Habari za Punde

MAAFISA USTAWI WA JAMII NA MAAFISA MAENDELEO YA JAMII WAHIMIZWA KUENDELEA KUTOA HUDUMA BORA KWA WATU WENYE ULEMAVU

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga akizungumza na Maafisa Ustawi wa Jamii pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii wakati wa kikao kazi kilichofanyika Jijini Dar es Salaam Disemba 30, 2020 katika ukumbi wa Mkutano wa Anatouglou uliopo kwenye ofisi ya halmashauri ya Ilala lengo ikiwa ni kujadiliana na kushauriana namna bora ya kuhudumia watu wenye ulemavu pamoja na kutatua changamoto zinazo wakabili. (Kushoto) ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Bi. Charangwa Makwiro.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Bi. Charangwa Makwiro akieleza jambo wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga alipokutana na Maafisa Ustawi wa Jamii pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii kujadiliana pamoja na kushauriana namna bora ya kuhudumia watu wenye ulemavu pamoja na kutatua changamoto zinazo wakabili.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga akipitia taarifa ya ripoti zilizokuwa zikiwasilishwa na Maafisa Ustawi wa Jamii pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhusu uwezeshaji wa mikopo ya 10% inayotolewa na halmashauri kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu. Kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Bi. Charangwa Makwiro na (kulia) ni Afisa Mipango na Uratibu ambaye pia ni Mwakilishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Gerald Sando.
Baadhi ya Maafisa Ustawi wa Jamii pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii walioshiriki kikao kazi hicho wakifuatilia kwa makini hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (hayupo pichani).

Na: Mwandishi Wetu

Maafisa Ustawi wa Jamii pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii wamehimizwa kutoa huduma bora kwa watu wenye ulemavu ili kuimarisha ustawi na kuchochea maendeleo ya kundi hilo maalum.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga alipokutana na Maafisa hao katika kikao kazi kilichofanyika Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Mkutano wa Anatouglou uliopo kwenye ofisi ya halmashauri ya Ilala lengo ikiwa ni kujadiliana pamoja na kushauriana namna bora ya kuhudumia watu wenye ulemavu pamoja na kutatua changamoto zinazo wakabili.

Mheshimiwa Ummy alieleza kuwa Serikali kwa kutambua na kuthamini haki za wenye ulemavu imekuwa ikishirikiana na asasi za Watu wenye ulemavu kwa nia njema na dhamira ya dhati ili kuhudumia kundi hilo kwa kuwapatia huduma bora kulingana na jamii inayowazunguka.

“Katika kipindi kifupi serikali imetimiza wajibu wake huo kwa kutoa Elimu, huduma za Afya, mafunzo ya stadi za kazi, ajira, nyenzo za kujimudu, huduma za kijamii, kuwezeshwa kiuchumi na vilevile kuboresha miondombinu ili iwe Rafiki kwa matumizi ya watu wenye ulemavu katika kupata huduma stahiki,” alieleza Mheshimiwa Ummy

Aliongeza kuwa kundi hilo hapo nyuma liliachwa lakini tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani kundi hilo linapigiwa chapuo na limekuwa likijumuishwa katika kila nyanja muhimu, lakini serikali iliyopo imeendelea kujenga mazingira kwa wenye ulemavu ili waweze kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali zilizopo katika kuboresha huduma zao.

“Malengo ya serikali ni kuhakikisha inaendeleza watu wenye ulemavu pasipo kuachwa nyuma na hivyo katika kutambua hilo imeendelea kuwahamasisha wenye ulemavu kushiriki katika kila nyanja,” alisema

Sambamba na hayo, amewata Maafisa hao kuongeza juhudi na kasi katika kuhamasisha Watu wenye Ulemavu, Vijana na Wanawake kuanzisha vikundi ambavyo vitachangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri kwa kuanzisha miradi au kuendeleza miradi waliyonayo ili waweze kujikwamua kiuchumi.

“Upo umuhimu wa kutambua uwezo na vipaji maalum vya watu wenye ulemavu, vijana na wanawake na kuweka mikakati madhubuti ya kuviendeleza vikundi wanavyoanzisha ili waweze kujikomboa kiuchumi na waweze kuajiri watu wengine,” alisema Ummy

Alifafanua kuwa katika suala la uwezeshaji wa watu wenye ulemavu inaonyesha kuwa wametambua umuhimu wa mikopo hiyo inayotolewa na halmshauri na ndio maana wamekuwa wakijitokeza kuchukua mikopo inayotolewa na halmashauri.

“Jambo hili limenifurahisha kuona sasa mikopo inatolewa kwa wingi kwa watu wenye ulemavu ambao wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi, tunashuhudia kupitia uwezeshaji huo kumekuwa na ongezeko la miradi mbalimbali inayoendeshwa na wenye ulemavu,” alisema Ummy

“mafanikio haya yanayoonekana yanatokana na juhudi zenu kama maafisa wa serikali katika kupanga utekelezaji wa shughuli zenu vizuri, muongeze juhudi katika kutoa huduma bora ili kwa pamoja kutimiza malengo ya kukuza uchumi wa taifa letu,” alieleza

Aidha, Naibu Waziri Ummy alitoa rai kwa vikundi ambavyo vimekuwa na tabia ya kukopa katika halmashauri moja na baadae kuhamia kwenye halmashauri nyingine kutaka kukopa tena kwenye halmashauri nyingine kuacha mara moja tabia hiyo huku akiwataka warejeshe mikopo yao kwanza ndio wakope tena.

Pia, Mheshimiwa Ummy alitumia fursa hiyo kuvitanga vikundi vya watu wenye ulemavu kuachana na kasumba kuwa mikopo wanayopatiwa na halmashauri ya 2% kuwa ni misaada au inatolewa bure badala yake wakope na kurejesha kwa wakati ili waweze kukopeshwa tena zaidi.

Akizungumza kabla, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Bi. Charangwa Makwiro alieleza kuwa bado yanafanyika maboresho makubwa katika kuwezesha watu wenye ulemavu, vijana na wanawake ili kuboresha miradi yao iweze kunufaika kiuchumi zaidi.

Kwa upande wake, Afisa Mipango na Uratibu ambaye pia ni Mwakilishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Gerald Sando alieleza kuwa Halmashauri zote sita za mkoa zimekuwa zikitoa mikopo hiyo katika kila mwaka wa fedha sambamba na kujiwekea mikakati ya kuwezesha vikundi vingi zaidi.

Naye, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Kigamboni Bi. Christina alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa halmashauri hiyo wamefanikiwa kuwezesha vikundi vingi ikiwemo watu wenye ulemavu kwa kuwapatia mikopo ya bajaji, usindikaji na mikopo mingine inayoendana na ulemavu alionao mtu husika.

Katika kikao kazi hicho walishiriki Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na Maafisa Vijana ambao walipata fursa ya kutoa taarifa ya uwezeshaji wa mikopo ya 10% inayotolewa na halmashauri zao kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.