Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Mohamed Mwalimu
(kushoto) na Meneja Masoko wa Zantel-Zanzibar, Rukia Mtingwa (pembeni)
wakimsikiliza mfanyabiashara akielezea biashara yake katika warsha ya
biashara-mtandao (e-commerce) iliyofanyika Kisonge Zanzibar.
Wafanyabiashara
wa Zanzibar wameaswa kutumia vyema wigo wa biashara ya mtandaoni (e-commerce)
kuuza na kutangaza bidhaa zao katika masoko ya ndani na nje ya nchi ili kukuza
biashara zao na mitaji.
Hii
ni kutokana na kuwa na uwanja mpana wa masoko ya mtandaoni kwa wafanyabiashara
kuuza bidhaa na huduma zao katika muda mfupi na kwa gharama ndogo za
uendeshaji.
Meneja
Masoko wa Zantel-Zanzibar, Rukia Mtingwa
alisema wakati wa warsha ya Biashara-Mtandao iliyoandaliwa na Zantel kujadili
fursa na changamoto za biashara za mitandaoni kwamba; wafanyabiashara watapata
wateja wengi wapya kutoka masoko mapya ya mtandaoni na kuongeza mauzo yao na
mitaji.
Warsha
hii ya siku mbili iliyofanyika Agosti 14 na 15, 2021 Zanzibar, iliwaleta pamoja
wawakilishi wa serikali, wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa biashara.
Wafanyabiashara pia walipata fursa ya kuonyesha na kutangaza bidhaa zao
mbalimbali.
“Kwa
kutumia simu ya mkononi au kompyuta yako, unaweza kutangaza bidhaa au huduma
yako kupitia kurasa zote za mitandao ya kijamii kama WhatsApp, Instagram,
Facebook, Twitter na YouTube. Pia unaweza kufungua duka lako mtandaoni na
ukauza bidhaa zako katika masoko ya ndani na nje ya Zanzibar,” alisema.
Aliongeza
“Biashara-mtandao pia huokoa muda na kupunguza gharama za uendeshaji. Mfano,
ukiwa na duka la mtandaoni, hauna haja ya kukodi eneo la kufanyia biashara;
maana unaweza kuwa na bidhaa nyumbani kwako au kwenye chombo cha usafiri na
ukafanya biashara yako vizuri sana.”
Kwa
walio na biashara zao masokoni, wakulima na wavuvi; wanaweza kutangaza biashara
zao mtandaoni na kuelekeza wateja wao mahala walipo.
“Warsha
hii ni muendelezo wa kuiishi dhamira ya Zantel, ambayo inalenga kuendeleza
matumizi ya intaneti na mfumo wa kidijitali katika masoko yetu. Tunaendelea kuboresha mtandao wetu wa
intaneti kutoka kasi ya 2G na 3G na kuweka mtandao wa 4G katika baadhi ya
maeneo,” alisema.
Warsha
hii pia ni muendelezo wa kampeni yake kabambe ya PASUA ANGA KI ZANTEL 4G inayolenga
kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa intaneti katika kuchochea maendeleo ya
kijamii na kiuchumi.
Akizungumza
kwa niaba ya Mkurugenzi wa Biashara na Masoko kutoka Wizara ya Biashara na
Maendeleo ya Viwanda – Zanzibar, Khamis Shauri, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala
wa Vipimo Mohamed Mwalim alisema warsha hii ya biashara za kimtandao
(e-commerce) ni mwanzo mzuri wa kusaidia kukuza sekta ya biashara nchini.
Aliwaasa
wafanyabiashara kutumia vyema wigo mpana wa soko la kimtandao ambalo kwa mujibu
wa takwimu za za Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), idadi ya Watanzania wanaotumia
mtandao wa intaneti imeongezeka kutoka milioni 26,83 mwaka 2020 hadi milioni
29.07 mwezi Aprili 2021.
“Biashara
za mitandao zinasaidia wafanyabiashara kupata idadi kubwa ya wateja, urahisi wa
kutangaza biashara, kupata bidhaa kwa manunuzi, kuokoa wakati na gharama
ndogo,” alisema.
Aliongeza
“Kulingana na mlipuko wa janga la ugonjwa wa mapafu (Covid-19), dunia yote
imehamishia biashara zake kwenye mitandao ambapo biashara hufanyika bila mteja
na muuzaji kukutana. Hivyo, ni lazima na sisi wana Zanzibar tubadilike”
Kutokana
na umuhimu wa e-commerce, alisema, serikali imeweka sheria na miongozo
mbalimbali ili kuweza kuboresha na kusimamia ufanyaji wa biashara za aina hiyo.
No comments:
Post a Comment