi kiwango na kukubali kutimiza kanuni na taratibu zitakazowekwa.
Waziri wa Fedha na Mipango alifahamisha kwamba eneo la Michenzani limeingizwa katika Mradi Maalum uliokusudiwa kuendelezwa na Serikali Kuu kwa kubadilisha umbo la Mji wa Zanzibar mradi unaokusudiwa kuanzia Mtaa wa Kariaboo kupitia Michenzani hadi Mtaa wa Mkunazini unaounganisha eneo la Mji Mkongwe uliomo ndani ya Hifadhi ya Uridhi wa Kimataifa.
Ujenzi wa Majengo pacha ya Kisasa ya Michenzani Kisonge { Michenzani Mall na Thabiti Kombo Mall chini ya usimamizi wa Wahandisi wa Kampuni ya Kimataifa ya China {CRJE} umeanza mnamo Mwezi Oktoba Mwaka 2018 na unatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa Serikalini ndani ya Wiki Mbili zijazo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.