Habari za Punde

Rais Dk Hussein Ali Mwinyi amteua Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.


 

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

  Zanzibar                                             07.12.2020

---

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amemteua Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

 

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, uteuzi huo umeanza jana tarehe 6 Disemba, 2020.

 

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kwamba kwa kuzingatia matakwa ya Kifungu cha 9(3) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kinachosema kwamba “Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa Umoja wa Kitaifa na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na lengo la kufikia demokrasia”.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya Chama cha upinzani cha ACT Wazalendo kuafikia uamuzi wa kujiunga na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itakayokuwa na Muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

 

 

Katibu Mkuu wa chama hicho cha ACT Wazalendo Ado Shaibu akizungumza na waandishi wa habari hapo jana tarehe 6 Disemba, 2020 huko Jijini Dar-es Salaam alisema kuwa katika mkutano maalum wa Kamati Kuu ya chama hicho wameamua kupendekeza jina la mwanachama atakayekuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

 

Sambamba na hayo, chama hicho pia, kimeruhusu Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge, na Madiwani waliochaguliwa kukiwakilisha chama hicho na wananchi waliowachangua kushiriki kikamilifu katika nafasi zao walizochaguliwa.

 

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.