Habari za Punde

Tamko la Waziri Dkt.Gwajima Kuelekeza Siku ya Kimataifa ya Wazee Oktoba Mosi.2021

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akiwasalimia wananchi waliokuja kupata huduma katika Zahanati ya Sukamahela Wilayani Manyoni Mkoani Singida wakati alipotembelea Makazi ya Wazee ya Sukamahela kuelekea Siku ya Wazee Duniani Oktoba Mosi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na mzee William Mbogoni alipotembelea Makazi ya Wazee ya Sukamahela Wilayani Manyoni Mkoani Singida kuelekea Siku ya Wazee Duniani Oktoba Mosi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akikagua upatikanaji wa dawa katika Zahanati ya Sukamahela Wilayani Manyoni Mkoani Singida, alipotembelea Makazi ya Wazee ya Sukamahela kuelekea Siku ya Wazee Duniani Oktoba Mosi.

Baadhi ya Wazee wanaoishi katika Makazi ya Wazee ya Sukamahela Wilayani Manyoni Mkoani Singida wakimsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alipokuwa akitoa tamko kuelekea Siku ya Wazee Duniani Oktoba Mosi.

Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW

Na Mwandishi Wetu Manyoni

Serikali imesema ipo katika hatua za mwisho za Mapitio ya Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 kwa kushirikiana na wadau na imeendelea kutekeleza afua mbalimbali zinazolenga  kutatua changamoto zinazowakabili Wazee.

Hayo yamesemwa Wilayani Manyoni Mkoani Singida na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima  alipotembelea Makazi ya Wazee wasiojiweza ya Sukamahela kuelekea Siku ya Wazee Duniani Oktoba Mosi.

Waziri Dkt. Gwajima ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuboresha maisha ya wazee hapa nchini ili kuhakikisha wanapata huduma jumuishi na stahiki kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao, ikiwemo kuboresha utoaji wa huduma kwa wazee kuwa ni moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ameongeza kuwa Maadhimisho haya kwa mwaka huu 2021 yatafanyika katika ngazi za mikoa na yataongozwa na  Kauli Mbiu isemayo:“Matumizi Sahihi ya Kidigitali kwa Ustawi wa Rika Zote”.

"Sherehe za maadhimisho ya siku ya wazee itahusisha huduma mbalimbali kama vile wazee kupima  presha, kisukari, tezi dume, huduma za msaada wa kisaikolojia na elimu kuhusu kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 pamoja na kuhamasisha wazee na wananchi kupata chanjo." alisema Dkt Gwajima

Katika hatua nyingine Waziri Dkt Gwajima ameiagiza mikoa ya Rukwa na Njombe kuunda Mabaraza ya Wazee ya Mikoa hiyo ili kuwezesha kuanzishwa kwa Baraza la Taifa la Wazee litakalosaidia kuleta wazee pamoja katika mijadala mbalimbali na kuweka mikakati ya kutatua changamoto zinazowakabili.

Akisoma taarifa ya Makazi ya Wazee Sukamahela Afisa Mfawidhi wa Makazi hayo Twaha Kibalula amesema kuwa Makazi hayo yanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa gari kwa ajili ya kutoa huduma kwa Wazee hao ikiwemo huduma za kiafya zinazopatikana kwenye hospitali za Wilaya na Mkoa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mhe. Rahabu Mwigwisa amemshukuru Waziri Dkt. Gwajima kwa kuwatembelea Wazee hao na amemuhakikishia kuwa Wilaya itaendelea kuwaangalia kwa ukaribu Wazee hao kwani ni tunu kwa Taifa hivyo itahakikisha wanapata huduma zote stahiki.

Akitoa salamu kwa niaba ya Wazee wenzake Mwenyekiti wa Wazee hao  Mzee Adrea Yohana amemshukuru Waziri Dkt Gwajima na Serikali kwa ujumla kwa huduma wanazozipata na kumuomba kuendelea kuboresha huduma za afya, chakula na malazi ili waweze kuishi kwa amani na furaha zaidi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.