Habari za Punde

Zanzibar Itaendeleza Ushirikiano Wake wa Kihistoria na Oman Pamoja na Kushirikiana Kibiashara Kiuchumi na Kijamii.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Balozi Mdogo wa Oman anayefanyika Kazi zake Zanzibar Mhe.Said Salim Al Sinawi, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha rasmin leo, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza mgeni wake Balozi Mdogo wa Oman anayefanyika Kazi zake Zanzibar Mhe. Said Salim Al Sinawi, alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano wake wa kihistoria kati yake ya Oman ikiwa ni pamoja na kushirikiana kibiashara, kiuchumi na kijamii.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa Oman anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Said Salim Alsinawi ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alimkaribisha Zanzibar Balozi  Alsinawi na kumuhakikishia kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake wote wataendeleza uhusiano na ushirikiano na Oman ambao ni wa kihistoria.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimuhakikishia Balozi huyo mdogo wa Oman anayefanya kazi zake hapa Zanzibar kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano na Oman kwani inathamini sana juhudi za Ubalozi huo za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi mbali mbali ya maendeleo.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na Oman na inatambua hatua na juhudi mbali mbali inazozichukua Serikali ya Oman katika kuiunga mkono Zanzibar hivi sasa ikiwa ni pamoja na kusaidia ujenzi wa Jumba la Beit Al Jaib pamoja na Jumba la Wananchi “Peoples Palace”, lililopo Forodhani

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ujenzi huo una umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Zanzibar huku akisisitiza kwamba kuna kila sababu ya kuzitunza nyumba za Mji Mkongwe wa Zanzibar kutokana na haiba yake.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi huyo kwamba uwepo wa Kampuni ya ndege ya Oman Air yenye kufanya safari kati ya Zanzibar na Oman kumeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha biashara kati ya pande mbili hizo huku akisisitiza kwamba Zanzibar ina bidhaa nyingi zenye soko nchini Oman.

Mapema, Balozi Mdogo wa  Oman anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Said Salim Alsinawi alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Serikali Oman iko tayari kuendeleza ushirikiano wake na Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuiunga mkono katika kumarisha miradi yake ya maendeleo.

Balozi huyo Mdogo wa Oman alimueleza Rais Dk. Mwiny kwamba, Serikali ya Oman inatambua uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliopo kati ya Oman na Zanzibar pamoja na watu wake hivyo, nchi yake itaimarisha zaidi mahusiano yaliopo.

Aidha, Balozi huyo alieleza kuwa Oman inathamini uhusiano na ushirikiano huo wa kihistoria uliopo na inatambua juhudi kubwa anazozichukua Rais Dk. Mwinyi za kuiletea Zanzibar maendeleo hivyo haina budi kumuunga mkono ili kufikia lengo lake alilolikusudia.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.