Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi Amewataka Waumini wa Kiislam Waliokusudia Kwenda Kuhijj Makka kwa Mwaka Huu Badala Yake Wajipange Kwa Mwakani.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kutowa salamu kwa Wananchi wa Kijiji cha Unguja Ukuu, baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Masjid Nour Unguja Ukuu Kae Pwani Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaeleza wananchi wa Zanzibar kwamba mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka jana hapatakuwa na fursa ya kwenda kuhiji Makka kwa wale waumini wote waliokusudia kufanya ibada hiyona badala yake wajipange kwa mwakani.

Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa salamu zake kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na wananchi wote mara baada ya Sala ya Ijumaa huko Masjid Nour, Unguja Ukuu Kae Pwani, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika salamu hizo Alhaj Dk. Mwinyi alisema kutokana na taarifa iliyotolewa na Serikali ya Saud Arabia inayosema kuwa kwa hali ya ugonjwa wa COVID 19 bado mwaka huu hawatoruhusu mahujaji kutoka nje na watakaoruhusiwa ni wale raia wa Saudi Arabia na wageni wanaoishi nchini humo.

Hivyo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatoa taarifa rasmi kwa wananchi kwamba na mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka jana hapatakuwa na fursa hiyo ya kwenda kuhiji nchini humo.

Aliongeza kuwa kabla ya kutolewa taarifa hiyo na Serikali ya Saud Arabia, tayari alikwisha kutoa taarifa kwa wananchi kwamba mahujaji wote watakaoshiriki ibada hiyo mwaka huu  kutoka hapa nchini watapatiwa chanjo kwa wale watakaopenda kuchanjwa.

Kutokana na hali hiyo, Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba ni vyema waumini hao wakajipanga vyema kwenda kufanya ibada hiyo hapo mwakani kutokana na uwezekano mkubwa wa gharama za Hijja kuongezeka.

Hivyo Alhaj Dk. Mwinyi aliwataka wale wote waliokuwa wamedhamiria kufanya ibada hiyo mwaka jana na wale wa mwaka huu waendelee kujipanga zaidi kwenda kufanya ibada hiyomwakani kwa vile washatia nia na Mwenyezi Mungu atawaikubalia nia yao.

“...lakini kama tunavyoambiwa na Masheikh kwamba jambo ukishalitilia nia basi Mwenyezi Mungu anakuandikia thawabu zake...basi tunamuomba Mwenyezi Mungu wale wote waliotia nia mwaka jana na mwaka huu wawe wamepata thawabu za kuhiji kama walivyokuwa wametia nia....na tunaomba Mwenyezi Mungu atujaalie sote wale waliotia nia na sie tunaotegemea kutia nia basi tuweze kuipata Hija ya mwakani na miaka inayokuja”,alisema Alhaj Mwinyi.

Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi amewataka wana siasa, viongozi wa dini pamoja na vyombo vya habari kuhakikisha kwa pamoja wanahubiri amani.

Alifahamaisha kwamba kauli zinazotolewa na wanasiasa, viongozi wa dini na vyombo vya habariwakati wote zihakikishe zina jenga amani kwani kinyume yake zinaweza kuiondosha amani iliyopo.

Alisema kuwa kuna nchi nyingi duniani amani yake imeondoka kutokana na kauli za wanasiasa, viongozi wa dini ama vyombo vya habari.

Hivyo, Alhaj Mwinyi alieleza kwamba wananachi wote wana wajibu wa kuhakikisha wanadumisha amani na kusisitiza kwamba  ajenda ya amani iwe ni ajenda ya kudumu.

Alisema kwamba maendeleo yote yanayotarajiwa kufanyika nchini bila ya amani hayawezi kupatikana, hivyo amani ni vyema ikahubiriwa kila wakati.

Alhaj Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa uongozi wa msikiti huo kwa mapokezi mazuri waliyompa huku akiahaidi kushirikiana nao katika ukamilishaji wa ujenzi wa msikiti wao huo ambao umedumu kwamuda mrefu katika ujenzi wake.

Nae Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume aliwaeleza waumini hao wa Unguja Ukuu kwamba Alhaj Dk. Mwinyi amekuwa na hikma kubwa jambo ambalo linajidhihirisha kwa jinsi anavyowapenda wananchi wake kwa kushirikiana nao katika sala za Ijumaa katika misikiti mbali mbali hapa nchini.

Hivyo, aliwataka waumini hao pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kuendelea kumuombea dua ili Mwenyezi Mungu aendelee kumpa wepesi wa kutekeleza vyema yale yote aliyoyakusudia na yale aliyowaahidi wananchi wake.

Mapema akisoma hotuba ya Sala ya Ijumaa Khatibu wa Msikiti huo Sheikh Ramadhan Rajab Mtoro alieleza haja kwa waumini wa dini ya Kiislamu kutilia mkazo malezi bora ya watoto.

Akitoa neno la shukurani kwa Rais, Sheikh Ramadhan Rajab Mtoro alitoa pongezi kwa Alhaj Dk. Mwinyi kwa hatua yake ya kwenda kijijini kwao na kusali nao pamoja huku wakimuombea dua kwa Mwenyezi Mungu aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Pamoja na hayo, Sheikh Mtoro alitoa ombi maalum kwa Alhaj Dk. Mwinyi la kushirikiana nao katika ukamilishaji wa ujenzi wa msikiti wao huo ambao ujenzi wake tayari umedumu kwa miaka 16 hivi sasa lakini bado haujamaliza, ombi ambalo Alhaj Dk. Mwinyi alilipokea mikono miwili.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.