Habari za Punde

Bodaboda waaswa kutoshiriki Uhalifu

 

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo akizungumza katika Mkutano Maalumu na Waendesha Mabasi, Daladala, Bajaji na Bodaboda uliofanyika leo jijini Arusha huku changamoto mbalimbali zilijadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.
Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 

Na Mwandishi Wetu

Serikali imewaasa madereva wa bodaboda nchini kutoshiriki matendo ya uhalifu ikiwemo usafirishaji wa wahamiaji haramu,dawa za kulevya,mauaji na uporaji wa vitu mbalimbali huku ikisisitiza atakayematwa akishiriki matendo hayo atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo wakati  akizungumza katika Kikao Maalumu kilichowashirikisha madereva wa bodaboda, daladala na bajaji  ambapo changamoto mbalimbali zilijadiliwa ikiwemo ushiriki wa bodaboda kwenye matukio ya uhalifu,kuzidisha upakiaji wa abiria katika vyombo hivyo vya usafiri na Jeshi la Polisi kutoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva hao ili kupunguza matukio ya ajali yanayopelekea ulemavu na vifo.

“Nawaasa bodaboda kuachana na matendo ya kihalifu,serikali tunawategemea sana vijana kama nguvu kazi lakini kuna baadhi ya vijana sio wote wanatumika katika matukio ya uhalifu ikiwemo ujambazi,dawa za kulevya na wengine wakitumika huko mipakani kusafirisha wahamiaji haramu sasa tusizitumie bodaboda zikaleta sura mbaya  kama chombo cha kutumika kufanya uhalifu wakati lengo lake ni kutumika kujikwamua kiuchumi” alisema Naibu Waziri Khamis Hamza Chilo

Akizungumza katika Mkutano huo Mbunge wa Arusha Mjini,Mrisho Gambo amewaomba bodaboda kutii sheria za usalama barabarani huku wakisubiri mapendekezo ya Bunge kuhusiana na kila kosa kutozwa Shilingi Elfu Kumi yapitishwe

“Serikali imesikia kilio chenu cha muda mrefu cha kushushiwa gharama ya faini kutokana na makosa ya barabarani tunamshukuru Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kusikia kilio chenu nawaomba sasa mfuate sheria za usalama barabarani mkishirikiana na Jeshi la Polisi” alisema Gambo

Kwa upande wake Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamanda wa Polisi Mmoa wa Arusha.Kamishna Msaidizi wa Polisi Justine Maseji amewaonya  watu wanaoshiriki matendo ya kuteka na kuwaua madereva bodaboda huku likionya kwa yoyote anayejaribu kucheza na Maisha ya watanzania kushughulikiwa ipasavyo.

“Mpaka mwezi wa tatu tumekamata pikipiki sitini,nitoe onyo kali kwa watu wanaopora mali za wananchi waache kufanya mambo ya ovyo ovyo tutachukua hatua kali,mtu anayetafuta dozi sisi tutapeleka dozi kali zaidi na wao wahalifu wanafahamu maana sio kila kitu tunaweka wazi wanazijua ‘sindano’ tunazopeleka”alisema ACP Justine.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.