Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais Mhe Hemed alifungua Tamasha la 14 la asasi za Kiraia

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akisalimiana na Viongozi mbali mbali wa Serikali alipowasili Viwanja vya Nje vya Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil kufungua Tamasha la 14 la Asasi za Kiraia.
 Mheshimiwa Hemed Suleiman akijitayarisha kuingia katika Ukumbi wa wa Sheikh Idrisa Abdulwakil kufungua Tamasha la 14 la Asasi za Kiraia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiangalia na kupata maeleo kwa Wadau wa Maonyesho ya Asasi za Kiraia waliohudhuria Tamasha la 14 la Asasi hizo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiangalia na kupata maeleo kwa Wadau wa Maonyesho ya Asasi za Kiraia waliohudhuria Tamasha la 14 la Asasi hizo.


Mjumbe wa Bodi ya Jumuiya ya The Foundation for Civic Society Bibi Munira Humud akitoa salamu kwenye hafla ya ufunguzi wa Tamasha la 14 la Asasi za Kiraia.
Mwenyekkiti wa Mwamvuli wa Asasi za Kiraia Zanzibar {Angoza } Bibi Asha Aboud akitoa Taarifa ya muendelezo wa Matamasha yanayoandaliwa na Asasi za Kiraia.
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikaliza Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mh. Masoud Ali akijiandaa kumkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman kulifungua Tamasha la Asasi za Kiraia kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi.
Baadhi ya Viongozi wa Kiserikali wakishuhudia matukio mbali mbali yaliyojiri kwenye ufunguzi wa Tamasha hilo la Asasi za Kiraia hapo Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakili Kikwajuni.
Baadhi ya Wadau wa Asasi za Kiraia wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa Tamasha lao la 14 ambapo Mgeni Rasmi ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman kwa niaba ya Rais wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akilifungua Tamasha la 14 la Asasi za Kiraia kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Hussein Ali Mwinyi  hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na watendaji baada ya kulifungua Tamasha la 14 la Asasi za Kiraia kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Hussein Ali Mwinyi  hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis , OMPR

Asasi za Kiraia zina Wajibu mkubwa wa kuchangia katika kushirikiana na Serikali Kuu kwenye Mikakati ya kukuza Uchumi wa Taifa kwa kupiga vita vitendo vya ufisadi, rushwa na ubadhirifu kwa kuyabaini pale yanapokuwepo kupitia shughuli za uwajibikaji kwenye matumizi ya Fedha na utoaji huduma.

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla wakati akilifungua Tamasha la 14 la Asasi za Kiraia hapo Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil.

Alisema Asasi ya Kiraia siku zote zinakuwa kama daraja la kuwaunganisha Wananchi wa Serikali yao katika kusimamia utekelezaji wa Mipango  ya Maendeleo inayolenga kuimarisha hali za maisha ya Wananchi wote kwa ujumla wake.

Dr. Hussein alisema Serikali inahitaji kuwa na Zanzibar iliyoungana na kwamba tofauti za kifrika, Imani, itikadi, rangi, kanda, jinsia zisiwe sababu ya maafa  bali jamii ichote kutoka utajiri wa tofauti hizo na Asasi za Kiraia ndio yenye dhima kwa hilo hasa kwa kuwa ziko karibu zaidi na Jamii.

“ Kwa dhati kabisa ninatambua kazi kubwa inayofanywa na asasi za kiraia kwenye maeneo mbali mbali kama vile Afya, Elimu, Utawala Bora, Haki za Binaadamu na kadhalika”. Alisisitiza Dr. Hussein Ali Mwinyi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alisema anayaelewa mazingira ya Wadau wa Asasi za Kiraia hasa upatikanaji wa fedha  ambao kwa kiasi kikubwa unategemea wafadhili kutoka Nje ya Nchi ambao umekumbwa na changamoto kubwa.

Alisema uwepo wa uhaba wa Rasilmali fedha,mifumo ya kisheria iliyopitwa na wakati inayosimamia Sekya hiyo ya Asasi za  Kiraia na wakati mwengine masharti yanayopkwenda sambamba na ufadhili huo vinayafanya mazingira ya kukuwa na kushamiri kwa Asasi za Kiraia kuwa na dhiki mno.

Alifahamisha kwamba changamoto hizo kwa ujumla zimekuwa  zikirejesha nyuma jitihada za Asasi hizo za kuungana na Serikali katika utoaji wa huduma na hili limethibitika kwa baadhi ya asasi hizo huanzishwa zikiwa na dira, dhamira na malengo mazuri lakini zinakufa kipindi kifupi baada yha kukosa ufadhili.

Alisema inapendeleza kuona hivi sasa zipo Asasi za Kiraia zipatazo Elfu Mbili katika ngazi mbali mbali zikihitajiwa zote ingawaje katika mazingira ya sasa ni chache mno zinazoonekana au kusikika.

Dr. Hussein Ali Mwinyi alibainisha kwamba kwa vile suala la utungaji wa Sera na Sheria ni wajibu wa Serikali na zipo changamoto zinazoihusu Serikali moja kwa moja hivyo alisema kamwe hatopenda kuona vipo vikwazo wakati Serikali ikitambua wazi mchango unaotolewa na Taasisi hizo.

Aliwaeleza Wadau hao wa Asasi za Kiara kwamba hivi sasa mchakato wa utengenezaji wa sharia ya Jumuia zisizo za Kiserikali Zanzibar unaendelea na jitihada zimezingatiwa katika kupata Sheria rafiki zitakazotokana na ushiriki wao katika hatua mbali mbali.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  alilipongeza Shirika la The Foundation for Civil Society kwa kuwa karibu karibu na ASASI ZA Kiraia katika kuzisaidia kifedha na kiutaalamu ambazo nyingi hivi sasa zimeweza kukomaa.

“ Mimi binafsi pamoja na Mamlaka mbali mbali za Kiserikali tutajitahidi kwa uopande wetukushirikiana nanyi ili kuona Sekta hii inashamiri. Hivyo inaahidi kuweka mazingira mazuri ili sekta ya Kiraiaiwe hai na imara”. Alisisitiza Dr. Mwinyi.

Alielezea matumaini yake kwamba Asasi za Kiraia zitaitumia fursa hiyo waliyoipata ya majadiliano katika Tamasha hilo kwa kushirikiana na Taasisi za Kiserikali kwa lengo la kuleta Maendeleo kwa Watu wote wa Zanzibar kwa vile wote wanajenga Nyumba Moja.

Naye kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Jumuiya ya The Foundation for Civic Society Bibi Munira Humud alisema kwa vile Asasi za Kiraia ni mtetezi wa Jamii ipo haja ya kuongezwa kwa ushirikiano na wadau wote ili kuona dhamira hiyo inafanikiwa vyema.

Bibi Munira alisema ushirikishwaji wa Asasi za Kiraia  katika Maendeleo ya Taifa na Jamii haila mjadala wakati huu kutokana na malengo yake moja kwa moja yanamgusa Mwananchi katika naeneo yake yote ya ustawi.

Akitoa taarifa Mwenyekkiti wa Mwamvuli wa Asasi za Kiraia Zanzibar {Angoza } Bibi Asha Aboud alisema asasi za kiraia zimekuwa na Utamaduni wa Kuendeleza Matamasha kila mwaka yanayoongeza wigo wa ufanisi katika kuimarisha uchumi na usawi wa Jamii yote ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.

Bibi Asha alisema Utawala Bora na Uwajibikaji uliotukuka  unaoendelea kusimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane ni ishara njema ya muelekeo wa kushamiri kwa kasi ya Uchumi sambamba na kuiba Miyanya ya Rushwa, Ubadhirifu na Uzembe.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Tamasha hilo la Nane la Asasi za Kiraia Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikaliza Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mh. Masoud Ali alisema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Asasi za Kiraia katika Maendeleo ya Taifa.

Mh. Masoud alisema ni vyema kwa Wadau wa Asasi hizo wakaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika muelekeo wa kumkomboa Mwananchi zikijitathmini upya malengo yao ili ziende sambamba na dhamira ya dhati ya Serikali Kuu katika kuwahudumia Wananchi.

Alitahadharia kwamba Asasi za Kirais zijiepushe na cheche zozote zinazoashiria kurudisha nyuma muelekeo wa Serikali uliojikita kupiga vita mambo yote yanayozorotesha kasi ya kuongezeka kwa Uchumi na huduma za Kijamii katika maeneo mbali mbali Nchini.

Ujumbe wa Mwaka huu wa Tamasha la Asasi za Kiraia unasema:- Zanzibar iliyoshamiri Sekta hai ya Kiraia. Ujumbe huu unatoawito kwa wadau wote kuwa kushamiri kwa Zanzibar pamoja na mambo mengine kunahitajika pia Sekta ya Kiraia iliyo hai. Uhai huo ni pamoja na kutenda na kuonekana pia inatenda.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla  kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti Dr. Hussein Ali Mwinyi alipata fursa ya kukagua Maonyesho ya Wajasiri Amali wa Asasi za Kiraia wanaoshiriki Maonyesho hayo.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.