Habari za Punde

SMZ Itatoa Maamuzi Yenye Tija Kwa Ajili ya Muendlezo wa Eneo Hilo Linalotarajiwa Kujengwa Bandari Mpya ya Mwangapwani.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Ndg.Amour Hamil Bakari, akitowa maelezo ya michoro ya Ramani ya eneo la Ujenzi wa Bandari ya Kisasa katika eneo la Mwangapwani Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja wakati wa ziara yake kujionea eneo hilo linalotarajiwa ujenzi huo na (kushoto kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe,Ayoub Mohammed Mahmoud
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Hussein Ali Mwinyiamefanya  ziara katika eneo linalotarajiwa kujengwa bandari mpya ya Magapwani na kueleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa maamuzi yenye tija kwa ajili ya muendelezo wa eneo hilo.

Rais  Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo, mara baada ya kufanya ziara ya kulitembelea eneo linalotarajiwa kujengwa bandari mpya ya Mangapwani, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo pia, alitembelea miradi ambayo imeanza kabla ya ujenzi huo mpya.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali itakuja na maamuzi yenye tija ambayo yatasaidia kwa pande sote mbili ikiwemo upande wa wawekezaji ambao walianza kuekeza kwa muda mrefu katika eneo hilo pamoja na kwa upande wa Serikali kwa ujumla huku akiwataka wawekezaji hao kuwa na subira .

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali imeridhishwa na ukubwa wa eneo pamoja na hatua ya awali iliyofikiwa na kuelez ajambo kubwa lililompelekea kufanya ziara hiyo hivi leo ikiwa ni kwenda kujiridhisha  na kulielewa vyema eneo hilo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliwasisitiza wawekezaji hao kuwa na subira huku akisema kwamba atahakikisha jambo hilo linakwenda kwa haraka na ameahidi kukaa na wahusika mapema iwezekanavyo kwa azma hiyo hiyo ya kuharakisha mradi huo.

Alitumia fusra hiyo kutoa shukurani kwa wananchi wa eneo hilo kwa utayari wao waliouonesha kwa kuruhusu maendeleo kwa kushirikiana na Serikali yao kwa kuupisha mradi huo mkubwa wa bandari.

Pia, Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa wataalamu pamoja na washauri elekezi kwa kumaliza hatua ya mwanzo kwa kipindi cha miezi mitatu huku akieleza hatua zitakazofuata hivi sasa sambamba na maamuzi yatakayochukuliwa.

Aliongeza kwamba Serikali inafanya juhudi hizo kwa kuamini kwamba hivi sasa Bandari ya Malindi haikidhi haja tena  na ndio maanaimeamua kuanzisha mradi huo mkubwa wa Bandari ya Mangapwani kwa maendeleo ya Zanzibar.

Katika ziara yake hiyo, Rais Dk. Mwinyi alitembelea eneo la mradi wa Chelezo, Mradi wa Island Petroleum, Mradi wa Salama International Company na eneo la Mradi wa TP Invetment Depot na kupata maelezo kutoka kwa viongozi wa Serikali na wawekezaji.

Akiwa katika eneo hilo, Mapema alipata maelezo ya mradi huo kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Amour Hamil Bakari ambaye alimueleza namna ya michoro ya mradi huo zinavyoelekeza huku Katibu Tawala wa Mkoa huo wa Kaskazini Unguja Makame Machano Haji akieleza namna walivyoshirikiana na mshauri elekezi kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Nao wawekezaji wa eneo hilo ambao walianza kuekeza miradi yao kabla ya kuanzishwa kwa mradi huo mkubwa kwa nyakati tofauti walimueleza Rais Dk. Mwinyi hatua walizofikia katika miradi yao huku wakionesha utayari wao wa kuendelea kushirikiana na Serikali.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud alitumia fursa hiyo kumkaribisha Rais Dk. Mwinyi katika Mkoa huo pamoja na kueleza hatua zilizofikiwa na mradi huo kwa mashirikiano na wataalamu wa Wizara husika wakiongozwa na Waziri wa Wizara hiyo Rahma Kassim Ali.

Mnamo Mei 07, 2021 Rais Dk. Mwinyi alipokea Mpango wa ujenzi wa Bandari ya kisasa ya Mangapwani kutoka Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman (OIA), chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo Sheikh Mohammed Al Tooq ambapo mradi huo unahusisha maeneo makuu matatu, ikiwemo ujenzi wa Bandari mbali mbali, mji wa kisasa wa makaazi pamoja na Mpango wa kuiendeleza Bandari ya Malindi ili iweze kutumika kama Bandari ya utalii.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.