Habari za Punde

China Imeipongeza SMZ Katika Kumarisha Sekta za Maendeleo Ikiwemo Mikakati ya Kuimarisha Uchumi wa Buluu.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China anayefanyika Kazi zake Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng, alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo 19-5-2021, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa  ya kitabu na Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China anayefanyika Kazi zake Zanzibar Mhe.Zhang Zhisheng, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na mgeni wake Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China anayefanyia kazi zake Zanzibar Mhe.Zhang Zhisheng, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar, alipofika kujitambulisha


SERIKALI ya Jamhuri ya Watu wa China imepongezwa kwa kuendeleza utamaduni wake wa kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo mikakati iliyowekwa katika kuimarisha uchumi wa Buluu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa pongezi hizo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China  Zhang Zhisheng, aliyefika Ikulu kwa ajili ya Kujitambulisha.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa Jamhuri  ya Watu wa China ni mdau muhimu wa maendeleo ya Zanzibar kwani imekuwa ikiiunga mkono Zanzibar tokea miaka ya 60 mara baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.

Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi huyo mdogo wa China anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Zhang Zhisheng kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamani sana juhudi za Serikali ya China katika kuunga mkono miradi mbali mbali ya maendeleo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Jamhuri ya Watu wa China imeweza kuunga mkono sekta mbali mbali za maendeleo hapa Zanzibar ikiwemo afya, elimu, kilimo, viwanda  na nyenginezo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi  alieleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar ina furahishwa na juhudi za nchi hiyo za kuendeleza uhusiano na ushirikiano wake katika kuendeleza na kuimarisha sekta za maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Jamhuri ya Watu wa China katika kuhakikisha sekta za maendeleo zinaimarika sambamba na kuimarisha udugu na urafiki uliopo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi huyo mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika suala zima la ujenzi wa Bandari mpya ya Mangwapwani na kuwakaribisha wawekezaji pamoja na Kampuni kutoka China kuja kuekeza Zanzibar.

Mapema Balozi mdogo wa China Zhang Zhisheng alimueleza Dk. Mwinyi kuwa Jamhuri ya Watu wa China inathamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na kuahidi kuendeleza kwa manufaa ya pande zote mbili.

Balozi Zhisheng alimueleza Rais Dk. Mwinyi kuwa Jamhuri ya Watu wa China iko tayari kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza uchumi wake kupitia dira ya uchumi wa buluu pamoja na kulipokea wazo la kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini humo.

Katika maelezo hayo, Balozi huyo alieleza kwamba China ni miongoni mwa nchi za mwanzo  kuyatambua  Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, na kuanzia hapo ikiwa nchi ya kwanza kuleta wataalamu wakiwemo madaktari wa fani mbali mbali pamoja na wataalamu wa sekta za maendeleo na viwanda wakiwemo wataalamu wa kilimo.

Balozi Zhisheng alitumia fursa hiyo kumpongeza kwa mara nyengine tena Rais Dk. Mwinyi kwa niaba wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Xi Jinping kwa kuchaguliwa na wananchi wa Zanzibar kuwa Rais wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kishindo.

Aidha, Balozi Zhisheng alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kusimamia vyema  Serikali ya Umoja wa Kitaifa anayoiongoza na kueleza matumaini yake ya kwamba Zanzibar itapiga hatua kubwa ya maendeleo kutokana na mshirikiano makubwa yaliopo.

Pamoja na hayo, Balozi huyo amemuahidi Rais Dk. Mwinyi kwamba watalii kutoka Jamhuri ya Watu wa China wataongezeka kwa wingi kuja kuitembelea Zanzibar kwani kinachozuia hivi sasa ni kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa COVID 19 duniani.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.