Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman akisalimiana na Balozi wa Switzeland Nchini Tanzania Mhe.Didier Chasot alipowasili katika ukumbi wa mkutano Ofisini kwake Migombani Jijini Zanzibar kwa mazungumzo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe, Othman Masoud Othman akizungumza na Balozi wa Switzerland Nchini Tanzania.Mhe.Didier Chasot, kwa mazungumzo yaliofanyika ofisini kwake Migombani jijini Zanzibar kwa lengo la kuendeleza ziara yake yenye lengo la kukuza uhusiano wake na Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe, Othman Masoud Othman akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Switzerland Nchini Tanzania.Mhe.Didier Chasot,baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika ofisini kwake Migombani jijini Zanzibar.
Na.OMWR.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Switzerland katika kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa masuala ya rushwa na uhujumu uchumi itakayoisaidia serikali kuandaa mbinu bora za kupambana na wahalifu wa rushwa nchini.
Mheshimiwa Othman aliyasema hayo wakati akizungumza na Balozi wa Switzerland nchini Tanzania, Bwana Didier Chasot, aliyefika ofisini kwake Migombani jijini Zanzibar kwa lengo la kuendeleza ziara yake yenye lengo la kukuza uhusiano wake na Zanzibar.
Mheshimiwa Othman amesema serikali imeandaa mfumo huo kwa lengo la kuhakikisha kuwa Zanzibar inaendelea kufanikisha mapambano dhidi ya rushwa pamoja na kuzuia matumizi ya mali zinazopatikana kwa njia haramu.
Amesema mfumo huo unaotumika katika nchi mbali mbali duniani, umekuwa ni chachu ya kupambana na tatizo hilo hali iliyopelekea kuendelea kwa nchi hizo.
Aidha amesema tayari Switzerland imeingia makubaliano ya awali na Mamlaka ya Kuzuiwa na Kupambana na Rushwa Zanzibar (ZAECA) kwa ajili ya kujenga uwezo katika eneo la kuzifuatilia mali za watu waliopatikana na hatia ya uhalifu chini ya sheria zinazoambatana na rushwa na uhujumu uchumi.
Akizungumzia swala la utawala bora, Mheshimiwa Othman alisema: "Serikali imejipanga katika kujenga uwezo wa taasisi mbali mbali na kutoa mafunzo kwa watendaji wa taasisi hizo pamoja na kuandaa mpango wa urekebishaji wa baadhi ya sheria zinazohusika na usimamizi wa masuala mbali mbali nchini".
"Kabla ya kukutana nami, Balozi huyu alikutana na Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi, hivyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakaa na kuangalia maeneo muhimu zaidi ya kuweza kushirikiana na Serikali ya Switzerland kwa hatua za utekelezaji", alieleza Makamu huyo wa Kwanza wa Rais.
Naye, Balozi Didier amesema wataendelea kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kushirikiana na jumuiya zisizo za kiserikali kwa lengo la kuwajengea uwezo vijana ili kupambana na ukosefu wa ajira, kuimarisha sekta ya afya pamoja na uwezeshaji wa Serikali katika kusimamia utawala bora.
No comments:
Post a Comment