Habari za Punde

Uzinduzi wa Kituo Cha Ubunifu wa Programu ya Kituo Cha Sayansi Skuli ya Jangombe.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Simai Mohammed Said akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa Kituo cha Programu ya Ubunifu katika Kituo cha Skuli ya Sekondari Jangombe Wilaya ya Mjini. uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Skuli hiyo Jangombe Jijini Zanzibar.





Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said  amewataka waangalizi wa vituo vya ubunifu wa kisayansi kuitumia fursa walionayo ili kufika malengo ya Serikali waliyojiwekea.


Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Programu katika kituo cha ubunifu wa Kisayansi Jang'ombe Wilaya ya Mjini Unguja  amesema vituo hivyo vitakapotunzwa vitadumu na kuzalisha wataalamu wa fani mbalimbali.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha Taifa linapunguza changamoto ya  upungufu wa wataalamu wa sayansi nchini.

Amesema nchi nyingi zimepiga hatua kutokana na matumizi mazuri ya Sayansi na Teknolojia, hivyo amewataka walimu kuwa tayari kuzalisha wajuzi wa fani hiyo ili Taifa  nalo liendelee kupiga hatua kutokana na taaluma hiyo.

Aidha amewasisitiza wazazi nao kuhakikisha wanashirikiana na Walimu kwa lengo la kuwasaidia watoto wao kufikia ndoto zao za kimaisha ikiwemo kuweza kuingia katika soko la ajira haraka kutokana na taaluma zao katika sayansi.

Aidha amewataka  Wanafunzi kuwa na jitihada na kulipenda somo la ubunifu (fine art) kwani litasaidia kuweza kujiajiri wenyewe hapo baadae ambapo amemtaka Mkurugenzi Idara ya Elimu Sekondari kuandaa utaratibu maalum wa mashindano ya kituo cha kisayansi kinachofanya vizuri zaidi ili kutengeza ushindani wa masomo hayo. 

Nae Mkurugenzi Idara ya Mipango Sera na Utafiti Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar  bwana Khalid Masoud Waziri akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara hiyo amesema ujenzi wa vituo hivyo ni miongoni mwa jitihada na ahadi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kuboresha elimu ili  Taifa lizalishe  wataalamu wazalendo.

Amesema pia lengo la ujenzi wa vituo hivyo ni kuhakikisha wanazalisha wabunifu mbalimbali  hasa wa Sayansi na kuinua kiwango cha ufaulu kwa masomo hayo.

Nae Mwakilishi wa jimbo la Jan'gombe mhe Ali Abdul Gulam Hussein amesema ni jambo la faraja kuona kwenye jimbo lake kuna kituo cha ubunifu hivyo anesema yupo tayari kuongeza nguvu ili jimbo lake liwe na historia ya kutengeneza wanasayansi wazalendo.

Jumla ya vituo 21 vya ubunifu wa kisayansi vimejengwa nchini ambavyo 14 vipo Unguja na 7 kwa upande wa Pemba ambapo kauli mbiu ni "Ubunifu ndio ufunguo wa  fursa ya maendeleo".

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.