Habari za Punde

Uzinduzi wa mradi wa kuiongezea thamani tiba asili wafanyika Zanzibar

Mkurugenzi Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar Dkt. Mayasa Salim Ali akizungumza machache na kuwakaribisha wajumbe katika uzinduzi wa mradi wa kuongezea thamani tiba asili, hafla iliyofanyika Ukumbi wa Mkutano Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar.
Mwenyekiti Baraza la Tiba Asili Profesa Hamis M. Malebo akitoa maelezo kuhusu  mradi wa kuongezea thamani tiba asili, wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika Ukumbi wa Mkutano Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar.
Dkt.  Afua Mohammed akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Dkt. Rahma S. Mahfoudh katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa kuongezea thamani tiba asili huko Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar.
Mkurugenzi Tiba  Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia, na Watoto Amour Suleiman Mohamed akizindua mradi wa wa kuongezea thamani tiba asili, huko Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar.

Mratibu Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt Khalfan Amour akizungumza wakati wa  Uzinduzi wa mradi wa kuiongezea thamani  tiba asili hafla iliyofanyika Ukumbi wa Mkutano Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar.

PICHA NA FAUZIA MUSSA – MAELEZO ZANZIBAR


Na Sabiha Khamis   Maelezo   24/09/2021

Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar (ZAHRI) imetakiwa kuendeleza kufanya utafiti wa dawa za asili ili zitumike kwa usahihi katika kutibu maradhi yasiyoambukiza.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Uongezaji wa Thamani  Tiba za Mimea ya asili katika kutibu maradhi yasiyoambukiza ofisini kwake Mnazi Moja, Mkurugenzi Tiba kutoka Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Dk. Amour Suleiman Mohamed, amesema tafiti zinazofanywa zitawasaidia wanajamii kutibu maradhi ya kuambukiza kwa usahihi na kuepuka kubahatisha.

 Alisema kuwa, idadi kubwa ya wanajamii hutumia dawa za asili bila kuwa na elimu na kipimo sahihi jambo ambalo husababisha madhara makubwa kwa afya zao.

Alisema ili kuiepusha jamii na madhara hayo, ipo haja ya kutoa elimu juu ya viwango na matumizi sahihi ya dawa hizo ili kuleta matoke chanya ya dawa zinazotumiwa.

“Jamii hutumia dawa asili za mimea bila kiwango, kupitia tafiti hizi zitasaidia kugundua maradhi na kutumia tiba kwa kiwango kinachotakikana ili kuwasaidia wazee wetu majumbani  kuweza kutumia dawa kwa usahihi kulingana na majibu sahihi yanayotolewa na tafiti ili kuleta tija” alisema Dk Amour.

Alifahamisha kuwa, dunia ilipokumbwa na janga la Uviko 19 ambayo ni maradhi yanayoambukiza, tiba asili zilisaidia katika kupambana na janga hilo, hivyo ni vyema kuongeza jitihada katika kuzipa thamani dawa hizo  za mimea na kuzitumia kama zinavyotumika katika nchini nyengine.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Baraza la Tiba Asili Prof. Hamis Malebo amesema jamii inapaswa kupewa elimu kuhusiana na kuhifadhi na kutunza rasilimali ya  mimea dawa, kwani inamchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya afya nchini.

Vile vile ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar, kwa kuchukua fursa hii muhimu ya kuanzisha mradi huu utakaosaidia kuonesha thamani ya dawa asili zinazotokana na mimea.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.