Habari za Punde

Kamati za Pamoja za SMT na SMZ Kukutana Zanzibar Kujadili Masuala Mbalimbali ya Muungano.

 Na.Issa Mzee  - Maelezo Zanzibar.

Kamati ya pamoja ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoshughulikia masuala ya Muungano inatarajia kufanya vikao kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya Muungano nchini.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Suleiman Jafo, huko Vuga Mjini Unguja kuhusu kikao cha kamati ya pamoja inayoshughulikia Muungano, alisema Mawaziri na Makatibu Wakuu wa pande zote mbili wapo Zanzibar kwa ajili ya vikao hivyo.

Alieleza kuwa, vikao hivyo vinatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa wiki hii, amabapo tarehe 23 mwezi huu kutakuwa na kikao cha Mawaziri wa serikali zote mbili mahsusi kwa ajili ya kujadili masuala ya Muungano.

Alisema kuwa marabaada ya kikao hicho cha Mawaziri wa SMT na SMZ, wajumbe watapata fursa ya kutembelea miradi ya kimkakati ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amanai Karume (terminal III), na kiwanda cha Maziwa cha Bakhresa Fumba, ambayo ni miongoni wa hoja za Muungano ambazo zimekuwa zikitafutiwa ufumbuzi na kamati ya pamoja.

 Waziri Jafo alihamisha kuwa, tarehe 24 mwezi huu kutakuwa na kikao cha kamati ya pamoja ya SMT na SMZ, katika ukumbi wa sheikh Idriss Abdul-wakil ambapo mwenyekiti wa kikao hicho atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Philip Mpango, na Wajumbe wengine akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

“Ni matumaini yetu kuwa kupitia vikao hivi tutapata ufumbuzi wa hoja mbalimbali zinazotukabili katika utekelezaji wa masuala ya muungano” alisema Waziri huyo.

Alifahamisha ya kwamba, mara baada ya kikao hicho kutakuwa na utiaji saini wa hati za makubaliano ya hoja zilizopatiwa ufumbuzi katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi.

Alisema tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa kushughulikia hoja za muungano kupitia vikao vya kamati ya pamoja mwaka 2006, hoja 25 zimejadiliwa na mpaka sasa hoja saba tayari zimepatiwa ufumbuzi na hoja kumi na nane zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi.

Alifafanua kuwa, hoja mbili zilizopatiwa ufumbuzi zilisainiwa hati za makubaliano katika kikao cha mwaka 2010 na kuondolewa katika orodha ya hoja za Muungano.

Akizitaja hoja hizo, alisema moja ni Utekelezaji wa Sheria za Haki za Binaadamu Zanzibar, na Utekelezaji wa Sheria ya Mechant Shiping Act katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha aliendelea kwa kusema katika kikao kilichofanyika oktoba mwaka jana, hoja tano zilizopatiwa ufumbuzi zilisainiwa hati za makubaliano na kuondolewa katika orodha ya hoja za Muungano.

Alisema hoja hizo ni Ushirikishwaji wa Serikali ya Zanzibar kwenye masuala ya Kimataifa na kikanda, Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Gharama za kushusha mizigo Bandari ya Daresalaam kwa mizigo inayotoka Zanzibar, Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia, na Uratibu wa Vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya kushughulikia masuala ya Muungano.

Alifahamisha kuwa,lengo la kuweka utaratibu huu ni kuimarisha Muungano wetu kwa kuhakikisha kuwa changamoto zote zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais, Dk.Saada Mkuya alisema majadiliano ya hoja mbalimbali yatafanyika katika vikao hivyo ili kupata ufumbuzi wa mambo mbali mbali katika Muungano.

Alisema kuwa ufumbuzi utakaopatikana utasaidia katika kuimarisha nyanja mbalimbali kwa maendeleo ya taifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.