Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi Ajumuika na Waumini wa Dini ya Kiislam Katika Sala ya Ijumaa Masjid Istiqaama Shangani Jijini Zanzibar.Ski MherA

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali  Mwinyi akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislam katika Masjid Istiqaama Shangani Jijini Zanzibar baada ya kumaliza Sala ya Ijumaa katika Masjid hiyo leo 4/12/2020.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaomba Waislamu kuendelea kumuunga mkono na kumuombea dua ili Mwenyezi Mungu amsaidie kwa yale yote ambayo amedhamiria kuwafanyia wananchi wa Zanzibar apate wepesi wa kuyatekeleza.

Alhaj Dk. Hussein aliyasema hayo leo huko Masjid Istiqama Shangani Jijini Zanzibar wakati akitoa salamu kwa Waumini wa dini ya Kiislamu mara baada ya kumaliza sala ya Ijumaa.

Alhaj Dk. Hussein Mwinyi alisema kwamba tayari ameanza kufanya kazi na ameona kasoro zilizopo na anataka kuzirekebisha lakini anajua kwamba ni jambo la kawaida iwapo kasoro zitakapoanzwa kurekebishwa kuna mambo yatatokezea.

Akiyataja mambo mawili yatakayotokea katika hatua hiyo, Alhaj Dk. Hussein Mwinyi aliyataja kuwa ni pamoja na wengi watafurahia kwa sababu watanufaika na wachache hawatofurahia kwa sababu katika mfumo uliokuwa na makosa walikuwa wananufaika hivyo bila shaka watu hao hawatompenda.

Hivyo, Alhaj Dk. Hussein Mwinyi aliwaomba Waislamu wamuombee dua ili aweze kutekeleza dhamira yake ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar.

Alhaj Dk. Hussein alisema kuwa aliomba nafasi ya Urais kwa dhamira moja tu ambayo ni kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na kuwaletea maendeleo ambapo ndani yake havitokosa vikwazo hivyo alimuomba Mwenyezi Mungu kuviondoa ili yale yote yaliyokwenye dhamira yake yaweze kutekelezwa.

Alitoa shukurani kwa kukamilisha uchaguzi kwa salama na amani na kumuomba Mwenyezi Mungu amani iliyopo izidi kudumu ili kuweza kuishi kwa amani na kufanya ibada kwa amani .

Alhaj Dk. Hussein Mwinyi alieleza kuwa wakati wa kipindi cha uchaguzi alikwenda msikiti hapo na kuwaomba Waislamu na wananchi wote wa Zanzibar kwamba mara nyingi kipindi cha uchaguzi ndipoambapo amani huvunjika na matatizo mengi hutokea kipindi kama hicho.

Hivyo, aliwaomba wananchi wote waendelee kuilinda amani iliyokuwepo na kumuomba Mwenyezi Mungu kwa kujaalia kumalizika kwa uchaguzi mkuu kwa salama na amani na kusisitiza kwamba lililobaki hivi sasa ni kuendelea kuijenga nchi.

Alhaj Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa nchi hujengwa na wananchi wote na sio Serikali pekee yake na kutilia mkazo kwamba kila mtu akifanya wajibu wake pale alipo basi nchi itajengeka.

Aliongeza kuwa kila pale anapofanya uteuzi wa Wasaidizi mbali mbali amekuwa akisisitiza kwamba kila mtu awajibike katika nafasi yake ya kazi.

Hivyo, Alhaj Dk. Hussein Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wote kila mtu alipo akiwa katika kazi ya Serikali, binafsi, ufugaji, mvuvi, ukulima kwani kila mtu akifanya jukumu lake ndipo maendeleo ya nchi hupatikana.

Alisisitiza kuwa kwa upande wa Serikali anayoiongoza inafanya kila linalowezekana katika kuhakikisha yale yaliyoelezwa katika Ilani ya Uchaguzi na katika ahadi yanatekelezwaambapo ili yatekelezwe kuna hitajika mambo mawili likiwemo la kwanza ni kuilinda amani iliyopo.

Aidha,alilitaja jambo la pili kuwa kuhakikisha kuwa kila mtu anwajibika katika nafasi yake ya kazi aliyonayo,kwani  iwapo uwajibikaji utakuwepo na kila mtu atawajibika wakiwemo viongozi wa Serikali hakuna shaka kwamba yote yaliyoahidiwa kwa wananchi yatatekelezwa ikiwa ni pamoja na kuwaletea wananchi maendeleo.

Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Hussein aliwashukuru na kuwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuendelea kudumisha amani iliyopo na kusisitiza kwamba hivi sasa na kwa upande wa Serikali iko tayari kuijenga nchi kwa mashirikiano ya wananchi wa Zanzibar na kumuomba MwenyeziMungu azidi kuleta baraka zake ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.