Habari za Punde

ZEC Yapongezwa Kwa Kazi Nzuri Kukamilisha Zoezi la Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar Mwaka 2020.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikabidhiwa Ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ya Mwaka 2020 na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Mhe.Jaji mstaafu Hamid Mahmoud Hamid, hafla hiyo imefanyika katika Ofisi ya Makamu Vuga Jijini Zanzibar. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiipongeza Tume ya uchaguzi Zanzibar kwa kazi nzuri ya kufanikisha uchaguzi wa mwaka 2020 wakati tume hiyo ilipokabidhi ripoti yake kwake.

Na.Abdi Kassim . OMPR.                                                                                                                              Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameipongeza tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa kazi nzuri waliofanya ya kukamilisha vyema zoezi la uchaguzi uliofanyika Oktoba mwaka jana.                                                                                                           

Mhe. Hemed alieleza hayo wakati akipokea ripoti ya uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2020 iliowasilishwa na Mwenyekiti wa tume hiyo akiambatana na wajumbe tume hiyo waliofika Ofisi kwake Vuga Jijini Zanzibar.

Alisema Tume ya uchaguzi Zanzibar imefanya kazi zake kwa uweledi na umahiri kutokana na kuzingatia sheria zinavyowakeza jambo ambalo limesaidia wananchi kujenga Imani dhidi ya watendaji wa tume hiyo.

Alifafanua kwamba kazi nzuri iliofanywa na watendaji ni ya kupigiwa mfano sambamba na kutoa ishara kwamba kupitia zoezi la uwendeshaji wa uchaguzi nchi nyengine kutoka Barani Afrika wanaweza kuja Zanzibar kujifunza namna bora ya kuendesha uchaguzi kuanzia hatua za awali za kuwaandikisha wapiga kura.

Aliwahakikishia kwamba yeye akiwa mtendaji mkuu wa shughuli za serikali ataendelea kutoa kila aina ya ushirikiano unaohitajika katika kufanikisha kazi za tume kutokana na Imani kubwa alionayo kwa viongozi wa tume.

“Mimi binafsi ni shuhuda wa kazi nzuri mulioifanya naendelea kuwapongeza na kuwashukuru kwa kazi nzito kutokana na kulikamisha vyema jukumu mulilokabidhiwa na Nchi yetu” Alisema Mh. Hemed

Alieleza licha ya changamoto zilizosababishwa na baadhi ya wanasiasa kutaka kuvuruga zoezi hilo lakini ubobezi na ufanisi wa watendani wa tume wakiongozwa na Makamishna, wameweza kuzikabili pamoja na kuzitatua changamoto hizo jambo ambalo limeonesha utayari na uweledi waliokuwanao watendaji wake.

Akiwasilisha ripoti hiyo Mwenyekti wa Tume ya Uchaguz Zanzibar (ZEC) Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Tume imeamua kukabidhi ripoti kwake kwa kutambua kuwa Makamu wa Pili wa Rais ndio kiongozi mkuu wa shughuli za Serikali lakini pia  kimuundo tume ya uchaguzi  Zanzibar ipo chini ya Ofisi ya Makamu  wa Pili wa Rais.

Mwenyekiti huyo wa Tume ya uchaguzi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa tume inatoa shukrani zake za dhati kwa serikali kwa ushirikiano wake katika kuiwezesha tume hiyo kufanikisha kazi zake.

Akibainisha mafanikio ya tume Jaji Mstafu Hamid Mahmoud alisema kwa mara ya kwanza tume imefanikiwa kuchapisha kura hapa hapa visiawani Zanzibar pamoja na kufanikiwa kutoa matokeo ya uchaguzi ndani ya kipindi cha masaa ishirini na nne (24).

Alieleza pamoja na mafanikio hayo lakini tume ilikabiliwa na baadhi ya changamoto katika baadhi ya maeneo ikiwemo changamoto ya kuwekewa vizuri kwa watendaji wake kuweza kufika katika vituo vya kuendesha zoezi la uchaguzi.

“Mhe. Makamu wa Pili wa Rais watendaji wetu walipata shida ya kusafirisha masanduku ya kura katika maeneo ya visiwa lakini pia katika maeneo mengine waliwekewa vizuwizi pamoja na kushambuliwa” Alieleza Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi

Ripoti hiyo iliowasilishwa kwa Makamu wa Pili wa Rais imeelezea kwa kina hali ya Uchaguzi ilivyo kabla, wakat na baada ya uchaguzi, ikihusisha mafaniko na baadhi ya changamoto zilizoikumba tume hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.