Habari za Punde

SMZ Inaendelea Kuutafutia Ufumbuzi wa Mgogoro wa Kampuni ya Master Life Microfinance Ltd na Kuweza Kuwasaidia Waathirika.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali  Mwinyi (katikati) akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na  Wawakilishi wa Waathirika wa Kampuni ya Masterlife waliofika  leo Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo nao.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaaendelea kuutafutia  uvumbuzi mgogoro wa Kampuni ya Masterlife Microfinance Ltdili kuweza kuwasaidia waathirika.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo ikulu Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na wawakilishi wa waathirika wa Kampuni ya Masterlife Microfinance Ltd iliyokuwa ikiendesha shughuli za kifedha hapa Zanzibar  kinyume na sheria na taratibu za nchi.

Alisema kuwa juhudi hizo zinaendelea kuchukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kukaa na uongozi wa Kampuni hiyo ya Masterlife ambayo ilikushanya fedha nyingi za wananchi kinyume na taratibu za nchi ambapo fedha zilizopatikana kutoka kwa Kampuni hiyo hadhikidhi malipo kwa waathirika.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa taarifa zilizotolewa na uongozi wa Mastarlife ni watu  11,000tu ambao wametoa fedha zao na sio watu 39,000 idadi iliyotolewa hapo mwanzo na Maofisa wa Wizara ya Fedha.

Alisema kuwa kwa upande wake ana nia njema kwani ameapa kuwatendea haki wananchi wa Zanzibar na hayuko tayari kuona mwananchi hata mmoja anadhulumiwa.

Alisema kuwa yeye kwa upande wake angependa jambo hilo liishe kwa salama kwani anatambua kwamba ana dhima kubwa kwa wananchi wa Zanzibar na kueleza kuwakilichokuwa kikifanyika sio mfumo wa ‘Musharakah’ kama ilivyoelezwa na waathirika hao bali uliokuwa ukifanyika ni mfumo wa  ‘Pyramid Scheme’.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kilichokuwa kikifanywa na Kampuni ya Masterlife hakikubaliki katika jamii na yeye kwa upande wake bado anaendelea na mazungumzo na Kampuni hiyo katika kuhakikisha fedha za watu zinarudi kwani walioathirika ni wengi.

Alisema kuwa Serikali haina nia ya mwananchi hata mmoja kuikosa fedha zake na kilichokuwepo ambacho ilipelekea Serikali kuisimamisha Kampuni hiyo ni kuona kwamba watu wengi wangejiunga na hatimae kukosa haki zao.

Alisema kuwa kwa kawaida hakuna biashara inayoweza kumpa mtu faida ya asilimia mia pale mwanzoni kwa miezi mitatu na hakuna faida inayoweza kumpa mtu faida ya asilimia 50 kwa miezi mitatu.

Alisema kuwa Serikali haikuwa na nia ya watu wadhulumiwe ama wapoteze fedha zao kwani Kampuni hiyo haikuwa na biashara itakayotoa faida ya kuwapa watu.

Aliongeza kuwa biashara zilizokuwa zikiendeshwa na Kampuni hiyo hazikuwa na lengo zuri la kutoa faida kwa watu na hata kiwango kinachotolewa cha watu waliojiunga na Kampunin hiyo si chauhakika. 

Alisema kuwa anachotafuta hivi sasa ni kupata ufumbuzi kabla ya yeye kuchukua hatua na ameahidi kulifuatilia suala hilo mpaka watu wapate fedha zao.

Alieleza kuwa azma ni kulifanyia kazi suala hilo na kusema kwamba uvamizi uliofanyika katika Kampuni hiyo ulifanwya kwa lengo la kuhakikisha angalau kilichokuwepo kiweze kupatikana ambapo fedha zilizopatikana hazikufika hata Bilioni 5licha ya kukusanya fedha nyingi za watu.

Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba jambo hilo ni kubwa sana na watu waliochukuliwa fedha zao ni 11,000 ambao ni wengi sana licha ya idadi ya awali iliyotolewa na Maofisa wa Wizara kuwa ni watu 39,000 lakini hata hivyo ni watu wengi kwa Zanzibar.

Alisema kuwa taarifa aliyoitoa kwa wananchi mnamo Aprili 6,2021 ni kwa ajili ya kuutahadharisha umma kutokana na mchezo huo mchafu uliokuwa ukifanywana Kampunin hiyo kwani kila mtu alikuwa anataka kupeleka fedha yake ambapo hali hiyo ingeachiwa ingeliathiri watu wengi zaidi.

Alisema kwamba kurejewa rejewa taarifa hiyo katika vyombo vya habari ilikuwa na nia ya kwamba watu wasidanganyike kupeleka fedha kwa Kampuni nyengine kama hiyo ambayo tayari ilikuwepo na ilikuwa ikikusanya fedha za watu kwa njia ya simu.

Alisisistiza kwamba kikubwa kilichokuwepo hivi sasa ni kuhakikisha fedha za watu zilizokusanywa na Kampuni hiyo zinarudishwa kwani watu wamepoteza fedha zao nyingi.

Alisema miongoni mwa mambo aliyoyafanya ni kuviita vyombo vya Sheria na kuwapa maelekezo ya kwamba ni vyema watu wa Kampuni hiyo watafutwe wahusika ili wawalipe watu pesa zao kwanza na baadae mengine yafuate.

Rais Dk. Mwinyi alieleza juhudi alizozichukua katika kuhakikisha taratibu za kifedha zinafanywa lakini akasisitiza ni kuhakikisha fedha hizo zinarudii na baada ya hapon ndio masuala mengine yatafuata kama vile ushauri.

Waathirika hao kwa upande wao walitoa shukurani zao kwa Rais Dk. Mwinyi na kueleza jinsi walivyofarajika kutokana na maelezo na maelekezo yake juu ya suala hilo na jinsi hatua za makusudi zinazochukuliwa na Serikali.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

1 comment:

  1. Ni hatua nzuri yenye matumaini. Mungu ajaalie malipo yafanyike kila mmoja apate haki yake.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.