Habari za Punde

Zanzibar Imeanzisha Sera Maalum Kwa Ajili ya Kuendeleza Uwekezaji Kuimarisha Uchumi Wake

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akizungumza na  mgeni wake Balozi wa Qatar nchini Tanzania Mhe.Hussain Ahmad Al Humaid wakati alipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo katika mazungumzo yao walisisitiza uhusiano katika kukuza Uchumi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akimsikiliza mgeni wake Balozi wa Qatar nchini Tanzania Mhe.Hussain Ahmad Al Humaid wakati   wa mazungumzo yaliyofanyika leo alipofika Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameiomba Serikali ya Qatar  kuwashajiisha Wawekezaji wa nchi hiyo kuja nchini kuwekeza katika sekta za Utalii, Uvuvi pamoja na mafuta na Gesi.   

Dk. Mwinyi ametoa ombi hilo Ikulu jijini Zanzibar, alipozungumza na Balozi wa Qatar nchini Tanzania Hussain Ahmad Al Humaid, aliefika kujitambulisha.

Amesema tayari Zanzibar imeanzisha Sera maalum kwa ajili ya kuendeleza Uwekezaji, ikiwa ni hatua ya kuimarisha uchumi wake.

Rais Dk. Mwinyi aliiomba nchi hiyo kuangalia uwezekano wa kuisaidia Zanzibar katika uimarishaji wa sekta za Maji, Afya pamoja na elimu.

Alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya nchi mbili hizo, na kubainisha umuhimu wa  hatua hiyo kuendelezwa katika sekta binafsi.

Aidha, Dk. Mwinyi alisema kuwepo kwa safari za Ndege kati ya Zanzibar na Qatar ni fursa muhimu ya kuendeleza biashara kati ya nchi mbili hizo, na kuiomba Qatar kuweka mazingira bora ya soko la bidhaa mbali mbali.

Katika hatua nyengina, Dk. Mwinyi alimshukuru Balozi huyo kwa utayari wake wa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kuwashajihisha wawekezaji wa nchi hiyo kuja nchini kuwekeza.

Aidha, aliiomba Serikali ya Qatar kutoa taarifa  za ujio wa wana familia ya Kifalme katika shughuli za kitalii mapema iwezekanavyo, ili waweze kupata hadhi wanazostahili.

Vile vile aliitakia mafanikio mema nchi hiyo katika maandalizi  ya  Kombe la Dunia yanayoendelea,  ambapo fainali zake zitafanyika mwaka 2022.

Nae, Balozi  Humaid aliahidi Serikali ya Qatar kukuza uhusiano na kuendeleza ushirikiano uliopo katika yake na Zanzibar katika sekta mbali mbali za kijamii, ikiwemo elimu, maji na Afya.

Alisema nchi hiyo imekuwa ikitoa watalii wengi wanaozitembelea nchi mbali mbali duniani ikiwemo Zanzibar, miongoni mwao  wakitoka katika Familia ya Kifalme.

Aliahidi kubeba dhima ya kuwashajihisha wawekezaji wa nchi hiyo kuja nchini kuwekeza, ikiwa hatua ya kukuza ushirikiano uliopo.

Aidha, alimuomba Mwenyezi Mungu kuondokana na ugonjwa wa Corona unaoikabili Dunia hivi sasa, ili nchi hiyo iweze kukamilisha maandalizi yanayoendelea ya  Kombe la Dunia.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.