Habari za Punde

Wabunge Wataka "Luku " za Maji (Mita za Malipo ya Kabla ) Ziharakishwe.

 *Wabunge Wataka Luku za Maji (Mita za Malipo ya Kabla) Ziharakishwe*

*Waipongeza Wizara ya Maji kwa kuliwekea mkazo suala hilo

*Wasema ndiyo mwarobaini wa kumaliza malalamiko ya bili za maji

*Majaribio kuanza nyumba za wabunge kati ya Julai hadi Septemba  mwaka huu

Na.Jamvila Habari Updates.

Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wameipongeza Wizara ya Maji kwa kulipa msukomo suala la mita za malipo ya kabla (Prepaid Meters) na kuitaka kuharakisha suala hilo ili kuondoa malalamiko ya wananchi kuhusu bili kubwa za maji na bili bambikizi.

Wajumbe hao wamesema hayo wakati wakichangia katika kikao cha Kamati hiyo na Watendaji wa Wizara akiwemo Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi, Katibu Mkuu wa Maji, Mhandisi Antony Sanga, na Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Nadhifa Kemikimba, kuhusu masula ya Ankara za maji.

Akichangia mjadala huo Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, alisema anaipongeza Wizara kwa hatua hiyo na kusema kuwa maamuzi hayo yamechelewa sana.

“Naunga mkono mawazo haya kwasababu huu ndo mwarobaini wa malalamiko ya wananchi kuhusu kubambikiwa bili na mimi hili suala lilipoanza niliweka hizi mita na naitumia ina tija kubwa sana,” alisema Gambo.

Naye Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde alisema anaunga mkono wazo hilo lakini yeye akatofautiana na Gambo katika suala la kugharamia mita hizo kwa kupendekeza kuwa Serikali ibebe mzigo huo kwani baada ya muda itapata fedha kupitia mita hizo.

Kwa Upande wake naibu Waziri wa maji Mhandisi Maryprisca Mahundi ameeleza kuwa wananchi watakaokuwa wanatumia huduma hiyo ni wale wale wa maisha ya kawaida na wa chini kama ilivyo kwa luku za umeme.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Alieleza kuwa Mita hizo za Malipo ya Kabla Zitakuwa Zinafanya kazi kama Ving'amuzi na watumiaji watakuwa na uwezo wa kudhibiti matumizi kwa simu za mkononi, pamoja na kupata taarifa zote ikiwemo matumizi ya maji na kasi ya utumiaji.

"Pre Paid ambazo tunaziunga ni zile zinazofanya kazi kama Ving'amuzi na watakaokuwa wanafunga hizi mita za maji tumezungumza nao na wamekubali kufungua kiwanda hapa nchini" Alieleza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Antony Sanga

Akizungumza mara baada ya kusikiliza maoni ya Wabunge,Waziri wa Maji, Jumaa Aweso aliwatoa hofu wabunge kuhusu utekelezaji wa suala hilo na kusema pamoja na kwamba mwanzo huwa unatia hofu lakini hawana sababu ya kuogopa.

"Kuhusu gharama za mita za Malipo ya Kabla Wizara  itaanda utaratibu wa kuita wadau huru wanaohusika tuzungumze nao ili kuweza kupata mita za gharama nafuu kadiri inavyowezekana" Aliongeza Waziri Awesso

Aidha Waziri Awesso amependekeza  utaratibuwa mita hizi kuanza na viongozi wa Serikali na Wabunge ili iwasaidie kujifunza namna ya kwenda kuutekeleza kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.