Habari za Punde

Hamasa na Vugu vugu Kuelekea Siku ya Wiki ya Maadhimisho ya Saratani Ulimwenguni

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akianzisha Rasmi hamasa na vugu vugu kuelekea ndani ya Wiki  ya maadhimisho ya Siku ya Saratani Ulimwenguni inayofikia kilele chake ifikapo Tarehe Nne Febuari ya kila Mwaka Afisini kwake Vuga.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Taasisi zinazojihusisha na mapambano dhidi ya Maradhi yasiyoambukiza Zanzibar pamoja na baadhi ya Viongozi wa Wizara ya Afya.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imezidi kuimarisha mipango yake ya udhibiti wa ongezeko na kupunguza athari zinazosababisha uwepo wa maradhi ya saratani Nchini ikilenga kulipa umuhimu mkubwa suala zima la Afya bora kwa Wananchi wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alitoa kauli hiyo Afisini kwake Vuga wakati akianzisha Rasmi hamasa na vugu vugu kuelekea ndani ya Wiki  ya maadhimisho ya Siku ya Saratani Ulimwenguni inayofikia kilele chake ifikapo Tarehe Nne Febuari ya kila Mwaka.

Maadhimisho hayo yatatanguliwa na Siku Tatu za Kambi ya upimaji wa Saratani, ushauri pamoja na utolewaji wa Elimu itakayoendelea kuwawezesha Wanawake wafikie hatua ya kuweza kujipima wenye maradhi hayo.

Mheshimiwa Hemed alisema Saratani ni miongoni mwa  maradhi sugu yanayosababisha vifo vingi duniani kwa mujibu wa Takwimu za Shirika la Afra Ulimwenguni |{WHO} zinazothibitisha ufariki wa Watu 17 kila Dakika Moja  kutokana na maradhi hayo.

Alisema uwepo wa ushirikiano kati ya Serikali, Taasisi, Jumuiya zisizo za Kiserikali pamoja na Jamii unaweza kupunguza vichocheo vinavyochangia kuugua maradhi hayo ikiwemo sigara, matumizi ya pombe, ukosefu wa mazoezi, kiwango kikubwa cha mlo wa mafuta pamoja na uhaba wa mboga mboga na matunda.

Mheshimiwa Hemed alieleza kwamba Wataalamu wa Afya wamekuwa wakifanya uchunguzi wa maradhi ya Saratani  za shingo ya Kizazi, Matiti kwa Wanawake na Tezi Dume kwa Wanaume yanayoonekana kuathiri idadi kubwa ya Wananchi Visiwani Zanzibar.

Alisema uchunguzi huo wa Saratani ya Shingo  ya Kizazi umehusisha Zaidi ya akina Mama 34,000 ambapo jumla ya akina mama 371 waligundulika katika hatua za awali za saratani na kupewa matibabu wakati Wanawake 34 waligundulika kuwa na kiwango cha juu cha ugonjwa huo na kupewa rufaa ya kupata matibabu katika Hospitali Bingwa Jijini Dar es salaam.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini mchango mkubwa unaoendelea kutolewa na Taasisi na Jumuiya zisizo za Kiserikali  zinazoonyesha nia na juhudi za kuunga mkono jitihada za Serikali katika mapambano dhidi ya maradhi hayo.

Mheshimiwa Hemed alitolea mfano mzuri ulioshuhudiwa hivi karibuni ni ule  ushirikiano na Jumuiya inayopambana dhidi ya Maradhi yasiyoambukiza pamoja na ile ya Muungano wa Watu wanaoishi na Maradhi yasiyoambukiza Zanzibar walipofanya uchunguzi wa Saratani ya Matiti, Kisukari na Shindikizo la Damu.

Alielezea faraja yake kutokana na ushiriki wa Wananchi waliowengi kwenye zoezi hilo lililojumuisha Wanawake Mia Tano na Sitini na Tisa ambapo kati ya hao Wanawake Watatu waligundulikwa kusumbuliwa na Saratani ya Matiti,

Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwataka Wananachi, na Wataalamu ambao tayari wameshakuwa na uzoefu na mazoezi kama hayo wakaendelea kushajiisha wananchi kushiriki kwenye upimaji wa maradhi hayo linalotarajiwa kufanyika Hospitali ya Wete Pemba kuanzia asubuhi ya Tarehe Pili Febuari Mwaka huu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwanasihi na kuwaomba Wanahabari Nchini kuendelea kushirikiana na Wataalamu wa Afya na washirika wengine  kwa kutumia Taaluma zao kuielimisha Jamii juu ya masuala ya kinga, ugunduzi wa mapema wa saratani ili kuweza kudhibiti ongezeko la ugonjwa huo hapa Zanzibar.

Mapema Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dr. Fadhil Mohamed Abdulla alisema mazoezi kama hayo ni muendelezo wa muda mrefu wa utoaji wa mafunzo ya jinsi ya kujikinga na maradhi yasiyoambukiza hapa Nchini.

Dr. Fadhil alisema Mchango mkkubwa wa Taasisi na Jumuiya zisizo za Kiserikali za ndani na nje ya Nchi umesaidia kwa kiasi kikubwa mapambano dhidi ya kuondosha maradhi ya Saratani za Matiti hapa Nchini.

Mkurugenzi huyo wa Idara ya Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman  kwa kuwa mshirika muhimu wa masuala mengi ya Kijamii wakati alipokuwa Mkuu wa Wilaya na baadaye Mkuu wa Mkoa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.