Waziri
wa Nishati Tanzania, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, akizungumza na Waandishi wa
Habari, mara baada ya Mawaziri wa nchi tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi
zinazohusika na Mradi wa Umeme wa Rusumo kumaliza mkutano wao uliofanyika
tarehe 12 Juni, 2021 mara baada ya kutembelea eneo la Mradi na kuridhishwa na
hatua ya ujenzi iliyofikiwa na wakandarasi.Kushoto
kwa Waziri wa Nishati Tanzania, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, ni Waziri wa
Miundombinu Rwanda, Mhe. Balozi Claver
Gatete.
Waziri wa Nishati Tanzania, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, ( wa pili kutoka kushoto) akimuuliza swali Mhandisi Mshauri Bosco Mugabo anayesimamia ujenzi wa kituo cha kufua Umeme cha Rusumo kuhusu ukamilishaji wa ujenzi wa Bwawa la Mradi wa Umeme wa Rusumo.Kulia kwa Dkt. Kalemani ni Waziri wa Miundombinu Rwanda, Mhe. Balozi Claver Gatete na Waziri wa Nishati na Migodi wa Burundi Mhe. Ibrahim Uwizeye.
Na Dorina G. Makaya - Ngara
Waziri
wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani amesema, Mradi wa Umeme wa Rusumo
utakamilika Desemba, 2021.
Waziri
Kalemani ametoa taarifa hiyo tarehe 12 Juni, 2021 katika mkutano na waandishi
wa habari baada ya kumaliza kikao cha pamoja cha Mawaziri wa nchi tatu za
Tanzania, Rwanda na Burundi zinazohusika na Mradi wa Umeme wa Rusumo
kilichofanyika katika eneo la mradi la Rusumo.
Waziri
Kalemani ameeleza kuwa, Mawaziri wa nchi zote tatu zinazohusika na Mradi wa
Rusumo, Waziri wa Nishati na Migodi wa Burundi, Mhe. Ibrahim Uwizeye, Waziri wa
Miundombinu Mhe. Balozi Claver Gatete pamoja
na yeye mwenyewe Waziri wa Nishati wa Tanzania,
wameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Rusumo ambao
ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 80.
Aidha,
Dkt. Kalemani amebainisha kuwa, handaki la kupitishia maji yanayotoka kwenye
bwawa kwenda kwenye mitambo ya kuzalisha umeme lenye urefu wa mita 703 tayari limekamilika
kwa asilimia 80 tarehe 12 mwezi Juni, 2021.
Waziri
Kalemani ameeleza kuwa, njia za kusafirisha umeme zitagharimu dola milioni
113.2 na kuwa, baada ya kukamilika ujenzi zitaokolewa dola milioni 25 ambazo
zitatumika katika kujengea njia nyingine ya umeme kwa nchi zote tatu ili
kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika nchi hizo.
Amebainisha
kuwa, jumla ya shilingi bilioni 10 za kitanzania zimetumika kwa ajili ya miradi
ya kijamii katika wilaya ya ngara kwa upande wa Tanzania, ambapo miradi hiyo
inahusisha ujenzi wa vituo vya afya viwili, ujenzi wa zahanati mbili, ujenzi wa
shule za sekondari 3, ujenzi wa shule za msingi mbili, ujenzi wa chuo cha
ufundi stadi na ujenzi wa miradi miwili ya maji pamoja na miradi ya kilimo na
ufugaji wa nyuki. inayowanufaisha wakazi wa wilaya ya Ngara
Dkt.
Kalemani ametoa wito kwa watumiaji wa maji ya mto Rubuvu na mto Kagera, kutumia
maji ya mito hiyo kwa uangalifu pamoja na kutunza vyanzo vya mito hiyo ili
Mradi wa Umeme wa Rusumo usipungukiwe na maji huku akibainisha kuwa, upo uwezekano
wa kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme wa Mradi wa Umeme wa Rusumo .
Ziara
hiyo ililenga kutembelea mradi huo na kuona maendeleo yake pamoja na kutoa
maelekezo kwa wakandarasi kuhusiana na
umuhimu wa kukamilishwa kwa ujenzi wa Mradi huo kama ilivyopangwa.
Mawaziri
kutoka Tanzania, Rwanda na Burundi walitembelea
eneo linapojengwa Bwawa, ( Dam site), Eneo la kuzalisha umeme ( Power
House), na Eneo la kupokea umeme kabla haujasambazwa ( Switch yard) na
kuridhishwa na kasi ya ujenzi.
Waziri
Kalemani amesema, Mradi wa Umeme wa Rusumo ni
muhimu sana na kukamilika kwake kutaondoa changamoto nyingi za umeme na
kuwa baada ya kikao cha pamoja cha Mawaziri wa nchi zote tatu, wamewataka
wakandarasi hao ifikapo mwezi Desemba, 2021 wawe wamekabidhi Mradi na wananchi
waanze kutumia umeme unaotokana na Mradi huo wa Umeme wa Rusumo.
Mradi
wa umeme wa Maporomoko ya maji Rusumo ulianza mwezi Machi 2017 na utazalisha MW
80 ambapo nchi tatu husika za Tanzania, Rwanda na Burundi zitapata mgao sawa wa
MW 27 zitakazoingizwa kwenye gridi ya Taifa kwa kila nchi.
Katika
ziara hiyo Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani, aliambata na Kamishna
Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga, wataalamu kutoka Wizara ya Nishati
na TANESCO pamoja na Uongozi wa Serikali wa Wilaya ya Ngara.
No comments:
Post a Comment