Waziri
wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza
wakati Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikiwasilisha taarifa kuhusu
huduma za mawasiliano na intaneti kwa Wabunge, Bungeni Dodoma. Kulia ni Naibu
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson na
katikati ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Seleman
Kakoso.
Naibu
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson (kulia)
akifunga kikao cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania baada ya kuwasilisha taarifa
kuhusu huduma za mawasiliano na intaneti kwa Wabunge Bungeni Dodoma. Kushoto ni
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile na
katikati ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Seleman
Kakoso.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula
(kushoto) akifuatilia wasilisho la Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA), Dkt. Jabir Kuwe kuhusu huduma za mawasiliano na intaneti kwa Wabunge
Bungeni, Dodoma. Anayefuata ni Mkurugenzi Msaidizi wa Tathmini na Ufuatiliaji
wa Wizara hiyo, Elisa Mbise.
Baadhi ya Wabunge wakifuatilia wasilisho la Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA), Dkt. Jabri Kuwe (hayupo pichani) kuhusu huduma za mawasiliano
na intaneti kwa Wabunge Bungeni, Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia
ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile
Na Prisca Ulomi, WMTH.
Waziri wa Mawasiliano
na Teknolojia ya
Habari, Dkt Faustine Ndugulile amesema kuwa Wizara yake iko mbioni kupeleka Bungeni muswada
utakaowezesha kutungwa kwa Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi iili kulinda faragha na taarifa
za mwananchi
Dkt. Ndugulile ameyasema hayo kwenye ukumbi wa Bunge, Dodoma wakati akijibu mijadala mbalimbali iliyotolewa na Wabunge kwenye semina iliyotolewa kwao kuhusu huduma za mawasiliano na intaneti ili waweze kufahamu namna Wizara inavyotekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini yake
Ameongeza kuwa Wizara inaandaa sheria hiyo ili kulinda faragha na taarifa binafsi za wananchi katika hatua ya ukusanyaji wa taarifa, usafirishaji, matumizi na utunzaji wa taarifa hizo kwa kuwa taasisi mbalimbali zinatumia taarifa husika hivyo amewataka Wabunge kuwa tayari pindi pendekezo la muswada litakapowasilishwa Bungeni ili sheria hiyo iweze kutungwa kwa maslahi mapana ya taifa
“Hivi sasa ujambazi umehama kutoka silaha za mkononi na kuhamia mtandaoni, Serikali itaendelea kuelimisha wananchi, kuboresha mifumo na teknolojia ili nchi iwe mbele zaidi katika kudhibiti uhalifu mtandaoni,” amesisitiza Dkt. Ndugulile
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Seleman Kakoso ameishauri Serikali iongezee fedha za kuuwezesha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kutoa ruzuku ya kutosha kwa kampuni za simu ili mawasiliano yafike kwa wananchi wote ikiwemo kuongeza usikivu wa redio kwenye maeneo ya mipakani
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Akson aliipongeza Wizara kwa kuleta semina hiyo kwa Wabunge na anatamani katika kipindi kifupi Wabunge wasizungumzie changamoto ya mawasiliano katika maeneo yao kwa kuwa mawasiliano ni huduma ya msingi kama ilivyo maji, barabara
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabir Kuwe amesema kuwa nchi inaelekea kutumia huduma ya 5G na majaribio yatafanyika ili kuhakikisha kasi ya teknolojia inayotakiwa inapatikana ili kuongeza huduma ya mawasiliano ya data nchini
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
No comments:
Post a Comment