Habari za Punde

Watatu Waswekwa kwa Ubadhirifu wa Fedha za Telesenta Sengerema.

 

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew akilinganisha taarifa ya manunuzi ya vifaa vya Telesenta iliyoonesha kuna bakaa ya Milioni 27.2 kati ya shilingi Milioni 103 na taarifa ya benki ya akaunti ya kituo hicho iliyoonesha hakuna fedha iliyopo. Anayefuata ni Mbunge wa Sengerema Mhe. Hamis Tabasamu.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew akikagua sifa (specifications) na ubora wa moja ya kompyuta 19 zilizonunuliwa katika Telesenta ya Sengerema kwa ufadhili wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Richard.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew akipitia taarifa ya manunuzi ya vifaa vya kituo Telesenta ya Sengerema. Kulia ni Mkuu wa Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Mhandisi Albert Richard.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew akikagua sifa (specifications) na ubora wa moja ya kompyuta 19 zilizonunuliwa katika Telesenta ya Sengerema kwa ufadhili wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Richard.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (wa nne kulia) akipitia taarifa ya manunuzi ya vifaa vya kituo cha Telesenta ya Sengerema. Wa nne kushoto anayeelekeza ni meneja wa Kituo hicho Sostenes Tangalo


Na Faraja Mpina, SENGEREMA

Watumishi watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema wanaosimamia Redio Sengerema 98.8 FM wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa ubadhirifu wa shilingi Milioni 27,720,000 ikiwa ni bakaa ya shilingi Milioni 103 zilizotolewa na taasisi ya mawasiliano ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa ajili ya kuboresha Telesenta ya Sengerema 


Maamuzi hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew baada ya kufika katika Telesenta hiyo na kusomewa taarifa ya matumizi ya fedha hizo iliyoonesha kuna bakaa ya shilingi Milioni 27,720,000 huku taarifa ya kibenki ya akaunti ya kituo hicho ikionesha fedha zote zimetumika na hakuna bakaa yeyote 


Aidha, baada ya Mhandisi Kundo kuhoji kwanini taarifa ya kibenki inakinzana na taarifa waliyomsomea ndipo Meneja wa Kituo hicho Sostenes Tangalo kukiri kuwa wakati kituo kinapatiwa fedha na UCSAF suala la kurekebisha studio ya redio halikuwepo lakini katika manunuzi hayo ambayo yalifanyika kwa malipo ya fedha taslimu yaani cash wao wakaona wanunue na vifaa vya kurekebisha studio hiyo pamoja na samani 


Baada ya maelezo hayo kuonesha kuna harufu ya ubadhirifu wa fedha za Serikali zilizotolewa na taasisi ya UCSAF ambayo ipo chini ya Wizara hiyo Mhandisi Kundo ameagiza Meneja wa Kituo hicho Sostenes Tangalo, mwanasheria Ilambona Mahuba na Afisa Habari kuwekwa ndani na taratibu za kisheria zifuatwe bila kukiukwa ikiwa ni pamoja na watuhumiwa hao kupewa haki ya kusikilizwa pasipo manyanyaso ya aina yeyote


Sambamba na hilo ametoa maelekezo kwa uongozi wa Wilaya hiyo kuunda kamati maalum ya kuchunguza mchakato mzima wa manunuzi yaliyofanyika itakayowahusisha Ofisi ya TAKUKURU, Usalama, OCD na Wataalam wa TEHAMA na Manunuzi katika wilaya hiyo na taarifa sahihi kuwasilishwa Wizarani


Katika hatua nyingine Mhandisi Kundo ameutaka uongozi wa Wilaya hiyo kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili kupatiwa leseni ya kuendelea kurusha matangazo ya redio hiyo kwasababu leseni zinazotolewa huwa zina muda wa kutumika lakini pamoja na juhudi za TCRA kuwasiliana na uongozi wa redio Sengerema kwa ajili ya taratibu za kufuata zinazohusu leseni uongozi huo umekuwa ukikaa kimya


Mhandisi Kundo amezungumza hayo kujibu changamoto ya kusitishiwa leseni ya kurusha matangazo ya redio hiyo na TCRA iliyowasilishwa na Mbunge wa jimbo la Sengerema Mhe. Hamis Tabasamu 


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.